Uchaguzi wabunge EALA…

Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano leo wanatarajia kuchangua wabunge tisa watakaoiwakilisha Tanzania katika Bunge la Afrika Mashariki (EALA).

Uchaguzi huu unaelezwa na wafuatiliaji wa masuala ya kisiasa kuwa ni vita kati ya rushwa na haki. Pia umetawaliwa na u-kanda. 

Kumekuwapo matukio mengi ya utoaji rushwa ya waziwazi kwa baadhi ya wagombea wenye ukwasi.

Wagombea na wapambe wao wanahaha huku na kule katika Manispaa ya Dodoma kuwashawishi wapiga kura ambao ni wabunge.

Hata hivyo, kwa upande wa CCM ambao ndiyo wanaotarajiwa kutoa wabunge wengi kulingana na uwiano wa wabunge wao bungeni, ndiko kwenye matukio mengi ya rushwa.

Wagombea wawili wanaume wamekuwa wakihaha na mikoba ya fedha. Wameonekana waziwazi wakitoa ushawishi wa fedha bila kukemewa na uongozi husika kutoka katika chama hicho.

Kumekuwapo habari kwamba baadhi ya wagombea wamekuwa wakihonga hadi Sh milioni moja kwa kila mgombea, lakini wapo pia wabunge kadhaa waliokubali kupokea hata Sh 50,000 kutoka kwa wagombea wasiokuwa na ukwasi.

Hali ni tofauti kwa vyama vingine vya siasa ambavyo wagombea wake wanaonekana kutokuwa na mafungu ya fedha ya kuwashawishi wagombea.

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimemteua Anthony Komu kuwania ubunge huo. Komu aliwashinda Godfrey Mnubi, Edgar Chibura, John  Malanilo, Patrick  Nkandi, Anna  Maghwira, Deogratias Assey, Pasquina Lucas, Deusdedit Kahangwa, na Mwantum Mgonja.

Kwa upande wa CCM, kundi la wanawake kutoka Zanzibar wanaopambana ni Septuu Nassor, Safia Ali Rijaal na Mariam Usi Yahaya.

Katika kundi la wanaume upande wa Zanzibar wanaochuana ni Dk. Said Bilal, Abdallah Ali Mwinyi, Zuber Ali Maulid, Dk. Haji Mwita Haji, Amada Khatibu na Hamis Jabir Makame.

Kwa upande wa wanawake Bara, wanaopambana ni Angela Kizigha, Janeth Mmari, Janet Mbene, Fancy Nkuhi, Shy-Rose Bhanji na Godberha Kinyondo.
Wanaume Bara ni Adam Kimbisa, Dk. Edmund Mndolwa, Siraju Kaboyonga, Bernard Mulunya, William Malecela, Elibariki Kingu, Dk. Evance Rweikiza, Mrisho Gambo na Charles Makongoro Nyerere.

Mgombea kupitia TLP ni Michael Mrindoko. Uchaguzi wa mwisho ulifanyika mwaka 2006. Uhai wa Bunge la sasa la EALA unamalizika Juni 4, mwaka huu.