Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia

Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), limefanikiwa kuongeza mapato kutoka sh bilioni 114.42 kwa mwaka 2021 hadi sh bilioni 257.47 mwaka 2022 huku mauzo ya nyumba yakipanda kutoka sh bilioni 29.33 mwaka 2021 hadi kufikia sh 121.95 mwaka 2022.

Hayo yamebainishwa leo Agosti 3, 2022 na Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo, Hamad Abdallah wakati wa kikao kazi na wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari jijini Dar es Salaam ambapo mkutano huo uliandaliwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina.

Mkurugenzi huyo amesema mwaka 2021/22, mapato ya kodi yalipanda na kufikia Sh bilioni 90.76 kutoka Sh bilioni 89.23 mwaka 2020/21.

Aidha,amesema mapato ya miradi ya ukandarasi yamekua kutoka Sh bilioni 25.60 mwaka 2020/21 hadi kufikia Sh bilioni 43. 98 mwaka 2021/22.

Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo, Hamad Abdallah akizungumza wakati wa kikao kazi na wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari jijini Dar es Salaam leo Agosti 3, 2023

“Faida halisi inayotokana na shughuli za shirika iliongozeka hadi kufikia shilingi bilioni 60.7 mwaka 2021/22 kutoka shilingi bilioni 31.7 mwaka 2020/21.

“Ongezeko hili lilienda sambamba na ongezeko la majengo. Hali ya soko la nyumba imeanza kuimarika,” amesisitiza Abdallah.

Abdallah ameongeza kuwa kwa mara ya kwanza tangu kuanzishwa kwa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), linatarajia kuorodhesha hatifungani yake kwenye soko la hisa baada ya kuwa na rekodi nzuri ya mauzo, faida na mapato.

“Ndani ya kipindi cha mwaka mmoja tunakwenda kutoa hati fungani katika Soko la Hisa la Dar es Salaam, itajulikana kama Nyumbani Bond,” amesema mkurugenzi huyo.

Amesema kwamba hati fungani ya nyumba ya NHC sasa iko katika hatua za maandalizi ndani ya taasisi hiyo ambapo pendekezo la kwanza lilikuwa tayari limewasilishwa kwa bodi ya wakurugenzi.

Hata hivyo amesema kuwa thamani ya mali za NHC kama zilivyokaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), zinaonyesha kuwa hadi kufikia Juni 31, 2022 zilikuwa Sh trilioni 5.04.

“Mizania hii imeendelea kukua mwaka hadi mwaka kwa wastani wa asilimia 12 katika kipindi cha miaka mitatu kuanzia 2019. Thamani hii inahusisha vitega uchumi vya majengo na ardhi ghafi inayomilikiwa na shirika ambayo bado haijaendelezwa ikiwa ni pamoja na miradi ya nyumba inayoendelea,” amesema.

Amesema shirika hilo liliweza kulipa kodi mbalimbali inayofikia takribani Sh bilioni 32.4 kwa mwaka 2021/2022 na kulipa gawio serikalini la Sh milioni 750 kwa mwaka 2021/2022.

Akizungumzia utekelezaji wa miradi amesema baada ya kupatiwa kibali na Serikali ya Awamu ya Sita, NHC inaendelea na miradi iliyokwama kwa takribani miaka saba, ambayo ni mradi wa Morocco Square wenye gharama ya Sh bilioni 137) ambao umeshakamilika kwa asilimia 97 na tayari umeanza kupata wapangaji na wanunuzi wa nyumba na mradi wa Kawe 711 utakaogharimu Sh bilioni 105.1.

Kwa mujibu wa Abdallah mradi wa Morocco ni mkubwa utakaohusisha nyumba za kupangishwa, hoteli, kituo cha biashara na ukikamilika utaingizia shirika hilo Sh milioni 850 kwa mwezi na kwa mwaka zaidi ya Sh bilioni tisa.

Aidha amesema shirika hilo linatekeleza mradi wa ujenzi wa nyumba 5,000 za gharama ya kati na chini za mradi wa Samia Housing Scheme (SHS) ambao umefikia asilimia 40 na utagharimu Sh bilioni 466.

“Mradi huu wa nyumba za kuuza na kupangisha unakusudia kuenzi kazi nzuri anazofanya Rais Samia na tunatamani Watanzania waje wamkumbuke kwa miaka mingi ijayo.

Asilimia 50 ya nyumba hizi zitajengwa Dar es Salaam, Dodoma asilimia 20 na mikoa mingine asilimia 30. Tayari asilimia 85 ya nyumba zilizoanza kujengwa zimeshauzwa.

Ametaja miradi ya ukandarasi inayoendelea kuwa ni ujenzi wa majengo ya Ofisi za Wizara nane Jijini Dodoma (awamu ya pili), usanifu na usimamizi wa soko la Kariakoo na usanifu na ujenzi wa jengo la soko la madini (Tanzanite) eneo la Mirerani Manyara.

Katika eneo la ubia, amesema hadi sasa, miradi 24 ya ubia yenye thamani ya Shbilioni 340 imepitishwa na Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika.

Abdallah pia amesema shirika hilo, limekuwa likidaiwa na benki mbalimbali kiasi cha 163 ambazo zimekuwa zikilipwa kwa kuwa limekuwa likiingiza mapato ya Sh bilioni nane kila mwezi kutoka vyanzo vyake mbalimbali.