Timu ya taifa ya Argentina imefanikiwa kutwaa ubingwa wake wa tatu wa Michuano ya Kombe la Dunia baada ya ushindi wa jumla ya mikwaju ya Penalti 4-2 dhidi ya timu ya taifa ya Ufaransa kwenye mchezo uliohitimishwa kwa dakika 120’ kwenye dimba la Lusail International, nchini Qatar.
Katika mchezo huo wa Fainali, Argentina na Ufaransa walitoshana nguvu kwa mabao 3-3 huku mabao ya Ufaransa yote yakifungwa na Mshambuliaji, Kylian Mbappé kwenye dakika ya 80’ kwa Penalti, dakika ya 81’ kwa shuti kali na dakika ya 118’ kwa Penalti pia.
Mabao ya Argentina yamefungwa na Nahodha wa timu hiyo, Lionel Messi kwenye dakika ya 23’ kwa Penalti na dakika ya 108’ wakati bao la pili la timu hiyo lilifungwa na Angel Di Maria dakika ya 36’.
Hata hivyo, Mbappé ameonyesha kiwango bora sana katika mchezo huo baada ya kufunga mabao matatu peke yake na kufunga mabao mawili kwa njia ya Penalti yaliyomshinda Golikipa wa Argentina, Emiliano Martinez katika mtanange huo wa Fainali.
Baada ya Michuano kutamatishwa nchini Qatar, Tuzo ya Mchezaji Bora wa Mashindano (Adidas Golden Ball) imeenda kwa Nahodha wa Argentina, Lionel Messi, huku Mshambuliaji wa Ufaransa Kylian Mbappe akibeba tuzo ya Mfungaji Bora wa Mashindano (Adidas Golden Boot).
Golikipa wa Argentina, Emiliano Martinez ameondoka na tuzo ya Golikipa Bora wa Mashindano (Adidas Golden Glove) huku Enzo Fernandez akiwa mshindi wa tuzo ya Mchezaji Bora Chipukizi.