Uongozi wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) unatuhumiwa kukaidi amri ya Mahakama ya Rufani Tanzania, iliyotolewa miaka 13, iliyopita ikiwaamuru kumrudisha katika nyumba au kumlipa afisa mstaafu wa Serikali ya China, Li Jianglan, baada ya kumwondoa bila kufuata taratibu.
Li Jianglan, aliyefanya kazi kama msaidizi wa masuala ya diplomasia ya kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere, alikuwa mwakilishi kutoka serikali ya China.
Akizungumza na JAMHURI, Li Jianglan amesema uongozi wa NHC haukutumia ubinadamu wakati wa kutekeleza jambo la kumwondoa ndani ya nyumba namba 3,5,7 na 9 katika kiwanja namba 103 kilichopo katika Barabara ya Haile Selassie, Masaki, Dar es Salaam.
“Nimeishi hapa nchini kwa zaidi ya miaka 40 hadi sasa, na kufanya kazi mbalimabi za maendeleo, nimekuja hapa nikiwa bado binti wa miaka 20 na kuanza kufanya kazi na Serikali ya Awamu ya Kwanza,” amesema Li.
Li amesema kabla ya kuhamia katika nyumba hiyo, aliingia mkataba na NHC. Mkataba huo ulihusu kufanya ukarabati katika nyumba hizo uliogharimu zaidi ya Sh milioni 10.
Kupitia hukumu ya Mahakama ya Rufani iliyotolewa chini ya jopo la majaji watatu, Jaji Bernard Luanda, Jaji Edward Rutakangwa, Jaji January Msoffe, ilimpatia ushindi Jianling Li.
Amesema walisaini mkataba wa makubaliano ya matengenezo Januari 6, 2003, na kukamilisha matengenezo hayo Oktoba, 2004 na akahamia ndani ya nyumba hiyo kwa zaidi ya mwaka mmoja kabla ya mchakato wa kumwondoa kuanza.
Li amesema Novemba 2004, aliletewa notisi ya kufuta mkataba wake na NHC, akawasilisha malalamikio yake katika uongozi wa shirika hilo bila mafanikio.
“Wakati uongozi wa shirika hilo unaniondoa katika nyumba, hata zile fedha nilizotumia kwenye ukarabati zilikuwa hazijamalizika achilia mbali fedha ya pango niliyokuwa nimelipa,” anasema Li.
Amesema, sehemu ya mkataba wake na NHC ilimtaka alipe pango kila mwezi huku akiendelea kupata punguzo kutokana na fedha aliyotumia kufanya matengenezo.
“Mei 2006 walitoa vyombo vyangu nje ya nyumba kwa kuitumia kampuni ya udalali ambayo ninaitilia shaka – Manyoni Auction Mart – na kunisababishia hasara ya upotevu na uharibifu wa mali yenye thamani ya zaidi ya dola za Marekani 300,000 (sawa na sh milioni 600),” anasema Li.
Akizungumza na JAMHURI, Mkurugenzi Mkuu wa NHC, Nehemiah Mchechu, amesema analifahamu tatizo hilo na kusema shauri bado lipo mahakamani.
“Ni kweli shirika limekuwa katika mgogoro na aliyekuwa mpangaji wake Jianglin Li kwa zaidi ya miaka kumi, lakini shauri bado liko mahakamani, siwezi kuliongelea kwa undani zaidi,” anasema Mchechu.
Mmoja wa wajumbe katika Bodi ya Shirika hilo, Patrick Rutabanzibwa, alipoulizwa juu ya mgogoro huo alikiri kuufahamu na kudai kuwa ulishafikishwa na uongozi kwenye bodi na kujadiliwa.
“Suala hilo ni la muda mrefu lakini kutokana na mfumo wetu wa kikazi, mwenye mamlaka zaidi ya kuweza kulizungumzia kiundani ni Mwenyekiti wa Bodi,” anasema Rutabanzibwa.
Naye Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika hilo, Deo Mmari, amesema mgogoro huo umechukua muda mrefu, huku akikiri suala hilo linafahamika kwa wajumbe wa bodi yake.
“Ni kweli NHC ina mgogoro na mteja wake, Jianglin Li, lakini tulichoelezwa ni kuwa shauri bado lipo mahakamani na ufumbuzi haujapatikana,” anasema Mmari.
Li amesema NHC baada ya kushindwa kesi walikuja na mapendekezo kwamba wamalize tatizo hilo nje ya Mahakama, walifanya hivyo kupitia kwa wakili wake, Fatma Karume, kutoka Kampuni ya uwakili ya IMMMA, wakitaka kumlipa Li Sh milioni 150.
Amesema katika mapendekezo ya NHC, walitaka wamuuzie nyumba moja iliyopo Kigamboni yenye thamani ya Sh milioni 60, na fedha zinazobaki wampe lakini hawakuelewana kutokana na hasara waliyomsababishia.
Wakili Fatma Karume aliyekuwa mwakilishi wa mlalamikaji, amesema hawezi kueleza kwa undani kuhusu shauri hilo lililokaa mahakamani zaidi ya miaka 10.
“Miiko yangu ya kitaaluma hainipi nafasi kutoa siri za mteja bila ya idhini yake… naomba tuliache suala hilo,” amesema Karume.
Msajili Mwandamizi wa Mahakama ya Rufani Tanzania, John Kahyoza, amesema kwa kawaida shauri linapokuwa limetolewa uamuzi wa kisheria ngazi ya Mahakama ya Rufani huwa ni mwisho na kinachotakiwa kufuata ni utekelezaji tu.
“Hukumu haiwezi ikatolewa na jopo la majaji watatu au zaidi halafu urudi kukata rufaa kwa jaji mmoja hilo halipo kisheria, hapa kwetu Mahakama ya Rufani ndiyo ngazi ya mwisho,” amesema Kahyoza.