Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla, amefuta leseni ya umiliki wa kitalu cha Lake Natron East kinachoendeshwa na Kampuni ya Green Mile Safaris (GMS).

Kwenye maelezo yake hakuwa na mengi, isipokuwa amenukuu kifungu kwenye Sheria ya Wanyamapori Na. 5 ya mwaka 2009; pia kwenye mitandao ya kijamii amesema amefanya hivyo kwa kuzingatia ‘masilahi mapana ya nchi’. Mara zote kiongozi akishatumia maneno hayo, maana yake anatutaka tusihoji. Nani ana ubavu wa kuhoji masilahi mapana ya nchi!

Siandiki kupinga uamuzi wa waziri au kuwatetea GMS, la hasha! Naandika kwa sababu ningependa Watanzania na walimwengu wajue na waheshimu kauli ya “Mnyonge mnyongeni, lakini haki yake mpeni”. Inawezekana kabisa Green Mile Safaris tukawa hatumpendi kwa sababu hii au ile, lakini kutumia visingizio na upotoshaji wa kuumba ili kumpoka kitalu, si jambo la kiungwana hata kidogo.

Tena basi, inawezekana taarifa za ‘kiintelijensia’ walizopewa wakuu wa nchi ni kuwa kampuni hii ni ya majangili, ina magaidi, inakwepa kodi, inafadhili wanaoipinga CCM na mambo mengi ya uongo ya aina hiyo. Kwa kuzingatia hayo ndiyo maana nimeona ni vema Watanzania wakawa na rekodi sahihi kuhusu sakata hili. Green Mile anapambana na nguvu kubwa ya ndani na nje ya nchi – na kwa bahati mbaya watetezi wanaogopa hata kama wanaujua ukweli. Wanaogopa kupachikwa majina mabaya. Woga ndiyo silaha dhaifu kuliko zote.

Dk. Kigwangalla, kama kweli anamwamini Mungu anatambua kuwa hicho anachokisema kuwa ni ‘masilahi mapana ya nchi’ si masilahi ya nchi, bali ni masilahi ya genge la watu na kampuni zinazoamini zina haki ya kufaidi rasilimali za nchi hii na kufanya chochote kwa wanayetaka kumkomoa.

Tena basi, kwa kuhakikisha mpango huu unakwenda ‘kisayansi’ na watu wengi wasishituke, akawatumia Mkuu wa Mkoa wa Arusha na Mkuu wa Wilaya ya Longido (wa sasa) kufanikisha hiki ambacho hatima yake imetolewa naye waziri.

Sana sana hoja aliyonayo waziri ni kuwa Green Mile anadaiwa Sh milioni 300 za vijiji! Sidhani kama madai hayo ni ya kisheria au ni ya hisani ya mwekezaji. Waziri huyu huyu anajua ni wizara hiyo hiyo iliyokuwa chini ya waziri mwenye masilahi kwenye vita ya kitalu hiki aliyeifungia Green Mile kwa miaka miwili shughuli za uwindaji. Bila shaka kwa kulitambua hilo, na kwa utu, angesema Green Mile apewe muda wa kulipa fedha hizo kama kweli ni malipo ya lazima.

Fukuto la kitalu hiki kwa awamu hii ya Kigwangalla lilianza baada ya taarifa za kuuawa twiga kwenye ukanda huo. Mara tukasikia vitisho vya mkuu wa mkoa akisema Green Mile wana dharau. Hazikupita siku nyingi tukamsikia mkuu wa wilaya akitangaza ‘kufuta’ leseni ya kampuni! Fikiria, DC anakuwa na uwezo wa kuifuta kampuni! Wenye akili walijua nini kitakachofuata. Bahati mbaya sana Mkuu wa Wilaya wa sasa Longido, ama ni mwoga kupindukia, au ni mtiifu aliye tayari kutenda kila anachoamriwa na mkuu wa mkoa bila kutafakari kwa kina.

Si vibaya ijulikane kuwa mkuu wa wilaya aliyekuwapo awali alitofautiana na mkuu wa mkoa kwa shinikizo hilo hilo la kumtaka atekeleze amri ya kuwatimua Green Mile Safaris. Nayasema haya ili Watanzania wajue suala la Lake Natron si ‘masilahi mapana ya nchi’, bali ni masilahi mapana ya viongozi kadhaa.

Machi, mwaka huu kulifanyika kikao jijini Arusha. Kikao hicho kilihudhuriwa na wadau wa utalii. Kiliwahusisha wakubwa kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii. Mada moja ilikuwa na hiki: “Investment Opportunities”. Hapo kukaorodeshwa mapori ya akiba ya Swagaswaga, Kijereshi, Mpanga-Kipengele, Mkungunero, Maswa na Pori Tengefu la Lake Natron. Wanaojua mpango huo walipotazama tu orodha hiyo wakajua kina nani wanalengwa. Nikaonya wakati huo kwa kusema walengwa wakuu hapo ni Maswa na Lake Natron. Nitaeleza mbele ya mfululizo huu.

Green Mile Safaris amepambana na wakati mgumu. Katikati ya vita ya kiuchumi, akapatikana na kashfa ya wageni wake kukiuka taratibu za uwindaji. Akafutiwa leseni kwa miaka miwili. Baadaye Wizara ya Maliasili na Utalii iliyokuwa na Waziri Profesa Jumanne Maghembe, Katibu Mkuu Meja Jenerali Gaudence Milanzi na Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori, Profesa Songorwa – watu makini na wapenda nchi – wakaiona Green Mile haina hatia kwani kosa lililofanywa waliostahili kubeba adhabu ni PH (Professional Hunter) na askari wa wanyamapori waliokuwa na wageni. Kuifungia Green Mile ilikuwa ni kumwonea mmiliki wake kwa sababu ni kama kumwadhibu mmiliki wa kampuni kwa kosa la dereva wa basi la kuvuka taa nyekundu! Busara ikaona wenye hatia ni PH na askari wa wanyamapori – mwajiriwa wa serikali.

Kufungiwa kwa kampuni hiyo kulikuwa ni furaha kubwa sana kwa Waziri wa Maliasili na Utalii wa wakati huo, Lazaro Nyalandu, ambaye aliona ni fursa pekee kwa rafiki zake aliowapenda kurejea kwenye kitalu cha Lake Natron East. Kwa ufupi ni kuwa Kampuni ya Green Mile imekuwa kwenye mapambano ya muda mrefu na Kampuni ya Marekani ya Wengert Windrose Safaris Ltd (WWS) ambayo ni mojawapo ya kampuni tanzu mbili za Friedkin Conservation Fund (FCF) zinazojihusisha na uwindaji wa kitalii hapa nchini. Kampuni nyingine ni Tanzania Game Trackes Safaris (TGTS) Ltd.

Historia ya mgogoro

Kampuni hizo ziliwasilisha maombi ya kumilikishwa vitalu  10 vya uwindaji wa kitalii kwa msimu wa mwaka 2013-2018.

Kabla ya ugawaji wa mwaka 2011 kampuni hizo zilikuwa zinamiliki vitalu 14. Vitalu vya uwindaji vilivyoombwa na vile walivyomilikishwa kampuni za Fredkin Conservation Fund kwa kipindi cha uwindaji cha 2013-2018:   

WENGERT WINDROSE SAFARIS

1. Moyowosi GR Njingwe South

2. Muhesi GR

3. Kizigo GR East

4. Kizigo GR Central

5. Lake Natron GCA (North)

  

TANZANIA GAME TRACKERS SAFARIS

LTD

1. Monduli Juu Open Area

2. Kizigo GR (West)

3. Maswa GR (Kimali)

4. Maswa GR (Mbono)

5. Ugalla GR (East)

6. Ugalla GR (West)

7. Moyowosi GR

Njingwe North

8. Makere/Uvinza FR

9. Moyowosi GR (Central)

Rekodi zinaonyesha kuwa baada ya matokeo ya ugawaji wa vitalu kampuni zote mbili (TGTS na WWS) ziliwasilisha rufaa kwa Waziri wa Maliasili na Utalii kupitia Kamati ya Ushauri wa Ugawaji Vitalu (iliyokaa Januari 2012) kutaka kufahamu sababu za kutokupewa baadhi ya vitalu walivyoomba kikiwemo cha Lake Natron Game Controlled Area (North).

Wakapewa sababu kuwa ni kutokana na ushindani mkubwa. Ushindani uliongezeka zaidi kutokana na mabadiliko ya sheria ambapo kifungu cha 39(3)(b) cha Sheria ya Kuhifadhi Wanyamapori Na. 5 ya mwaka 2009 kinataka kampuni zitakazomilikishwa vitalu; asilimia 85 ziwe zinamilikiwa na Watanzania na asilimia 15 wageni.

Kamati ilipendekeza mgawo kwa kuzingatia matakwa ya sheria na ushindani, hali ambayo ilisababisha kampuni hizo zisigawiwe vitalu vinavyokidhi idadi iliyoombwa na maeneo yaliyokuwa wamemilikishwa.

Nini kilichofuata?  Kukaibuka mgogoro wa Lake Natron Game Controlled Area (North) kutokana na WWS kutogawiwa kitalu cha Lake Natron Game Controlled Area (North) ambacho kampuni hiyo ilikuwa inakitumia hapo awali kwa shughuli za uwindaji wa kitalii. Wakapeleka malalamiko kwa Waziri wa Maliasili na Utalii. Novemba 21, 2011 Kamati ya Ushauri wa Ugawaji Vitalu ilimshauri waziri kuwa ili kusuluhisha mgogoro huo, Kampuni ya GMS igawiwe kitalu cha Ruvu Masai GCA ambacho walikiomba na Lake Natron GCA (North) wagawiwe WWS. Hata hivyo, waziri hakuafiki ushauri wa kamati. Desemba 12, 2011, Kamati ya Ushauri iliitisha kikao cha pamoja kati ya WWS na GMS kujadili uwezekano wa kutafuta muafaka wa suala la umiliki wa kitalu cha Lake Natron GCA (North).  Desemba 13, 2011 WWS ilikutana na GMS na kujadiliana makubaliano ya kibiashara juu ya kitalu chake cha Lake Natron GCA (North).

Hata hivyo, kwa mujibu wa WWS, ilibainika baadaye kuwa makubaliano hayo yasingeweza kutekelezwa kwa sababu kulikuwa na mchakato wa kuanzisha Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori ya Jamii (WMA). WWS ilidai kuwa ilikuwa imeingia mkataba wa matumizi ya ardhi na vijiji 33 katika eneo hilo hilo, hali ambayo ingesababisha mgogoro.

Kutokana na hali hiyo, WWS ilishauri Kamati ya Ushauri wa Ugawaji Vitalu iendelee kufikiria ombi lao la kubakia na kitalu hicho kwa kuzingatia sheria, mikataba na masuala ya kiikolojia. Sababu za kiikolojia zilizobainishwa na WWS ni pamoja na kupinga eneo la Lake Natron GCA North kugawanywa kuwa vitalu viwili (Lake Natron GCA (North) na Lake Natron GCA (North-South).

Idara ya Wanyamapori ilihakiki ramani za vitalu vya uwindaji wa kitalii kabla ya kuzigawa kwa kampuni zilizokuwa zimepata mgawo wa vitalu kama zilivyowasilishwa na Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori Tanzania (TAWIRI) kwenye Kamati ya Ushauri. Uhakiki wa ramani hizo ulibaini kasoro za majina ya baadhi ya vitalu ambayo hayakuzingatia uhalisia wa kijiografia na asili ya eneo, hivyo kupendekeza marekebisho ya majina hayo.

Ramani za vitalu ziligawiwa  Oktoba, 2012 kwa kampuni za uwindaji wa kitalii zikiwa na mabadiliko ya majina hayo. Baada ya mgawo ramani hizo, WWS ilikuja na hoja mpya kuwa kitalu chake cha Lake Natron GCA North-South kimebadilishwa (swapped) na kupewa Kampuni ya GMS. Ramani ya Lake Natron GCA North-South iliyofanyiwa marekebisho ya jina ilionyesha ukubwa wa kitalu ulibaki vilevile na katika eneo na daraja lilelile pamoja na

jira za mpaka (GPS coordinates) zikiwa zilezile. WWS iligeuza madai hayo mapya kuwa hoja ya msingi badala ya hoja za awali.

Baada ya hapo suala hilo likageuka kuwa mgogoro kati ya serikali, WWS na GMS kwamba kuna udanganyifu umefanyika wa kubadilisha vitalu.

Katika kikao cha  Mei 24, 2013, kati ya Idara ya Wanyamapori, WWS, GMS, TAWIRI na Kitengo cha Sheria cha Wizara; Mkuruguenzi wa GMS alitaarifu kuwa katika mojawapo ya majadiliano kati ya GMS na WWS kuwa WWS iliiomba GMS kuiuzia kitalu chake cha Lake Natron GCA North, lakini GMS ilikuwa tayari kuiuzia safari na siyo kitalu.

Baada ya GMS kukataa ombi lao, WWS ilianza kampeni za kuichafua Kampuni ya GMS ikiwa ni pamoja na tukio la Reno-Nevada, Marekani wakati kampuni hizo zikiuza safari za uwindaji wa kitalii Januari, 2015. Katika tukio hilo WWS iliifanyia fujo GMS kuwa kampuni hiyo inafanya utapeli kwa kusambaza vipeperushi vinavyopotosha kwamba inamiliki kitalu cha Lake Natron GCA North.

Hatua hiyo iliichafua GMS.

Kwa mujibu wa Sheria ya Uhifadhi Wanyamapori Na. 5 ya mwaka 2009, kampuni zote za uwindaji wa kitalii ikiwemo WWS zilitakiwa kuondoka katika vitalu  Machi 31, 2013 baada ya muhula wa umiliki wa vitalu kumalizika ili kupisha umiliki mpya ili kutekeleza mabadiliko mapya yaliyoainishwa katika sheria hiyo. Hata hivyo, WWS iligoma kuondoka na badala yake Mei 2013 iliamua kwenda mahakamani kudai haki.

Mmiliki mpya wa kitalu cha Lake Natron GCA North ambacho kilibadilishwa jina na kuwa East, Kampuni ya GMS aliwasilisha barua ya malalamiko kwa Mkurugenzi Idara ya Wanyamapori kwamba anashindwa kuendeleza kitalu pamoja na kujenga kambi ya uwindaji kwa kuwa bado WWS wamo ndani ya kitalu kinyume cha sheria.

Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori aliiandikia WWS barua ya Mei 20, 2013 ya kuiamuru kuondoka kwenye kitalu hicho katika muda wa siku tatu. Amri hiyo haikutekelezwa na badala yake WWS ilirudi kwa  Waziri wa Maliasili na Utalii ikipinga amri ya kuondoka iliyotolewa na Mkurugenzi wa Wanyamapori.  Sambamba na hatua hiyo, WWS iliwasilisha Mahakama Kuu – Kitengo cha Biashara kuomba zuio la GMS kufanya shughuli za uwindaji katika kitalu cha Lake Natron GCA East.

Waziri alimwagiza Mkurugenzi wa Wanyamapori kuitisha kikao cha wadau wote wanaohusika na mgogoro wa kitalu cha Lake Natron (GCA) (East) ili kulijadili tena suala hili. Hata hivyo, kikao hicho hakikufikia muafaka kutokana na WWS kuendelea kushikilia msimamo wa kukitaka kitalu hicho kwa gharama yoyote ile.

Katika kikao hicho nyaraka zote muhimu ziliwasilishwa ikiwemo Ripoti ya Taasisi ya Utafiti ya Wanyamapori Tanzania (TAWIRI) kuhusu Tathmini ya Vitalu vya Uwindaji wa Kitalii Tanzania toleo la 3.1 ya Februari 2011. TAWIRI ndiyo Mamlaka ya kisayansi ya utafiti wa wanyamapori Tanzania. Ikumbukwe kuwa mabadiliko ya majina hayo hayakuathiri ukubwa, mipaka na ajira (GPS coordinates) za vitalu.

Katika kikao cha  Mei 24, 2013  WWS iliwasilisha ramani ambayo inadai kuipatia TAWIRI inayoonyesha jina na mipaka kitalu cha Lake Natron GCA (North- South) ili kuthibitisha uhalali wa madai yao. Ilipohojiwa kuwa imekuwaje ipate ramani TAWIRI wakati taasisi hiyo haina mamlaka ya kutoa ramani hizo kwa kampuni za uwindaji, kampuni ya WWS ilieleza kuwa ililazimika kufanya hivyo kwa vile haikuwahi kupewa ramani ya kitalu hicho na Idara ya Wanyamapori, jambo ambalo si kweli.   Kikao hakikuridhishwa na maelezo ya WWS ambapo kampuni hiyo ilitahadharishwa kutowatumia watumishi katika ofisi za umma kupata nyaraka za serikali kinyume cha utaratibu.  WWS iliambiwa kuwa kitendo hicho ni cha ukiukwaji wa maadili na kinaashiria mazingira ya rushwa – jambo ambalo ni kosa la jinai kwa yule aliyetoa nyaraka hizo na aliyezipokea. Kampuni ya WWS iliendelea kufungua kesi mbalimbali katika Mahakama Kuu ya Ardhi na Mahakama ya Biashara bila mafanikio kama ifuatavyo:

i. Miscellaneous Land Application No. 44 of 2013 Wengert Windrose Ltd  Versus Green Mile Safari Ltd and Others.

ii. Commercial Case No. 113 of 2013 Wengert Windrose Safaris Versus  Green Mile Safari Ltd.

iii. Miscellaneous Commercial Case No. 88 of 2013 Wengert Windrose Safaris (T) Ltd Versus Green Mile Safari Ltd.

iv. Commercial Case No. 115 of 2013 Green Mile Safari Ltd Versus Wengert Windrose Safaris Ltd.

v. Miscellaneous Commercial application No. 92 of 2013 Green Mile Safari Ltd Versus Wengert Windrose Safaris Ltd.

vi. Miscellaneous Commercial Cause No. 26 of 2013 Wengert Windrose  Safaris Ltd Versus Green Mile Safari Ltd.

vii. Miscellaneous Commercial Application No. 26 of 2013 Wengert Windrose Safari Ltd Versus Awadh Ally Abdallah.

viii. Miscellaneous Commercial application No. 68 of 2014 Awadh Abdallah Versus Wengert Windrose Safari Ltd.

Ndugu zangu, ilikuwaje Green Mile ashinde kesi zote hizi kama hakuwa na haki? Ilikuwaje Green Mile ashinde rufaa zote wizarani kama kweli hakuwa na haki? Haya nitayajadili mbele ya safari.

Julai 05, 2013 Mkurugenzi wa GMS aliwasilisha malalamiko kuwa Kampuni ya WWS ilizuia wageni wa GMS wasifanye uwindaji katika kitalu cha Lake Natron GCA (East) ambako wafanyakazi wa Kampuni ya WWS waliandaa hila ya; kuyagonga magari ya GMS yakiwa na watalii; walichimba mashimo kwenye uwanja wa ndege ili kuzuia ndege za GMS zisitue; na walifunga barabara kwa magogo kuzuia magari ya wageni waliokuja kuwinda yasipite.

Sambamba na fujo hizo, Kampuni ya WWS iliwachochea wanakijiji cha Armani, Longido kufanya vurugu dhidi ya wageni wa GMS. Hali hii ilisababisha Mkuu wa  Wilaya ya Longido kuitisha kikao na wawekezaji wote na kutoa onyo dhidi ya mwekezaji yeyote ambaye angewachochea wananchi kuvuruga amani.

Julai, 2016 Wizara ya Maliasili na Utalii ilitoa taarifa kwa umma iliyosema: “Kimsingi, kampuni za FCF (WWS na TGTS) zimekuwa na tabia ya ubabe na usumbufu katika tasnia ya uwindaji wa kitalii dhidi ya kampuni nyingine na serikali. Tabia hizi zimeendelea katika sehemu mbalimbali ambapo kampuni hizi zinafanya shughuli za utalii.  Madai kuwa kampuni za FCF zinanyanyaswa na Idara ya Wanyamapori si ya kweli. Kimsingi, busara na uvumilivu mkubwa vimetumika kuendelea kufanya kazi na kampuni hizo…”

Kuhusu Green Mile Safari Ltd kurejeshewa kitalu, wizara ilisema: “Wizara ya Maliasili na Utalii iliamua kuirejeshea leseni Kampuni ya Green Mile Safari Ltd kufanya shughuli za uwindaji wa kitalii katika vitalu vyake vya Selous GR (MK1), Lake Natron GCA (East zamani North), Gonabis/Kidunda – WMA baada ya kupitia rufaa yake dhidi ya Mkurugenzi wa Wanyamapori kupinga kunyang’anywa leseni. Kampuni ya GMS ilifutiwa umiliki wa vitalu na leseni zake zote za uwindaji kupitia Taarifa ya Umma iliyotolewa Julai 11, 2014. Uamuzi huo ulifikiwa kutokana na ukiukwaji wa Sheria na Kanuni za Uwindaji wa Kitalii uliofanywa na wageni wa GMS wakati wakiwinda kwenye kitalu cha Gonabis/Kidunda WMA mwaka 2012. Matukio ya ukiukwaji yalibainishwa kupitia picha za video (DVD) iliyowasilishwa bungeni na Mhe. Peter Msigwa (Mb) wakati wa Bajeti ya Wizara ya Maliasili na Utalii mwaka 2014.

“Kampuni ya GMS kurejeshewa leseni kunatokana na hoja zilizoainishwa kwenye rufaa yake na tafsiri ya Sheria ya Wanyamapori Na. 5 ya Mwaka 2009 katika kifungu 38(12)(c) ikisomwa kwa pamoja na – kanuni ya 17 (2) (b) ya Kanuni za Uwindaji wa Kitalii za mwaka 2010 zilizofanyiwa marekebisho mwaka 2015. Hukumu ya mahakama iliyotolewa tarehe 31 Machi, 2015 na Jaji Songoro dhidi ya Kampuni ya WWS pamoja na tafsiri na ushauri kutoka kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa barua Kumb. Na. AGC/A.130/2J/9 ya tarehe 14 Desemba, 2015 aliyoeleza kuwa kifungu cha 38(12)(c)

kinampa mamlaka Waziri wa Maliasili na Utalii kufuta umiliki wa kitalu endapo mahakama itakuwa imemtia hatiani mmiliki wa kitalu.

Ni kwa msingi huu wizara ilitengua maamuzi yaliyotolewa na Mkurugenzi wa Wanyamapori na kuirejeshea haki Kampuni ya GMS kufanya shughuli zake za uwindaji wa kitalii.

“Aidha, wizara ilitoa maelekezo kuwa waliohusika na uvunjifu wa sheria, kanuni na taratibu za uwindaji zilizofanywa na wageni wa Kampuni ya GMS huko kwenye kitalu cha Gonabis/Kidunda WMA; wakiwamo askari wa Wanyamapori (waliosimamia uwindaji) pamoja na Mwindaji Bingwa (PH) wachukuliwe hatua za kisheria na kinidhamu.

Pamoja na hatua hizi, wizara ilielekeza Kampuni ya Green Mile Safari Ltd, irudi kwenye vitalu vyake na kuendelea na shughuli za uwindaji na kuwa serikali itawapatia ulinzi kila itakapohitajika.”

Kutokana na uamuzi huo, Kampuni ya WWS ilifungua shauri tarehe 25, Mei 2016 katika Makahama Kuu, Kitengo cha Biashara kuomba zuio dhidi ya utekelezaji wa amri ya wizara ya kuiamuru kuondoka katika kitalu cha Lake Natron GCA East ifikapo  Mei 31, 2016. Shauri hilo lilisikilizwa na Jaji Mwambegele, J. ambapo ombi hilo halikukubaliwa.

Wizara ya Maliasili na Utalii ikaitaka Kampuni ya WWS kuondoka mara moja katika kitalu ambacho haijamilikishwa kihalali, lakini ikaonya kuhusu jeuri; “Kwamba, FCF imewekeza nchini na kupewa hadhi ya uwekezaji mahiri (SIS) na inachangia maendeleo ya jamii. Hata hivyo, FCF ijue kuwa hadhi hii ya SIS si kibali cha kudharau uhuru wa nchi; kuvunja sheria zetu; kushawishi wananchi kuvunja sheria; na kutishia uhuru na haki za raia wa kigeni wanaoishi kihalali au kutembelea Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

“Kwamba, Tanzania ni nchi huru (sovereign state) na kwamba sheria ni msumeno, hivyo makampuni ya kigeni hayana kinga pale wanapovunja sheria za nchi.

“Kampuni za FCF ziache kuwarubuni na kuwatumia wananchi kufanya fujo (to use villagers and incite violence against competitors) kwa manufaa yao kibiashara hakikubaliki na ni uvunjaji wa sheria za nchi.

Wizara inashauri kuwa kampuni zinazojihusisha na shughuli za utalii zizingatie na kuheshimu sheria na kanuni za nchi wakati wote zinapofanya shughuli zao Tanzania.”

Ndugu zangu, kabla ya kuingia kwenye ukweli wa kinachoendelea kwenye kitalu hiki, nimeona ni vema kwanza mpate picha halisi ya mambo yalivyo. Mtafakari makala hii mkitambua kuwa hawa WWS wamekwisha kushindwa kwenye kesi zaidi ya saba mahakamani. Wameshindwa kwenye ngazi zote za rufaa katika Wizara ya Maliasili na Utalii. Siku hizi kuna visingizio vingi vya watumishi kuhongwa. Unaweza kujiuliza, hawa Green Mile kote huko wamehonga?

Usikose mwendelezo ili ujue bayana hawa WWS ni nani? Nani wanaowabeba? Malengo yao ni yapi? Nani wanafuata baada ya Green Mile? Je, mbigiri alizoacha Nyalandu katika Wizara ya Maliasili na Utalii zinaiumiza vipi wizara hii muhimu kwa uchumi wa nchi yetu? Mola akipenda tukutane Jumanne ijayo.