Fikiria maisha ya mijini, vyumba vya kupanga utaishia kulaza watoto wanne katika chumba kimoja, katika kitanda kimoja na ndani ya chandarua kimoja. Lakini pia katika maisha ya vijijini gharama zimepanda hata kama unaishi kwenye nyumba yako.
Wakati huo huo, kwa upande wa Taifa, kama wananchi wake wanazaliana kwa kasi ya kutisha litashindwa kujenga shule, zahanati, hospitali za kutosha na kadhalika. Kwa hivyo, mawazo ya Chadema kwamba itatumia idadi ya kubwa ya wingi wa watu kiuchumi, ni mawazo potofu na ya kijinga.
Tutakuwa na Taifa la watu wengi mno lakini wasio na afya na wanaoandamwa na maradhi. Vile vile tutakuwa na Taifa litakalotawaliwa na vurugu, pale kina baba watakaposhindana kupata nyumba ndogo baada ya kuwachakaza wake zao kwa kuwazalisha kila mwaka.
Mwanzo, hata tukizaa mabilioni ya watoto hatutaweza kuijaza Tanzania pia ni mwanzo potofu na wa kijinga.
Tazama, hivi sasa tuna ardhi kubwa lakini tayari kuna migogoro ya ardhi. Tuzingatie kuwa Tanzania ni nchi yenye miamba ya kale. Kwa hiyo ina utajiri mkubwa wa madini lakini ni sehemu chache zenye ardhi yenye rutuba. Kama ardhi yetu yote ingekuwa na rutuba tusingekuwa tunagombea ardhi.
Katika mazingira haya yote, hakuna msomi wa kweli anayeweza kuunga mkono sera ya Chadema ya kupuuza uzazi wa mpango. Hizo ni propaganda za kijinga kwamba Chadema inaungwa mkono na wasomi kupinga uzazi wa mpango.
Ni vyema vyama vya upinzani kama Chadema vikatambua kuwa hata kama haviongozi Serikali, vina jukumu kubwa la kuona kwamba haviongozi wananchi kwenye mambo yanayoweza kuhatarisha afya zao na usalama wao.
Kwa hiyo basi, Chadema isipinge mambo muhimu kwa Taifa kwa sababu tu ya kujitafutia umaarufu kwa wananchi, eti inapinga chama tawala na Serikali yake katika kila kitu.
Chama cha upinzani ni chama kinachopinga mambo yote yasiyo na maslahi kwa wananchi na Taifa kwa ujumla, yanayotendwa na chama tawala na Serikali yake.
Uzazi wa mpango una maslahi kwa wananchi na kwa Taifa kwa ujumla. Kwa hivyo, ni ujinga na ni upuuzi Chadema kupinga uzazi wa mpango.