Victor Wanyama ni mmoja wa wachezaji ambao walitikisa sana katika soka kiasi cha timu kubwa kama Totttenham kumchukua katika kikosi chake, lakini leo hii Wanyama anakosa hata nafasi ya kukaa benchi pale Tottenham.
Huu ni wakati muafaka kwake kuondoka na kutafuta nafasi sehemu nyingine, kwani bado ana uwezo wa kucheza katika timu nyingi kubwa.
Wanyama alithibitisha kuwa bado ana uwezo huo katika fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) pale Misri katikati ya mwaka jana. Katika kundi lao, wanyama aliiongoza Harambee Stars dhidi ya Senegal, Algeria na Tanzania.
Lakini si Wanyama peke yake anayepaswa kutafuta klabu nyingine ya kuchezea hivi sasa. Mchezaji mwenzake wa Harambee Stars, Michael Olunga, naye anapaswa kutafuta timu nyingine ya kuchezea ingawa kwa sababu tofauti.
Kama ilivyo kwa Wanyama, Olunga pia alikuwa mmoja wa washambuliaji walioiongoza Kenya katika kinyang’anyiro cha AFCON nchini Misri mwaka jana. Ni Olunga ambaye alifunga mabao mawili Harambee Stars walipomenyana na Taifa Stars kwenye fainali hizo.
Olunga alijinyakulia sifa pale alipoisaidia timu yake ya Kashiwa Reysol kwa kufunga mabao 27 katika msimu uliopita.
Mabao hayo ndiyo yaliisaidia Kashiwa kupanda kutoka daraja la pili hadi daraja la kwanza katika ligi ya Japan.
Kabla ya kuitumikia timu hiyo, Olunga alizichezea pia Gor Mahia, Tusker FC na Thika United katika Ligi Kuu ya Kenya. Wakati Wanyama akipaswa kutafuta timu nyingine kwa sababu anaonekana hatakiwi Tottenham, Olunga anapaswa kutafuta timu kubwa kuliko anayochezea sasa, kwa sababu ameonyesha uwezo wa hali ya juu.
Wachambuzi wa soka nchini Kenya na wachezaji wa zamani wote wanakubaliana na hoja kuwa wachezaji hao wawili wanapaswa kutafuta timu nyingine hivi sasa ili kuendeleza vipaji vyao.
Wanabainisha kuwa Olunga ameonyesha uwezo mkubwa sana na anaweza kucheza katika ligi kubwa yoyote duniani hivi sasa, hivyo ni wakati wa yeye kuondoka Japan na kutafuta timu katika ligi za Ulaya ambazo zina ushindani ambao anapaswa kuupitia hivi sasa.
Wachambuzi wanasema ili kuonyesha na kukuza uwezo wake, Olunga anapaswa kuipa kisogo Kashiwa aliyojiunga nayo mwaka 2018 na kutafuta timu nyingine barani Ulaya ambako kuna ushindani mkubwa.
Wachambuzi hao pia wanakubaliana na uamuzi wa Wanyama kutafuta timu nyingine, kwa sababu ya kukosa muda wa kucheza Tottenham, kwani hilo linaonyesha kuwa timu hiyo haina nafasi kwa ajili yake. Wanasema kuwa ili Wanyama aendelee kuwa mzuri uwanjani, anapaswa kucheza na kutopata kwake nafasi Tottenham kunaweza kuua kipaji na uwezo wake katika muda mfupi.
Wachambuzi wanataka Wanyama aondoke Tottenham wakati huu kwa sababu zipo klabu ambazo zimeonyesha kuihitaji huduma yake kama vile Celtic na timu nyingine kubwa Ulaya.