Wakati makada wa CCM wenye nia ya kumrithi Rais Jakaya Kikwete wakiendelea kutangaza nia zao, imedhihirika kwamba William Ngeleja naye atafanya hivyo Alhamisi wiki hii.
Taarifa ambazo gazeti hili imezinasa zinasema kwamba Ngeleja – mbunge wa Jimbo la Sengerema atatangaza nia yake kwenye Ukumbi wa Mwanza Hotel — iliyoko katikati ya jiji la Mwanza.
Ngeleja aliyewahi kuwa Naibu na Waziri kamili wa wizara ya Nishati na Madini anaamika kuwa mmojawapo wa mawaziri mihimili walioshiriki kufanikisha mafanikio ya Serikali ya Rais Kikwete katika sekta za nishati na madini, hasa baada ya kufanya mageuzi ya kisera na kisheria katika sekta hizo.
Taarifa za kuaminika kutoka mikoa ya kanda ya ziwa zinapasha kwamba watu mbalimbali kutoka katika kanda hiyo na sehemu nyingine nchini wanamiminika Mwanza ili kuhudhuria tukio hilo.
Mratibu wa maandalizi wa hafla hiyo, Geofrey Kusekwa, anasema: “Ni kweli Ngeleja atatangaza nia Alhamisi tarehe 4 Juni, mwaka huu. Kaka kila kitu kimekamilika hapa.”
Taarifa tulizozipata na kuthibitishwa na watu walio karibu na kambi ya Ngeleja kutoka jijini Mwanza, pamoja na baadhi ya wabunge na wajumbe wa NEC zimelihakikishia gazeti hili kwamba tetesi hizo ni za kweli.
“Inasemekana uamuzi huo umefikiwa baada ya mjadala mzito uliofanywa na baadhi ya wazee, vijana na makada mbalimbali wa CCM kutoka mikoa ya kanda ya ziwa wanaomuunga mkono Ngeleja,” anasema mmoja wa marafiki nwa Ngeleja.
Vyanzo vyetu vya habari vinabainisha kwamba uamuzi huo ulifikiwa ili kuipa heshima Kanda ya Ziwa ambayo ni ngome ya Ngeleja.
Ngeleja aliyetumikia Wizara ya Nishati na Madini kwa kipindi cha takribani miaka mitano anatajwa kuwa ni miongoni mwa makada vijana wachapakazi wazuri wa CCM na wenye ushawishi mkubwa na mahiri wa kujenga hoja.
Pamoja na kwamba Ngeleja hajawahi kutangaza nia yake ya kugombea urais, lakini kwa takribani miaka miwili sasa vyombo vya habari vimekuwa vikimhusisha na mbio za urais na hata CCM kumhoji juu ya mbio hizo.
Marafiki hao wa Ngeleja wanasema mipango iliyopo ni kwamba tukio hilo litafanyika kwenye hoteli hiyo na kwmaba wananchi wengi kushuhudia maelezo yaliyobeba dhamira ya kuiongoza Tanzania.
Taarifa zinasema kwamba baadhi ya makada wa CCM na wananchi kutoka maeneo mbalimbali ya Tanzania watahudhuria mkutano huo.
Ngeleja kwa sasa ni mbunge wa Sengerema tangu mwaka 2005, aliwahi kuwa Naibu Waziri wa Nishati na Madini kwa mwaka mmoja (Januari 2007-Februari 2008), na badaye akawa waziri kamili wa nishati na madini kuanzia februari 2008 hadi mei, 2012 alipojiuzuru uwaziri kufuatia kuchafuka hali ya hewa kisiasa Bungeni.