“Demokrasia si sawa na chupa ya soda aina ya Coca- Cola ambayo unaweza kuagiza kutoka nchi za ng’ambo. Demokrasia inapaswa kujiongoza na kujiendesha kwa mujibu wa mazingira ya nchi husika.”  Maneno haya yalizungumzwa na Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, mwezi Juni, 1991 jijini Rio De Janeiro, nchini. Brazil.

Nimenukuu maneno ya Mwalimu Nyerere kwa sababu bado naamini Watanzania wanamuenzi na kumkubali katika falsafa zake. Pili, najaribu kuangalia Demokrasia katika dhana mbili. Mosi, Demokrasia si sawa na chupa ya soda (Coca- Cola). Bidhaaa na burudiko la roho au moyo. Pili, Demokrasia ni dhana na nyenzo ya kisiasa kwa mujibu wa mazingira ya nchi husika.

Soda (Coca -Cola )  ni kinywaji kisicholewesha na kinapendwa na watu wa rika na hadhi mbalimbali duniani kote. Mtu ye yote anaweza kuagiza, kununua na kunywa au asifanye hivyo vyote na bado ikawa si dhima wala lawama kwake.

Radha ya soda hiyo haibadiliki kufuatana na mtu anayekunywa. Awe mwafrika,  mwarabu, mzungu au mwasia. Sababu kuu ni kwamba inatengenezwa kwa kutumia fomula moja tu. Hata kama itatengenezwa Marekani, Ulaya, Asia au Afrika na kusafirishwa hadi nchi fulani  bado ni soda aina ya Coca- Cola.

Kwa hiyo makundi ya watu; wanasiasa, wataalamu, wanaharakati  wanafunzi na makundi ya jumuiya nyingine hawalazimishwi kuagiza wala kutumia soda hiyo kwa sababu  eti imetengenezwa Mexico, Italy au China. Haina masharti au deni  kwa sababu  ni burudani ya hiyari ya mtu.

Demokrasia ni dhana yenye maana pana sana katika kuielewa na kuitekeleza na si sawa na chupa ya soda. Neno lenyewe asili yake ni huko Ugiriki. Leo lina miaka kadhaa tangu lianzishwe na Wagiriki mnamo karne ya tano ndani ya mji Polis  kitongoji cha Athens ( Athen Democracy)

Kuanzia wakati huo hadi karne hii ya 21 demokrasia imekua katika nyakati tofauti tofauti kuanzia demokrasia ya moja kwa moja (direct democracy) ambapo watu wote walikuwa na haki ya kushiriki katika kufanya maamuzi, isipokuwa Wanawake, Wafungwa( Watumwa) na watu wote waliokuwa chini ya umri wa miaka 18.

Na demokrasia ya uwakilishi ambayo watu wachache waliopewa ridhaa na watu wengi kushiriki katika vyombo vya maamuzi iwe katika Mahakama, Bunge na Serikali. Kwa misingi hiyo demokrasia imetofautiana kati ya tamaduni hadi tamaduni nyingine katika nchi (State) husika kwa maana ya mila, desturi, maadili na mienendo ya jamii.

Hata hivyo, wapo baadhi ya watu wanaamini kutokana na demokradia kumuhusu mtu, basi ni sawa kwa kila mtu hususani katika masuala ya haki za binadamu. Hapo ndipo penye matatizo ya uwelewa na umakini ndani ya jamii.

Ule mlango wa kujiongoza na kujiendesha kwa mujibu wa mazingira ya Nchi (state) husika hauna budi kufuatwa na kuzingatiwa. Leo nikiangalia nchi nyingi Ulaya au Marekani demokrasia zao zinalalia hapo. Tofauti na nchi za Afrika kupitia vyama vingi vya siasa havipo katika mlalo huo.

Kwa mfano Chama cha Democratic cha Marekani kitapambana vikali na Chama cha.Republican wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu. Chama kimoja wapo kikishindwa hufunga “vituko” vyake ili kuipa serikali ya chama mshindi kutekeleza sera na mipango yake kwa faida ya Wananchi.

Hali kadhalika Uingereza. Labour Party au Conservative, chama kinachoshindwa hufunga “vitimbi” vyake na kukipa nafasi chama kilichoshinda kutekeleza na kusimamia mipango yake kwa lengo na kustawisha masilahi ya wananchi.

Afrika tunaaminishwa kufanya kinyume chake cha kuendeleza visa na ghasia na mataifa hayo hayo. Vyama vilivyoshindwa hupata nafasi ya kusherehesha vituko na vitimbi.

Tangu tumalize Uchaguzi Mkuu, Oktoba mwaka jana Chama kilichoshinda kinapokea vitisho na vitimbi kutoka vyama vilivyoshindwa. Katika mazingira hayo haikosi Chama na Serikali yake inajazwa hofu kwamba haipati utii wa kisheria kutoka vyama vya upinzani.

Kadhalika vyama vya upinzani (UKAWA) vinajenga hofu kuwa vinadhalilishwa kidemokrasia na Serikali pamoja na vyombo vyake.  Ukweli kila upande unamuhofu mwenzake. Wananchi tunashuhudia yanayotokea mitaani na Bungeni. Wananchi tunaduwaa.  Na wengine kugawanyika katika kambi mbili hizo. Wapambe wa Ughaibuni wanazidi kupiga chapuo tuparaganyike.

Busara iliyoje kwa mihimili ya taifa, Serikali, Bunge na Mahakama kukaa meza moja kudadavua haya yanayotokea nchini. Tukumbuke Mwalimu kasema, “Demokrasia si sawa na chupa ya soda ya Coca – Cola.”