Karibu katika safu hii mahususi kwa ajili ya kukumbushana na kuelimishana mambo kadhaa yahusuyo sheria mbalimbali, kwa sasa tukiitazama kwa undani Sheria ya Mirathi. Kuifahamu vema sheria hii kutakupa nafasi ya kuepukana na mianya ya uonevu iliyokithiri katika baadhi ya jamii na familia nchini. Tuanzie pale tulipoishia wiki iliyopita…
Maombi ya usimamizi wa mirathi lazima yaeleze bayana juu ya kiasi na aina ya mali iliyoachwa na marehemu; majina na anwani za warithi; sehemu atokayo marehemu na mahali mali zilipo (hii ni muhimu, kwani husaidia kuamua ni mahakamani gani stahiki inaweza kupokea maombi ya ufunguzi wa mirathi).
Wajibu wa Msimamizi wa Mirathi
a.Kufungua shauri la maombi ya usimamizi wa mirathi.
b. Kuainisha na kutambua mali zilizoachwa na marehemu.
c. Kulipa na kukusanya madeni yaliyoachwa.
d. Kugawanya mali kwa warithi kulingana na sheria husika (sheria zisichanganywe).
e. Baada ya mgawanyo wa mali, msimamizi atawasilisha hati inayoonyesha orodha ya mali na jinsi zilivyogawiwa katika mahakama ambayo shauri lilifunguliwa.
f. Kwa mujibu wa Kifungu cha 10 cha Kanuni za Uendeshaji Mirathi katika Mahakama za Mwanzo GN Na. 49/1971 baada ya msimamizi wa mirathi kuchaguliwa na mahakama ndani ya muda usiozidi miezi sita tangu achaguliwe, msimamizi huyo aieleze mahamama kwa kutumia fomu Na. 5 jinsi alivyogawa mali na kulipa madeni.
Msimamizi lazima awe ndugu wa marehemu?
Si lazima. Msimamizi wa mirathi inaweza kuwa taasisi au ofisi fulani kama benki, ili mradi taasisi hiyo ifanye kazi ya kugawanya mali za marehemu kadiri ndugu na warithi watakavyopenda kwa kuzingatia haki na sheria.
Hata hivyo, taasisi za serikali kama Kabidhi Wasii Mkuu au Mdhamini wa Umma hawezi kuteuliwa kushughulikia mirathi inayotawaliwa na sheria za kimila au Kiislamu.
Kwa mujibu wa Sheria ya Kabidhi Wasii Mkuu, Sura ya 27 na Sheria ya Mdhamini wa Umma, Sura ya 31, taasisi hizo zinashughulikia mirathi ambayo sheria inayotumika si ya kimila au Kiislamu, bali ni sheria ya kiserikali.
Wajibu wa Msimamizi wa Mirathi
Kufungua shauri la maombi ya usimamizi wa mirathi, kuainisha na kutambua mali zilizoachwa na marehemu.
Kulipa na kukusanya madeni yaliyoachwa, kugawanya mali kwa warithi kulingana na sheria husika (sheria zisichanganywe), mfano, kama aliyefariki dunia alikuwa ni Muislamu, mali zigawanywe kwa mujibu wa sheria za Kiislamu.
Baada ya mgawanyo wa mali, msimamizi atawasilisha hati inayoonyesha orodha ya mali na jinsi zilivyogawiwa katika mahakama ambayo shauri lilifunguliwa.
Kwa mujibu wa Kifungu cha 10 cha Kanuni za Uendeshaji Mirathi katika Mahakama za Mwanzo GN Na. 49/1971, baada ya msimamizi wa mirathi kuchaguliwa na mahakama, ndani ya muda usiozidi miezi sita tangu achaguliwe, msimamizi huyo aieleze mahamama kwa kutumia fomu Na. 5 jinsi alivyogawa mali ya marehemu na kulipa madeni ya marehemu.
Taratibu za kufungua mirathi iwapo kuna wosia
Mambo yafuatayo sharti yazingatiwe katika kufungua mirathi endapo kuna wosia: Mtu akifariki dunia, kifo kiandikishwe kwa Mkuu wa Wilaya katika muda wa siku 30; kama wosia umemtaja mtu atakayekuwa msimamizi wa mirathi, msimamizi huyo afungue mirathi mahakamani akiwa na wosia ulioachwa pamoja na cheti cha kifo. Kama wosia haukutaja msimamizi wa mirathi husika, utaratibu wa wanandugu kukaa kikao ufanyike na kumteua mtu atakayekuwa msimamizi wa mirathi ila kwa kufuata wosia wa marehemu.
Mahakama kama kawaida itatoa tangazo la mirathi kwa muda wa siku 90 na kama hakuna pingamizi lolote, msimamizi hukabidhiwa barua ya kuhalalisha kugawa urithi na kulipa madeni. Msimamizi atagawa mali kwa mujibu wa wosia.
Msimamizi huyo akimaliza ugawaji wa mali, atapaswa kwa mujibu wa sheria kupeleka taarifa ya ugawaji mali mahakamani na mahakama hufunga jalada.
Barua ya kuomba usimamizi wa mirathi lazima itaje; jina la marehehemu, orodha ya mali za marehemu, majina na anwani za wasimamizi, maskani ya marehemu.
Hii ni muhimu, kwani mirathi hufunguliwa kufuatana na maskani ya marehemu. Aidha, lazima barua hiyo iambatane na cheti cha kifo na wosia. Msimamizi wa mirathi anaweza kuwa mtu mmoja au hata watu wawili wanaweza kuchaguliwa na kushirikiana kufanya usimamizi wa mirathi husika. Ikiwa atachaguliwa mtoto mwenye umri chini ya miaka 18 au mtu mwenye ulemavu kusimamia mirathi, inashauriwa kuwa na wasimamizi wawili kusaidia kuhakikisha usimamizi wa mali zilizoachwa na marehemu unafanyika kwa busara.
Itakuwaje ikibainika msimamizi hatendi haki?
Ndugu au wanufaika wa mirathi husika wanaweza kupeleka malalamiko yao mahakamani na kuomba amri ya mahakama ya kuhakikisha haki inatendeka au kuomba msimamizi aondolewe madaraka ya kusimamia mirathi.
Mirathi inapaswa kufunguliwa pale marehemu alipokuwa anaishi, yaani kama alikuwa anaishi Arusha lakini sehemu aliyozaliwa ni Kigoma, basi kesi hiyo ifunguliwe katika mahakama yenye mamlaka na sehemu husika, yaani Arusha.
Ofisi ya Kabidhi Wasii Mkuu wa Serikali (WAUU/RITA)
Hii ina mamlaka ya kusimamia mirathi pale ambapo marehemu ameacha wosia kwamba mirathi yake isimamiwe na ofisi hii au endapo mahakama itateua ofisi hii kuwa msimamizi wa mirathi.
Haya hutokea endapo kuna pingamizi dhidi ya wasimamizi wa mirathi. Ikiwa marehemu amefariki dunia bila kuacha ndugu yeyote au mtoto, mali zake zitasimamiwa na Kabidhi Wasii Mkuu wa Serikali.
Mali zenye wakfu kama vile msikiti, kanisa pamoja na mali ambazo serikali ina masilahi nazo kama hospitali au shule, zinabakia chini ya usimamizi wa Kabidhi Wasii Mkuu wa Serikali.
0754520109