Nimeulizwa na watu wengi ikiwa agizo la Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe, kuhusu kumtia mbaroni mara moja Dudubaya kwa maneno yake dhidi ya marehemu Ruge Mutahaba ikiwa ni sawa kisheria au si sawa. Ninaweka majibu wazi hapa ili hatimaye tufaidike wote, ambao waliuliza, kadhalika ambao hawakuuliza.

Swali la msingi lilikuwa ni je, kuna kosa la kutukana, kukashifu au kudhalilisha maiti hapa kwetu mpaka Dudubaya akamatwe? Hili ndilo swali la msingi nililoulizwa na wengi.

Jibu langu kwao lilikuwa ni ndiyo, kosa hilo lipo. Kifungu cha 127 cha Sheria ya Kanuni za Adhabu, Sura ya 16 kimeeleza jambo hili. Kifungu kinasema kuwa: “Mtu ambaye kwa makusudi atakuwa na nia ya kuumiza hisia za mtu mwingine yeyote, au kutukana dini ya mtu mwingine yeyote, akaivunjia heshima maiti ya binadamu (offers any indignity to human corpse) atakuwa ametenda kosa.”

Swali ambalo siwezi kujibu ni ikiwa maneno ya Dudubaya ni ya aibu au yameivunjia heshima maiti/mwili wa Ruge. Hilo ni suala la mahakama kupima uzito wa maneno yenyewe, kadhalika kuyatafsiri kwa tafsiri ya kawaida ya matumizi yake na kuona ikiwa yanajitosheleza kuitwa yenye kuvunja heshima ya maiti au hapana.

Hayo ni masuala ya mahakama, mimi kwangu ninaishia katika kusema kuwa kutamka maneno ya aibu, yenye kuvunja heshima dhidi ya maiti ya binadamu ni kosa hapa Tanzania.

Baada ya kuona uwepo wa kosa hilo, swali jingine ni je, kosa hilo lina adhabu? Jibu ni ndiyo, kosa hilo lina adhabu. Kifungu kinachoanzisha kosa hilo hakikutaja moja kwa moja adhabu ya kosa hilo. Isipokuwa sheria nyingine, Sheria ya Mwenendo wa Kesi za Jinai Sura ya 20, imetaja adhabu ya kosa hilo.

Jedwali la Kwanza, Sehemu ya 14 ya sheria hiyo inasema kuwa adhabu ya kosa hilo ni kifungo cha miaka 2 jela. Na inasema kuwa inaruhusiwa kumkamata mtu aliyetenda kosa hilo bila kuwa na hati ya kukamata (arrest warrant).

Na zaidi, sehemu hiyo inasema kuwa kosa hilo linapaswa kusikilizwa na mahakama za chini (subordinate courts), kwa maana ya mahakama ya hakimu mkazi, mahakama ya wilaya au ya mwanzo.

Hatujui mambo mengi ndiyo maana watu wameshangaa kuwa inakuwaje kuchoma moto tu unakwenda jela maisha. Yafaa sasa tulielewe hili ili watu wenye tabia za aina hii waelewe wanaweza kuchukuliwa hatua za kisheria na pengine kwenda jela kabisa.