Na Mwandishi Wetu,JamhuriMedia
Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), limesema limelipa kodi mbalimbali inayofikia takriban shilingi bilioni 22.0 kwa mwaka 2021/2022 pia limelipa gawio Serikali la sh.milioni 750 kwa mwaka 2021/2022.
Shirika limekuwa likichangia kila mwaka gawio la Serikali na kulipa kodi za Serikali pamoja na kujiendesha lenyewe kibiashara bila ya kupata ruzuku kutoka Serikalini.
Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Nehemia Mchechu wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na mwelekeo wa utekelezaji wa NHC kwa mwaka 2022/23 jijini Dar es Salaam.
Msechu amebainishwa kuwa NHC ni shirika la umma lakini halipati ruzuku kwani kwa mujibu wa sheria zao za mwaka 2005 linawataka kujiendesha kibiashara.
“Ni jambo jemaa kuona kuna baadhi ya mashirika machache ambayo yanatoa huduma,mengine yanasimamia biashara ndani ya serikali hivyo sisi tupo kwenye kundi la mashirika yanayotakiwa kufanya biashara’amesema..
Msechu amesema kuwa NHC imejipanga kuendelea kukamilisha ujenzi wa miradi iliyokuwa imesimama ikiwemo mradi wa Morocco Square ambao ujenzi wake upo kwenye hatua za mwisho kukamilika ambao unatarajiwa kuanza kutumika rasmi mwishoni mwa mwezi Machi 2023.
Pia mipango mingine kuwa ni utekelezaji wa mradi wa Samia Housing Scheme (SHS) katika maeneo mbalimbali nchini na ujenzi wa nyumba 560 eneo la Kawe Jijini Dar es Salaam umeanza na ujenzi wa nyumba 240 eneo la Medeli Jijini Dodoma kwa ajili ya kuuza.
Amesema kuwa programu ya nyumba za Samia Housing Scheme(SHS) imelenga kutatua changamoto ya makazi bora kwa watu wa kipato cha chini kati.
“Tunatarajia kuwa asilimia 50 ya nyumba za program hii zitajengwa Jijini Dar es Salaam, Dodoma asilimia 20 na mikoa mingine nchini asilimia 30. Programu hii inayotekelezwa kwa awamu itakuwa na jumla ya nyumba 5000 zitakazogharimu takriban TZS 466 bilioni.
“Programu hii inaenzi kazi nzuri anayoifanya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuijenga nchi yetu kiuchumi na kijamii ambapo kutakuwa na ujenzi wa Shopping Mall ya kisasa jijini Dodoma ili kuweza kuwapa wakazi wa Jiji hilo eneo zuri na kubwa la kujipatia huduma mbalimbali za kijami,” amesema.
Aidha Mchechu amesema kuwa kuhusu mizania ya shirika hilo imefikia kiasi cha shilingi Tril 5.04 ambapo sehemu kubwa ipo katika ujenzi wa majengo mbalimbali.
Amesema kuwa mizania hiyo imekuwa kwa asilimia 12 sambamba na mtaji wao kukua kutokana na thamani ya Mali na uzalishaji ndani ya shirika hilo kuongezeka na kufikia Tril 3.4.
Mkurugenzi huyo amesema kuwa katika huduma za jamii Shirika hilo limejikita katika kurudisha kwa jamii kwa kuwezesha wananchi kupanga nyumba na hivyo kujipatia mahitaji mbalimbali.
Hata hivyo ameongeza NHC imekuwa ikishiriki katika utoaji suala la kukuza elimu na kuboresha sekta ya afya na mahitaji mbalimbali ya kijamii kwa kutoa misaada mbalimbali nchini.