Na Deodatus Balile, JamhuriMedia, Bunda

Naandika makala hii nikiwa safarini wilayani Bunda. Nimekuja Bunda si matembezini, bali kumzika mwanaparokia mwenzetu, ambaye alikuwa Mweka Hazina wa Parokia yetu ya Roho Mtakatifu Kitunda, ambako mimi ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Walei.

Ndugu yetu Joseph Mabusi ametutoka. Tulivyo sisi ndivyo alivyokuwa yeye, alivyo yeye ndivyo tutakavyokuwa sisi. Tumwombee. Raha ya Milele umpe Ee Bwana… na Mwanga wa Milele umwangazie, marehemu Mabusi apumzike kwa amani. Amina.

Leo ni Jumanne ya kwanza ya Mwaka 2025. Kwa mantiki hiyo ni makala ya kwanza ya Sitanii kwa mwaka 2025. Gazeti la JAMHURI tumeingia mwaka wa 14 tangu gazeti hili la uchunguzi tulianzishe. Mwaka huu tunafanya uchaguzi wa saba wa mfumo wa vyama vingi tangu uliporejeshwa. Mfumo wa vyama vingi umerejeshwa mwaka 1992. Uchaguzi wa kwanza wa vyama vingine ulifanyika mwaka 1995.

Sitanii, kabla ya hapo Tanzania ilikuwa na mfumo wa vyama vingi, ambao ulifutwa mwaka 1965, tukabaki na mfumo wa chama kimoja wa aina yake. Nasema wa aina yake, kwa maana pamoja na Zanzibar kuungana na Tanganyika mwaka 1964, mfumo wa vyama vingi ulipopigwa marufuku upande wa Tanganyika, uliendelea kuongozwa na Chama cha Tanganyika African National Union (TANU) na Zanzibar iliendelea kuongozwa na Afro-Shiraz Party (ASP).

Vyama hivi viwili viliendelea kufanya siasa Tanzania kwa maana ya upande wa Tanganyika na Zanzibar, hadi Februari 5, 1977 pale TANU na ASP zilipoungana na kuzaa Chama Cha Mapinduzi (CCM). Kwa mantiki hiyo, CCM sasa ina umri wa miaka 48 tangu imezaliwa. Mwaka 2027 itafikisha miaka 50. Ni vyama vichache mno katika Bara la Afrika vilivyofanikiwa kuwa na umri mkubwa kiasi hiki na vikabaki imara.

Mfumo wa chama kimoja ulioanza mwaka 1965, ulidumu kwa miaka 27, ukabadilishwa mwaka 1992 pale upepo wa mageuzi duniani ulipokuwa unavuma kama kisulisuli. Huu ulikuwa mwendelezo baada ya nchi nyingi duniani kubainika kuwa zilikuwa zinaelekea kufilisika mwaka 1978 (ikiwamo Tanzania), ndipo Benki ya Dunia ikaanzisha mazungumzo kuziokoa nchi 26 zilizokuwa katika hatari ya kufilisika.

Sitanii, hatari hii ilitokana na mfumo wa uchumi hodhi. Kwamba serikali za nchi hizi na nyingine duniani zilikumbatia mfumo wa serikali kuwa ndiyo kila kitu. Kwa wenye umri wa kwangu na zaidi mtakumbuka miaka ya 1970 mwishoni na 1980 mwanzoni, hasa baada ya vita ya Kagera, mwaka 1982 tuliambiwa tufunge mikanda kwa miezi 18, ambapo halijawahi kutolewa tangazo la kuifungua mikanda hiyo hadi leo.

Serikali ilimiliki maduka kupitia maduka ya vijiji, ilikuwa na Shirika la Taifa la Usagishaji, hakuna mtu binafsi aliyeruhusiwa kuwa na mashine ya kusaga unga, ungekutwa nayo, ungefunguliwa kosa la uhujumu uchumi. Maduka hayo kuna nyakati kwa mfano kwetu Kijiji cha Nyanga, Wilaya ya Bukoba (M), ilikuwa kila kaya inalazimika kwenda kupalilia shamba la chai la kijiji ndipo uweze kuuziwa sukari, chumvi, viberiti na bidhaa nyingine. Kama haumo kwenye orodha ya waliopalilia shamba la kijiji, usingeuziwa bidhaa.

Sitanii, serikali ndiye alikuwa mwajiri pekee rasmi. Serikali ilimiliki mashirika ya umma zaidi ya 500, ambayo yaliajiri kila aliyehitimu kuanzia elimu ya msingi hadi chuo kikuu, bila kujali kama linapata faida au la. Ilipofika mwaka 1987, Benki ya Dunia ikaleta mabadiliko ya lazima, ikiwamo kupuguza wafanyakazi na kuruhusu sekta binafsi kuanzisha biashara, yakifahamika kama Structural Adjustment Program (SAPS).

Sitanii, mpango huu ulisaidia kuipunguzia serikali mzigo wa kulipa mishahara na uendeshaji wa mashirika yasiyozalisha, lakini pia ukawapunguzia wananchi mzigo wa kulipa kodi nyingi, ikiwamo kodi ya kichwa kwa ajili ya kupata fedha za kulipa wafanyakazi walioajiriwa kila mwaka hata kama hawakuzalisha kitu kwa ajili ya taifa. Hali ya uchumi ilikuwa mbaya kweli kweli. Maduka hayakuwa na sabuni, tulikuwa funafulia sabuni za magwanji na kalyang’ombe.

Dawa ya mswaki/meno ilikuwa starehe. Sabuni ya Ilula, ukipata mche ndiyo ya kuogea kwa starehe. Tulifulia majani ya matembere na viazi, mapapai na mmea fulani Bukoba tunauita “oluzinga”. Nakiri sikupata kuvaa viatu shuleni kati ya darasa la kwanza hadi la saba. Na si mimi tu, ni kila mtoto. Ukumbuke baba yangu alikuwa Afisa Elimu Mkoa, lakini hakuweza kutununulia viatu, maana nchi nzima tulikuwa tunasoma peku. Leo kuna mtoto anakwenda shule peku?

Miaka michache baadaye, Hayati (Rais) Benjamin Mkapa, aliongoza mkakati wa kudai nchi maskini zipunguziwa madeni uliofahamika kama Highly Indebted Poor Countries (HPIC), mpango ambao ulisaidia kuzifutia madeni nchi maskini, yaliyokuwa yanazielekeza katika kufilisika. Tanzania ni moja ya nchi zilizonufaika na mpango wa HIPC.

Sitanii, barabara za lami ulikuwa msamiati. Nakumbuka mwaka 1978, baba alikuwa Afisa Elimu Biharamulo, mkoani Kagera. Ilikuwa tunakwenda Rwamishenye (Amjuju) tunapanda mabasi ya Kamata au Remtula, muda wa saa 9 alfajiri, kisha tunafika Biharamulo saa 7 usiku. Saa 22 barabarani kwa umbali wa kilomita 1,972. Eneo la Kasindaga basi lilikuwa linakwama wazazi wetu wanashuka na kusukuma. Halikuwapo suala la nimelipa nauli konda na dereva ndio walikwamue. Lilikuwa basi “letu” sote.

Leo kuna lami, mpwa wangu Grayson anatoka Biharamulo hadi Bukoba kwa saa 2 tu. Tena zipo nyakati anatoka Biharamulo anakwenda Bukoba, anafanya kazi na saa 12 jioni anatoka Bukoba anarejea Biharamulo, saa 2 usiku anakupigia kuwa amefika. Hapo sijazungumzia safari ya Bukoba – Dar es Salaam tulizokuwa tunapita Uganda na Kenya au Dar es Salaam – Kigoma au Dar es Salaam – Mtwara.

Sitanii, nimeyasema haya nikiamini ni hadithi inayofanana mkoa kwa mkoa. Ni hadithi inayoweza kutufikirisha. Ni hadithi inayolenga kunisaidia kufafanua hiki ninacholenga kukisema. Kwamba mwaka 2025 ni mwaka wa uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani. Huu ni mwaka wa kuamua hatima yetu katika nyanja mbalimbali.

Nasema nyanja mbalimbali kwa maana ya maendeleo ya sekta binafsi, elimu, ajira, miundombinu kama barabara za lami, reli ya mwendokasi, ndege, mabomba ya mafuta, mabomba ya gesi, huduma za afya za kiwango cha juu, utekelezaji wa sera ya viwanda kwa maana ya kuongeza thamani mazao yetu, lakini pia tukazalisha bidhaa na huduma.

Katika uchaguzi huu, natamani sana kusikia viongozi wakinadi sera zifuatazo. Kwamba chama fulani kikichaguliwa kitapuguza utitiri wa kodi. Kitaupunguza kwa kuanzisha viwanda vingi, hivyo kutanua wigo wa kodi, kikafungua masoko ndani na nje ya nchi, kitajenga mabomba ya gesi na mafuta mengi, tupate nishati ya bei rahisi kuendesha viwanda vyetu na tupate nishati safi ya kupikia.

Kwamba mabomba ya gesi yatapelekwa katika nchi zinazotuzunguka, tuuze gesi ya hadi dola bilioni 15 na zaidi kwa mwaka, hivyo chanzo kimoja pekee cha gesi kilete mapato ya kutosheleza bajeti ya taifa na ziada, hivyo kuiondolea nchi shinikizo la kukamata “wamachinga” walipe kodi. Kwamba chama kikishinda kitawapanga “wamachinga” kwa kuwajengea majengo ya kisasa kama walivyofanya Wamisri, na wote wauzie katika majengo maalumu nchi nzima.

Kwamba chama kitakachoshinda, kitawapanga waendesha bodaboda wawe na chama imara, waendeshe pikipiki kwa mujibu wa sheria bila kupita kushoto, taa nyekundu na kusababisha ajali. Na kwamba spea za pikipiki zote nchini zitatengenezwa hapa nchini, ikiwa ni hatua ya awali ya ujenzi wa viwanda vya pikipiki nchini.

Kwamba chama kitakachoshinda kitaanzisha viwanda mama angalau vitatu, vitakavyotumika kuzalisha mashine na mitambo midogo midogo hadi ya kati inayotumika kurahisisha kazi, kwa mfano kuzalisha misumari ya kuezeka yenye njoro zinazofungwa kwa mashine. Si hiyo tu, viwanda vizalishe vimashine vidogo vidogo vya rangi, kupalilia, bulb, switch socket, nyaya za umeme, nondo, chuma, vigae na vingine vya aina hiyo. Chama cha siasa kitangaze sera ya kuwezesha Watanzania kumiliki viwanda, hivyo fedha zisiende nje zibaki ndani.

Sitanii, nimetumia mfano wa sekta ya ujenzi, lakini hapa nalenga kusema zinatumika fedha nyingi kuagiza vifaa na huduma ambazo tungeweza kuzizalisha hapa nyumbani. Ni matarajio yangu kwamba chama cha siasa kinachopambana kushinda uchaguzi wa mwaka huu, kitatueleza kama ahadi yao kwetu kupitia ilani zao cha uchaguzi kwamba wakishinda watatutafanyia nini?

Hizi ahadi, zianzie katika ngazi ya kata. Kwamba mtu akichaguliwa kuwa diwani aeleze kwenye kata yake atapambanaje kuongeza ajira, badala ya vijiji vingi hapa nchini watu wake kugeuka ombaomba. Akija mgeni wanawaza kumwomba badala ya kumkirimu. Wanaomba si kwa kupenda, bali kutokana na umaskini. Kwa mfano kijiji kingekuwa na kiwanda cha kutengeneza hata pikipiki tu, kila kijiji kikawa na uwezo wa kuingiza Sh milioni 10 tu, kupitia mishahara ya waajiriwa wa viwanda hivyo, hali ya uchumi na mzunguko wa fedha katika vijiji vyetu utakua.

Tusiendelee na moyo wa kuwaza kuwa tunaomba Mhe. Rais atusaidie, bali vyama viandae sera za kuwezesha wananchi kiuchumi, kiafya na kielimu kuanzia ngazi ya kijiji, kubwa likiwa ni vyanzo vya mapato. Viwanda vidogo vidogo vya kimkakati na masoko ya bidhaa zitakazozalishwa, iwe sera ya msingi kwa vyama vyote vitakvyoshiriki uchaguzi ili kuwaondolea wananchi umaskini.

Sitanii, mwisho, nchi yetu inaandaa Dira ya Taifa ya Mwaka 2050. Ni matarajio yangu kuwa kila chama kitaandaa Ilani yake ya Uchaguzi iendane na Dira ya Taifa 2050. Vipaumbele vya taifa letu vimeainishwa kwenye Dira ya Taifa ya 2050 itakayokamilika mwaka huu. Hivyo, sitarajii vyama vya siasa kutushibisha matusi na ahadi hewe kwenye mikutano ya hadhara ambao ni ulaghai.

Kwamba kama vyama havitanadi sera katika mikutano ya hadhara, baada ya uchaguzi hatutakuwa na cha kuwadai. Tunasubiri sera, si maneno matupu. Mungu ibariki Tanzania.

0784 404827