Na Tatu Mohamed, JamhuriMedia, Dodoma
MKURUGENZI wa Masoko na Mawasiliano wa Shirika la Bima la Taifa (NIC), Karimu Meshack ametoa wito kwa Wakulima nchini kujiunga na Bima ya Kilimo.
Ameyasema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari kwenye maonesho ya Wakulima na Wafugaji (Nanenane) ambayo yanafanyika Kitaifa katika Viwanja vya Nzuguni, jijini Dodoma.
Amesema kuwa NIC katika maonesho hayo wamekuja na bidhaa mbalimbali ikiwemo huduma za bima za maisha, mali na ajali.
“Wakulima wanatumia fedha nyingi kuwekeza kwenye kilimo na kwamba kilimo na mifugo vimeambatana na changamoto, viashiria na majanga. Kwenye kilimo kuna mambo ya tabianchi ambapo mkulima anaweza akalima na akakutana na ukame, mvua nyingi zilizokithiri zikaharibu mazao na wadudu,” amesema.
Amebainisha kuwa, NIC inataka mkulima alime na kwamba yale majanga anayoambatana na kilimo awaachie Shirika hilo ambapo mtaji aliyowekeza kwenye kilimo usipotee huku akisema kuwa wao wanamkinga mkulima huyo na majanga yatakayotokea
“Ikitokea majanga yoyote kwenye kilimo NIC inamrudishia mkulima kile alichokuwa amekiwekeza katika kilimo na tunaanza kulinda kilimo kwenye shamba lenye ukubwa kuanzia hekta 100. NIC tunatambua wakulima wengi wanalima maeneo madogo madogo hivyo tunawaweka katika makundi, vyama vya msingi ili kupata hekta hizo ambazo zitapatiwa bima hiyo.
“Kama mkulima aliwekeza milioni 500 sisi tunamrudishia ili alime tena na akiwa hajakata bima ile milioni 500 inakuwa imepotea na itamgharimu kwenda kuitafuta ili aende akalime,” amesema na kuongeza:
“Kwahiyo tupo kwenye haya maonesho kwa ajili ya kutoa elimu na kuwashawishi wakulima waweze kujiunga na Bima ili kuweza kulima salama kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya nchi,” amesema.
Ameongeza kuwa kupitia bima hiyo tayari Mkoa wa Kilimanjaro baadhi ya wakulima wameshanufaika na bima hiyo ambapo NIC iliwalipa zaidi ya milioni 255 ili warudi shambani wakalime.
Aidha Meshack amesema kuwa mwitikio wa wakulima kwenye bima hiyo ni mkubwa kulingana na muda wa bima kuanza kutolea kwa wakulima hao.