Na MwandishibWetu, JamhuriMedia, Singida
Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), umepongezwa kwa kuanza utekelezaji wa Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote ambapo kwa sasa wananchi wanajiunga kupitia vifurushi vya Ngorongoro na Serengeti.
Pongezi hizo zimetolewa leo na Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi,Vijana, Ajira na Watu wenye ulemavu Bi. Zuhura Yunus wakati alipotembelea banda la NHIF kwenye maonesho ya Wiki ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi yanayoendelea katika viwanja vya Mandewa mkoani Singida.

“Mnastahili pongezi kwa hatua kuanza kutekeleza sheria hii ambayo tunaomba kila mwananchi awe na bima ya afya ili apate huduma za matibabu bila kikwazo cha fedha,” alisema Bi. Yunus.
Naye Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usalama na Afya Mahala pa Kazi Bi. Khadija Mwenda alifurahishwa na NHIF kushiriki maonesho hayo kwa kuwa suala la afya ni muhimu kwa wafanyakazi na wananchi kwa ujumla.
NHIF inashiriki maonesho hayo kwa lengo la kuhamasisha na kutoa elimu ya umuhimu wa kuwa na bima ya afya ili kuunga juhudi za Serikali katika kuhakikisha wananchi wanakuwa ndani ya mfumo wa Bima ya afya kupitia Bima ya Afya kwa Wote.
Bima ya Afya kwa Wote, Jiunge sasa

