Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dodoma
Katika dunia inayoendelea kwa kasi kwa kila nyanja, kuna kila sababu kwa Tanzania kuwa na chombo madhubuti cha kusimamia mazingira.
Ni jambo lisilokuwa na ubishi kuwa kwa hali ya sasa na hata hapo baadae, Baraza la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira haliwezi tena kuhimili changamoto za uhifadhi wa mazingira na kukabiliana na wanaoharibu mazingira kwa upande mwengine.
Kila mmoja ni shuhuda wa namna hali yetu ya uchafuzi wa mazingira ilivyo, kuanzia ukataji miti ovyo, utupaji taka taka ovyo, utiririshaji maji yasiyofaa hasa mitaro inayoelekezwa katika fukwe za bahari, Mito, Maziwa limekuwa tatizo sugu.
Wananchi nao wamekuwa wakilalamikia makelele katika mitaa yanayosababishwa na watu huku kukikosekana chombo madhubuti cha kudhibiti hali hiyo.
Tumeshuhudia kuongezeka kwa magugu maji katika Ziwa Victoria kiasi cha kutishia vyombo vya usafiri katika Ziwa pamoja na uhai wa viumbe wanaoishi katika Ziwa hilo.
Hali ya Fukwe zetu sio ya kuridhisha hasa katika fukwe za Mkoa wa Dar es Salaam.
Kila mmoja ni shuhuda wa hili, maeneo yanayoanzia ukingo wa bahari karibu na Hospitali ya Ocean Road, Agha Khan maji machafu yanayotoka katika ya Mitaa ya Jiji yanachafua madhari nzuri ya fukwe katika maeneo hayo,hali ambayo inawakirihisha wapita njia hasa wanaotumia fukwe kwa shughuli mbalimbali kama vile mazoezi, kupumzika au kuogelea.
![](https://www.jamhurimedia.co.tz/wp-content/uploads/2025/02/1002475703.webp)
Kimsingi, majukumu ya NEMC kama Baraza la Ushauri, hayawezi kutufikisha katika malengo ya utunzaji, uhifadhi na udhibiti wa wanaoharibu mazingira.
Karibu Mataifa mengi yamekuwa na chombo cha kudhibiti mazingira vikipewa nguvu na uwezo kisheria katika kuhakikisha nchi zao zinatunza mazingira,lakini pia kuwadhibiti wale wote wanaoharibu kwa namna moja au nyengine.
Ni wakati muafaka sasa kwa nchi yetu kuanzisha Mamlaka ya Taifa ya Kudhibiti na Kusimamia Mazingira( National Environmental Management Authority – NEMA).
Chini ya NEMA kama Taasisi madhubiti, itaweza kukabiliana na changamoto mbalimbali ambazo hivi sasa NEMC imeshindwa kuzitatua kwa sababu za muundo na majukumu yake kujiegemeza zaidi kama chombo cha ushauri na sio Mamlaka Kiutendaji.
Mwanga wa matumaini umeanza kuchomoza, Wabunge kupitia Kamati ya Maji na Mazingira nao wameanza kupaza sauti juu ya ulazima wa Serikali kuanzisha NEMA kama Chombo cha Mamlaka.
Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mbunge wa Jimbo la Kalenga, Jackson Kiswaga akiwasilisha taarifa ya Kamati yake mbele ya Bunge hivi karibuni, amesema ni muhimu kwa Serikali kulibadilisha Baraza la Taifa ls Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira( NEMC) kuwa Mamlaka.
Mtazamo wa Wabunge ni kuwa iwapo NEMC itabadilishwa na kuanzishwa NEMA, itakuwa ni chombo chenye nguvu na madaraka kiutendaji na hivyo kuweza kuleta ufanisi katika suala zima la menejimenti ya mazingira hasa suala zima la udhibiti na uhifadhi.
Mtazamo huo wa Wabunge wetu, unaongwa mkono na wakereketwa wa mazingira ambao kwa nyakati tofauti wanaona Tanzania imechelewa kuwa na chombo kama hicho cha Mamlaka.
” Tumechelewa sana kuwa na chombo madhubuti cha mazingira, nadhani wakati umefika sasa Serikali kusikiliza kilio cha wana-mazingira kwa kuanzisha Mamlaka ya Usimamizi wa Mazingira nchini”aAlishauri Johson Methew, Mdau wa Mazingira.
![](https://www.jamhurimedia.co.tz/wp-content/uploads/2025/02/1002475649-1.jpg)
Mdau mwengine wa Mazingira Ali Makame Issa anaunga mkono wazo la Wabunge la kuitaka Serikali kuipandisha hadhi NEMC kuwa NEMA hatua ambayo itasaidia kukabili manejimenti ya mazingira hapa nchini.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais( Muungano na Mazingira) Mhandisi Hamad Yussuf Masauni amesema Serikali imepokea maagizo ya Wabunge na kuahidi kuyafanyia kazi.
Waziri Masauni amesema Serikali inafanyia kazi mapendekezo matatu ya marekebisho ya Sheria ya Mazingira, Sura ya 191, ikiwa ni pamoja na kulifanya Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kuwa mamlaka kamili.
Msimamo wa Serikali umekuja baada ya taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira kwa mwaka 2024, iliyowasilishwa na Mwenyekiti wa kamati hiyo, Jackson Kiswaga, bungeni, ambapo Waziri Masauni amesema serikali imepokea na inaendelea kufanyia kazi mapendekezo hayo.
“Kama tulivyoahidi kwenye kamati, Mheshimiwa Spika, naomba kuthibitisha mbele yako kuwa tutayafanyia kazi mapendekezo yote yaliyotolewa na wabunge na kamati… Tayari tumeandaa mpango kazi kabambe, na hadi sasa hakuna hata kipengele kimoja ambacho hatujatekeleza. Tunaendelea vizuri,” alisema Waziri Masauni.
Waziri Masauni alisema kuwa matarajio ya serikali kuona mapendekezo hayo yanajadiliwa na kupitishwa katika kikao kijacho cha Bunge kwa ushirikiano mkubwa.