Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) imeamua kutoa elimu kwa wananchi, katika mchakato wa kutoa vitambulisho vya uraia kwa Jiji la Dar es Salaam unaotarajiwa kuanza wakati wowote mwanzoni mwa mwezi huu.
Hayo yameelezwa na Thomas William, Meneja Mawasiliano wa Mamlaka hiyo katika semina iliyotolewa kwa waandishi wa habari hivi karibuni jijini, kwa nia ya kuboresha shughuli zote zinazohusu NIDA na kuelimisha umma kupitia vyombo vya habari.

“Kazi kubwa ya NIDA ni kutambua watu wanaoishi nchini na kuandikisha taarifa zao kwa kushirikiana na vyombo husika, kutoa vitambulisho kwa raia na wageni wenye umri wa miaka 18 na kuendelea, kusimamia utendaji kazi wa Mamlaka kwa kuzingatia utawala bora na kutunza daftari la taifa la usajili na utambuzi na kushirikishana taarifa hizo na wadau kwa maendeleo ya taifa,” alisema William.

Katika semina hiyo, ilielezwa kuwa mfumo huu wa usajili na utambuzi wa watu umeleta mabadiliko makubwa ya kiuchumi na kijamii katika serikali nyingi duniani, zilizoamua kujenga utaratibu kama huu.

Meneja Uenezi wa NIDA, Alphonce Malibiche, alisema Tanzania ni lazima iwe na chombo muhimu cha kuweka mipango na kutunza taarifa sahihi za wananchi, kwa lengo la kuleta maendeleo ya kiuchumi katika nchi yetu kama zilivyo nchi za jirani kama Kenya, zinazoendesha bajeti za taifa bila kutegemea wafadhili. Taarifa kama hizi ndizo zinazokosekana kwa sasa hapa nchini.

Alisema uandikishaji vitambulisho ni kazi endelevu kuanzia sasa, na baada ya miaka 10 vitambulisho vitabadilishwa kulingana na wakati na sura halisi ya mhusika ili kuleta urahisi wa kumtambua raia, hivyo ni lazima kila raia awe na kitambulisho na anapokipoteza atalazimika kulipia kwa ajili ya kuandaliwa kingine.

Mfumo huu wa usajili na utambuzi wa watu uliandaliwa na NIDA tangu Agosti 1, 2008. Kutokana na faida zake kwa wananchi katika kuharakisha maendeleo ya nchi na baada ya Serikali kuona umuhumu wake, ikaifanya Mamlaka hii iwe chombo cha kusimamia ujenzi huu na kutoa vitambulisho kwa Watanzania, wageni na wakimbizi wanaoishi kihalali nchini.

Kazi hii itafanywa kwa kutumia maafisa watendaji wa kata, ambao sambamba na uandikishaji watagawa anwani za makazi kwa kila nyumba na kiwanja kilichopo na taarifa zake zitaungwa kutoa huduma kwa urahisi zaidi.

NIDA inalenga kutambua nani ni nani, yuko wapi, anamiliki nini na anafanya nini. Hii itasaidia katika kupunguza riba kubwa ya mikopo inayotozwa na benki mbalimbali, kwani kwa sasa hawajui wanamkopesha nani na anaishi wapi. Lakini kwa kutumia mfumo huu, wananchi watapata urahisi wa kukopa kwa riba nafuu pamoja na wao kupata taarifa sahihi zenye tija.

Kwa kuzingatia hayo, mfumo huu wa Taifa wa usajili na utambuzi wa watu utasaidia katika kupata taarifa zinazohitajika zikilenga maeneo yafuatayo: Kiuchumi – usajili utaongeza wigo wa ukusanyaji mapato ya Serikali na kupunguza wafanyakazi hewa kwenye orodha ya watu wanaolipwa mishahara. Pia itapunguza gharama za daftari la wapiga kura.

Serikali kwa upande wake, taarifa zitakazopatikana kutokana na uandikishaji, zitaiwezesha kupanga vizuri huduma za jamii kutokana na wingi wa watu kutambulika kwa uhalisia. Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) nayo itapata fursa ya kupata taarifa sahihi za wanafunzi wanaostahili na wasio stahili mikopo.

Suala la usalama kwa kupambana na ugaidi wa kimataifa na kupunguza uhalifu nchini, pia kwa utambuzi wa wananchi wote litakuwa rahisi. Taarifa zote za Watanzania, wageni na wakimbizi zitakuwa katika daftari la kumbukumbu la kielektroniki na taarifa sahihi ndiyo kigezo muhimu cha kufanya uamuzi na kuleta maendeleo, kitu kinachokosekana kwa sasa.

Kwa kuwa dafati la wapigakura linatakiwa kusafishwa mara mbili kabla ya Uchaguzi Mkuu, kwa maana hiyo hakutakuwa na gharama za kulisafisha kwani taarifa sahihi zitapatikana kwa urahisi kupitia vitambulisho vya uraia.

Faida nyingine ni katika mifuko ya hifadhi za jamii kama mfumo wa Bima ya Afya, PPF, NSSF na PSPF. Hizi zitatumia taarifa zilizo katika mfumo wa Taifa wa usajili na utambuzi wa watu katika kuwatambua wanaonufaika na mifuko hiyo.

Katika hatua nyingine, NIDA inafanya kazi sambamba na RITA kujua kuwa mdahiliwa anatakiwa kuthibitisha umri wake kuwa ni miaka 18 au zaidi, kwa kuwa taarifa sahihi za umri wa mhusika zinapatikana.

Kufanikisha ujenzi wa mfumo wa Taifa wa usajili na utambuzi wa watu, NIDA inatarajia kupata taarifa kutoka kwa wadau mbalimbali kama vile Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini/Ofisi ya Mrajisi (RITA/RGO), Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Kitambulisho cha Mkaazi Zanzibar na Uhamiaji.

Alivitaja vielelezo vinavyohitajika katika mchakato mzima kuwa ni pamoja na cheti cha kuzaliwa, cheti cha ubatizo/falaki, kitambulisho cha mpigakura, pasipoti ya Tanzania na cheti cha kuhitimu elimu ya msingi.

Changamoto kubwa ambayo Serikali inakutana nayo ni pale inapotokea majanga, kwa kutokuwa na utambuzi yakinifu wa wananchi wake waliopatwa na tatizo hilo, kuwalipa fidia au hata kuwasaidia kwa namna moja au nyingine inaweza ikakuta inawalipa wasiohusika.

Mfano mzuri ni mabomu ya Mbagala na Gongo la Mboto, majanga ya moto na mafuriko ya Kilosa pamoja na mafuriko yaliyolikumba Jiji la Dar es Salaam mwishoni mwa mwaka jana. Kwa kutumia mfumo huu, itakuwa rahisi kuwalipa waathirika wa majanga kwa kuwa na kumbukumbu sahihi.