πŸ“Œ Asema wakati Serikali ya Awamu ya Sita inaingia madarakani Vijiji 4000 havikuwa na umeme

πŸ“Œ Aitaka TANESCO na REA kuendelea kutoa elimu ya kuunganisha umeme

πŸ“Œ Nishati ya umeme yauongezea ufanisi Zahanati ya Mang’oto

Naibu Waziri Nishati, Mhe. Judith Kapinga amesema ni maono ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kuona wananchi wote wanapata huduma ya umeme.

Mhe. Kapinga ameyasema hayo leo Machi 17, 2025 katika Kijiji cha Mang’oto Wilaya ya Makete mkoani Njombe wakati wa ziara ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kukagua miradi ya umeme vijijini inayotekelezwa na Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA).

“Mheshimiwa Rais legacy yake na maono yake ni Tanzania nzima mijini, vijijini na vitongojini kupata umeme, ndio maana mnamuona anahangaika kutafuta fedha kwa ajili ya miradi ya umeme kwenye Vitongoji”. Amesema Mhe. Kapinga

Ameongeza kuwa mwaka 2020 Serikali iliahidi kuvifikishia umeme vijiji vyote 12,318 ifikapo Desemba 2025 na wakati Serikali ya Awamu ya Sita ilipoingia madarakani takribani Vijiji 4000 havikuwa vimefikiwa na huduma ya umeme.

Katika hatua nyingine Mhe. Kapinga amelitaka Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kuendelea kutoa ushirikiano kwa wananchi pamoja na utoaji wa elimu wa jinsi ya kufanya maombi ya kuunganisha umeme.

Ametoa rai kwa wananchi kuendelea kutoa taarifa kwa kutumia namba 180 ambayo haina malipo kwa mteja

Mhe. Kapinga amesisitiza kuwa azma ya Serikali ni kuhakikisha umeme wa uhakika na unaotabirika unawafikia wananchi wote ili waweze kunufaika kwa shughuli za kiuchumi.

Kufika kwa umeme katika Kijiji cha Mang’oto kumewanufaisha wananchi ambapo wamefungua shughuli za kiuchumi ikiwemo mashine za kusaga nafaka lakini pia kuweza kurahisisha huduma katika Zahanati ya Mang’oto ambayo hapo awali ilikuwa ikitumia umeme wa jua.

Kutokana na hilo wananchi wameipongeza Serikali kwa utekelezaji wa miradi ya umeme Vijijini kwani wameweza kuinua vipato vyao ikiwemo kufungua biashara kama za kuchomelea na kuboresha huduma za afya.