Mwanzoni mwa mwaka jana wakati Watanzania walipokuwa wakisubiri uchaguzi, baadhi ya watu walizungumzia sifa za Rais Watanzania waliokuwa wakimuhitaji.

Sifa ya kwanza iliyotajwa ni kuwa Watanzania walikuwa wanamuhitaji Rais dikteta yaani mwamrishaji. Waliotoa maoni hayo walidai kuwa nchi imefikia mahali pabaya kwa sababu Rais Jakaya Kikwete alikuwa mpole.

Uchaguzi ukaja mwezi Oktoba mwaka jana. Dk. John Magufuli akatangazwa kuwa mshindi. Mwanzoni mwa kazi yake watu wengi walivutiwa na utendaji wake na hasa utekelezaji wa kaulimbiu ya kutumbua majipu.

Hakuna waliochukia hatua ya mafisadi na wabadhirifu kutumbuliwa majipu, bila shaka ni hao walioendelea kutumbuliwa majipu na ndugu zao. Lakini Watanzania walio wengi walivutiwa na hatua hiyo iliyochukuliwa na Rais Magufuli kusafisha nchi.

Ulifika wakati ambao Katibu Mwenezi wa Chama Cha Mapinduzi, Nape Nnauye, alidai kuwa kasi ya utendaji wa Rais Magufuli  ingefutilia mbali upinzani nchini.

Lakini ukitaka kusema kweli, leo upinzani unaendelea kupata nguvu huku ukiungwa mkono na wananchi. Hali hii imejitokeza zaidi baada ya Serikali kuonekana kwamba inaingilia shughuli za Bunge na hasa kitendo cha matangazo ya Bunge kuzuiwa kuwafikia wananchi.

Kana kwamba hilo halikutosha, Kamati ya Maadili ya Bunge kuhariri hotuba ya bajeti ya Kambi Rasmi ya Upinzani kwa kuondoa maneno ambayo kwa maoni ya wajumbe wa Kamati hiyo, ilikiuka kanuni na maadili.

Hali hii inaonekana mbele ya watu wengi kwamba ni kitendo cha Serikali kupora uhuru wa Bunge. Kwa maneno mengine, inaonekana kwamba Serikali imejiweka juu ya Bunge kama ilivyokuwa wakati wa mfumo wa chama kimoja.

Wakati wa mfumo wa chama kimoja Serikali ilikuwa juu ya Bunge na juu ya Mahakama. Wakati huo Bunge na Mahakama vilihesabiwa kuwa sehemu ya Serikali.

Tuliokuwa walimu wakati wa mfumo wa chama kimoja, tulifundisha kwamba Serikali ina sehemu tatu nazo ni utendaji, utungaji sheria na utoaji haki.

Tulifundisha kuwa sehemu ya Serikali ambayo ni utendaji ni Baraza la Serikali. Sehemu ya Serikali ambayo ni ya utungaji sheria ni Bunge, na sehemu ya Serikali ambayo ni ya utoaji haki ni Mahakama. 

Kwa maana hiyo, Baraza la Mawaziri, Bunge na Mahakama vyote kwa pamoja zilikuwa idara au sehemu za Serikali. Serikali iliweza kuingilia idara zake hizo wakati wowote ule.

Mwaka 1975, Bunge la Tanzania kwa maendeleo ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) lilipitisha sheria ya chama kushika hatamu –  CCM ikawa juu ya Serikali, Bunge na Mahakama.

Kabla ya hapo, mwaka 1968 Halmashauri Kuu ya Taifa iliyokutana Tanga, ilifukuza wabunge kama tisa na kuwavua uanachama kwa kudai kwamba Bunge – chombo cha watu wote – lilikuwa juu ya chama.

Wakati huo huo, Serikali ya CCM iliendelea kukaidi uamuzi wa Mahakama kwa kuwa ilikuwa imejiweka juu ya Mahakama. Kwa mfano, ingawa Mahakama iliendelea kuamua mgombea binafsi aruhusiwe, yaliyokuwa madai ya Mchungaji Christopher Mtikila, Serikali iliendelea kukaidi amri ya Mahakama ambako kulikuwa kukiuka misingi ya utawala bora.

Kwa maelezo ya chama na Serikali yake pia, wananchi walipitisha sheria ya kuzuiwa kuhoji mahakamani matokeo ya uchaguzi wa Rais. Tume ya Uchaguzi ikawekwa juu ya Mahakama.

Hii ndiyo hali tuliyoendelea kushuhudia Tanzania hata kabla Rais Magufuli hajashika kiti cha urais. 

Huko nyuma, Katiba iliposema kwamba Bunge na Mahakama ni sehemu za Serikali ilihalalisha kwa kiasi fulani Serikali kuingilia shughuli za Bunge na Mahakama.

Lakini miaka kumi iliyopita (2005), Katiba ya Tanzania ilinyoosha mambo. Ilikuwa baada ya kuingizwa kwenye katika kipengele cha mamlaka ya nchi.

Katiba ya Tanzania inaeleza waziwazi kwamba Tanzania kuna mamlaka ya nchi. Mamlaka ya nchi ya Tanzania hujumuisha Serikali, Bunge na Mahakama. Vyombo hivi vitatu kila kimoja kinajitegemea na ni lazima viheshimiane. Serikali inawajibika kuheshimu Bunge.

Kwa kweli kitendo cha Serikali kuingilia masuala ya Bunge kimesababisha vyama vya upinzani kuonekana kwamba vinapambana na Rais Magufuli.

Hali hii inatia doa utendaji mzuri wa Rais Magufuli na hapa siyo siri wananchi wengi wapo upande wa wapinzani katika suala la kuzuiwa shughuli za Bunge kurushwa ‘live’. Wananchi wanataka kuangalia wabunge wao wanasema nini.

Lakini pia wananchi hawataki kusikia kwamba kamati fulani ya Bunge imehariri hotuba ya wapinzani, huku hotuba za mawaziri wa chama tawala zikiwa hazihaririwi na wapinzani. Hii ni kasoro.

Serikali inaweza kufanya jambo lolote lakini siyo kubana demokrasia kama ilivyokuwa wakati wa mfumo wa chama kimoja. Serikali ikibana demokrasia moja kwa moja inaonekana kuwa ni ya kidikteta. Serikali inapofanya hivyo husababisha kuchukiwa hata na wale ambao wameendelea kuiunga mkono. Serikali ijitazame upya.