Nilipozuru Cuba, nilistaajabu kukutana na mambo ambayo sikuyafikiria kabla. Niliposoma habari za Fidel Castro kwenye vyombo vya Magharibi, niliijiwa na picha ya mtu katili, muuaji, mpenda kusifiwa na mjivuni.

Nilipofika Havana, nilistaajabu kutoyaona hayo mambo. Sikuona utitiri wa picha za Castro mitaani. Mabango, baadhi ya mavazi, samani na vitu vingine vingi vilipambwa kwa picha za Che Guevara na Jose Marti. Huyu Marti ni mwanamapinduzi, mwanasiasa, mwanafalsafa, mtunzi wa vitabu, mwandishi wa habari na baba wa mapinduzi ya Cuba. Kwa Cuba, huyu ndiye Baba wa Taifa.

Fidel Castro, ambaye wengi wetu tunampa sifa za kuwa ‘Baba wa Taifa’ wa Cuba, hakuthubutu kwa namna yoyote ‘kuivuruga’ historia ya kweli ya nchi hiyo inayotambua na kuenzi nafasi ya Marti.

Castro na Mwalimu Nyerere wanafanana kwa mengi. Miongoni mwayo ni ile tabia yao ya kutotaka ‘kuabudiwa’. Barabara ya Pugu ilipobadilishwa jina na kupewa jina lake, alisema: “Si msubiri kwanza tufe?”

Baada ya Mwalimu kufariki dunia tumeshuhudia vitu vingi vikipewa jina lake. Tumeona majengo, madaraja, shule, kumbi, viwanja na hata vivuko. Hii inathibitisha mapenzi ya Watanzania kwa Mwalimu. Pamoja na nia njema, nimeonelea nitoe ushauri mdogo.

 

Mosi, jina la Mwalimu litumike kwenye mambo au vitu vinavyoshabihiana kwa sifa na heshima ya Mwalimu. Kwa mfano, ni jambo la fedheha kuona shule yenye jina la ‘Nyerere’ au ‘Kambarage’ ikiwa ndiyo inayoshika mkia au ikiongoza kwa watoto wa kike kutiwa mimba.

Inasikitisha, na kwa kweli inaleta sintofahamu kuona usafiri wenye jina la ‘Nyerere’ unashika nafasi ya pili kwenye rekodi ya vyombo vya majini vilivyoua Watanzania wengi.

Ni matumizi mabaya ya jina la ‘Nyerere’ kuona, kwa mfano, ukumbi uliopewa jina lake ukiwa hauna hata huduma za vyoo!

Inaudhi kuona au kusikia barabara yenye jina la ‘Nyerere’ ikiongoza kwenye ajali, au uwanja wa ndege uliopewa jina lake ukisifika kwa kuwa mapito ya mihadarati.

Kwa maneno mengine, nashauri jina la Mwalimu litumike tu kwenye vitu vinavyolingana kwa hadhi na yeye mwenyewe.

 

Pili, nadhani ni nchi chache mno, ikiwamo Tanzania ambako miji mashuhuri kama Dar es Salaam, Arusha, Mwanza au Morogoro ikiwa haina japo sanamu rasmi ya mkombozi wa taifa. Kwenye mataifa yanayothamini historia zao, kuna vielelezo vinavyowatambulisha watu muhimu au mashuhuri au wale waliotoa mchango katika ujenzi wa taifa husika. Mfano wa hili ni Afrika Kusini, ambako unapofika nchini humo huhitaji kuelezwa Mandela ni nani. Kila mahali Mandela yupo.

Kuwa na sanamu ya Mwalimu Nyerere hakumaanishi kuwa Watanzania wanaabudu sanamu, bali ni picha tu ya kutukumbusha Watanzania kuwa Mwalimu ni nani kwa Tanzania na walimwengu! Kwa sababu hiyo, napendekeza pale Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam kujengwe sanamu kubwa, ndefu na ya kipekee ya Mwalimu, pia sanamu za waasisi wengine wa taifa letu. Uwanja wa Mnazi Mmoja haupo kwa ajili ya makazi ya ombaomba.

Sanamu kama ile ya Dodoma hailingani na hadhi ya Mwalimu. Jiji la Dodoma liangalie namna ya kuwa na sanamu kubwa, nzuri kwenye uwanja mpana unaolingana na heshima ya Mwalimu. Sanamu ya Dodoma ni kama ya mtu fulani bustanini kwake. Hailingani na ukubwa na umaarufu wa Mwalimu.

 

Kijijini Butiama, kwa mgeni yeyote anayefika pale hakuna kiashirio kwamba yupo mahali alipozaliwa na kuzikwa mkombozi wa taifa hili. Makumbusho iliyoko si makumbusho, ni chumba tu ambacho mtu yeyote anaweza kuwa nacho na akakiita makumbusho. Hivi ni kweli makumbusho ile ina uwezo wa kuhimili kuhifadhi historia ya Mwalimu? Ule ni utani.

Wachina walifika pale. Wakalinganisha na makumbusho ya Mwenyekiti Mao, wakashika vichwa. Nadhani Profesa Muhongo bado anapambana kuhakikisha ahadi ya Balozi wa China kuhusu makumbusho hiyo inatekelezwa. Lakini kweli hata makumbusho ya muasisi wetu lazima tujengewe na Wachina? Sisi tunaweza nini?

Tatu, nashauri Siku ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere ibadilishwe. Nimejitahidi kuona kwa mataifa mengine yanavyowakumbuka mashujaa wao. Nimeona huwakumbuka siku walizozaliwa. Unapomkumbuka mtu siku aliyozaliwa, unashiriki tukio la furaha. Unamshukuru Mungu kwa kukupatia tuzo ya kuwa na mtu makini na wa aina ya pekee. Ni siku ya furaha, ni siku ya kucheza. Ni kama siku aliyozaliwa mtoto.

Kumbukizi kwa aliyefariki dunia ni siku ya maombolezo. Ni siku ya huzuni. Ni siku ambayo watu hujikunyata na kujuta kuondokewa na mpendwa wao.

 

Siku ya Mwalimu Nyerere, napendekeza iwe siku aliyozaliwa, ambayo ni Aprili 13. Siku hiyo iwe ya kutafakari, kuimba, kucheza na kuburudika tukikumbuka mazuri yake na kumshukuru Mungu kwa zawadi ya kutupatia huyu binadamu. Iwe siku ya kufanya tafakuri ya yale aliyotuasa. Oktoba 14 ni siku ya vilio. Ni siku ya nyimbo za maombolezo.

Kwa wenzetu kumbukizi nzuri wanazifanya siku aliyozaliwa mtu, siyo aliyofariki dunia. Nawashauri watunga sheria walitazame hili – Nyerere Day iwe Aprili 13.

Mwalimu Nyerere ndiye aliyeasisi mbio za Mwenge wa Uhuru. Mwenge ni matokeo ya mawazo yake mazuri. Siku ya kuzima Mwenge wa Uhuru isiwe Oktoba 14, maana tukio hilo linapokwenda pamoja na kumbukizi ya kifo cha Mwalimu ni kama vile Watanzania tunasema “Nyerere kafe na Mwenge wako.”

Hatujachelewa, bado tunaweza kurekebisha baadhi ya mambo yanayoleta ukakasi katika kuuenzi mwamba huu wa siasa duniani.