Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF),umesitisha mkataba na vituo vya kutolea huduma 48 na waajiri binafsi 88 ikiwa ni pamoja na kuwachukulia hatua watoa huduma 139 wa sekta ya afya.
Hayo yamebainishwa leo Julai 11, 2023 na Mkurugenzi Mkuu wa NHIF Benard Konga wakati akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam kuhusiana na kuanza kwa operesheni maalum kwa nchi nzima kupambana na udanganyifu wa baadhi ya wateja wasio waaminifu wanaotumia huduma hiyo.
Konga amesema kuwa operesheni hiyo ambayo awali ilianza na mikoa sita,imebaini mapungufu mbalimbali ikiwemo matumizi mabaya ya kadi ambazo hutumiwa na watu ambao si wanachama wa mfuko huo kinyume na taratibu.
“Kutokana na hali hiyo mfuko umesitisha mkataba na vituo vya kutolea huduma,waajiri binafsi 88 na kuwachukulia hatua watoa huduma 139 wa sekta ya afya kupitia mamalaka zao za ajira yakiwemo mabaraza yao ya kitaaluma,” amesema Konga.
Mkurugenzi huyo amesema kuwa awali lilianza Juni Mosi mwaka huu na kwamba waliingia kwenye vituo vya kutolea huduma ambavyo wana mkataba navyo katika mikoa sita ambayo ni Dar es Salaam,Mbeya,Mwanza,Arusha,Kilimanjaro na Dodoma.
Amesema kuwa pia operesheni hiyo ilibaini wanachama 2,490 ambao wameacha kadi zao vituoni na kuchunguzwa sababu za kutelekezwa kwa kadi zao.
“Mbali na kadi hizo kutelekezwa pia tumebaini wanachana 1,346 wameazimana kadi ambapo wakaguzi wamezikamata na kuanza kuchukua hatua zinazostahiki kulingana na taratibu pamoja na kuchukua hatua dhidi ya wachangiaji wa wanufaika 1197 ambao wamebainika kufanya udanganyifu,” amesema.
Amesema mfuko umechukua hatua mbalimbali ikiwemo kusitisha matumizi ya kadi za wanachama 697, kuamuriwa kulipa gharama za matibabu zilizotumika 325, kuwafungulia mashtaka 67 na kuwaripoti katika mamlaka za uchunguzi 108.
Ameongeza kuwa mfuko pia umezuia matumizi ya kadi 3,589 za wanufaika zilizokuwa na taarifa zenye mashaka na kuwataka kufika kuhakiki taarifa zao kama ilivyoelekezwa awali.
“Mfuko ulitoa tangazo mnamo mwezi Machi kwa makundi mbalimbali kufanya uhakiki wa taarifa zao ikiwemo taarifa za wategemezi wao,zoezi hili ni endelevu hivyo wanachama wanashauriwa kufika ofisini na kuhakiki taarifa hizo, kufanya uchambuzi wa matumizi ya kadi zote zilizobainika,” amesema,”alisema Kongwa.
Amesema hatua nyingine walizochukua ni kuzuia malipo ya huduma zote za matibabu zilizobainika kuwasilishwa kinyume na utaratibu uliowekwa na mfuko.
“Katika kuimarisha mfuko umeongeza wigo wa kuweka watumishi wa mfuko vituoni ili kuimarisha zoezi la uhakiki wa wanachama na utoaji wa huduma.
“Kuongeza wigo wa matumizi ya utambuzi wa wanachama kwa kutumia alama za vidole na sura kwa vituo vya kimkakati ikiwemo Kliniki za Kibingwa, Hospitali ngazi ya Rufaa, Kanda na Taifa.,”amesema Konga.