*Mtaji wake sasa wagonga shilingi trilioni 5.4

*Ndilo shirika la umma tajiri zaidi kwa sasa

*UN-HABITAT watoa mkopo nyumba nafuu

*Warejesha ofisi zao zilizofungwa Tanzania

 Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) ambalo ndilo shirika la umma mama hapa nchini, thamani yake ya mtaji sasa imefikia Sh trilioni 5.4.

Hayo ni kwa mujibu wa taarifa ya Mkurugenzi wa Fedha wa NHC, Adolph Kasegenya, kwenye kikao baina ya NHC na ujumbe wa Shirika la Makazi Afrika (Shelter Afrique) kilichofanyika Juni 28, 2022 katika Jiji la Ketowice, Poland ambako kongamano la 11 la miji duniani limefanyika.

Katika kikao hicho, ujumbe wa NHC uliongozwa na Balozi wa Tanzania nchini Kenya ambaye pia ni Mwakilishi wa Kudumu wa Shirika la Makazi Duniani (UN-Habitat) lenye Makao Makuu jijini Nairobi, Kenya, Dk. John Simbachawene.

Kasegenya anasema mtaji wa nyumba wa NHC unaofikia Sh trilioni 5.4 unaliwezesha kukopesheka, hivyo uongozi mpya wa NHC unalenga kuwezesha ujenzi wa miradi ya nyumba za gharama nafuu kwa watu wa kipato cha kati na chini ili kutoa fursa kwa Watanzania kumiliki nyumba, lakini changamoto iliyopo ni kupata fedha za kugharimia miradi hiyo.

Anasema NHC imeuona umuhimu wa kuzungumza na Shirika la Makazi Afrika ili ipate mkopo wenye riba na masharti nafuu utakaowezesha kutimiza malengo yake ya kujenga nyumba za gharama nafuu; na kwamba mazungumzo kuhusu mkopo huo yalikwishaanza na sasa umefika wakati wa kuyakamilisha.

Akijibu hoja na maombi ya NHC, Kaimu Mtendaji Mkuu wa Shirika la Makazi Afrika, Kingsley Muwowo, amesema shirika hilo linaiamini NHC kwa kuwa ni mlipaji mzuri wa mikopo na hivi sasa halina deni.

Muwowo anasema kwa kuwa NHC ina ardhi na soko la uhakika la nyumba za gharama nafuu, Shirika la Makazi Afrika liko tayari kukamilisha mazungumzo yaliyokwishaanza kabla ya Septemba, 2022 ili lipate mkopo ulioombwa. 

Kwa upande wake, Balozi wa Tanzania nchini Kenya, Dk. Simbachawene, amelishukuru Shirika la Makazi Afrika kwa kuonyesha nia ya kuisaidia Tanzania kujenga nyumba bora za gharama nafuu.

Ametoa mwaliko kwa wajumbe wa shirika hilo kuzuru Tanzania ili kukutana na NHC na kuona miradi inayohitaji kupatiwa msukumo wa haraka. Mwaliko huo ulikubaliwa na Shirika la Makazi Afrika.

Katika hatua nyingine ya mafanikio, Shirika la Makazi Duniani limekubali ombi la Tanzania la kurejesha ofisi za shirika hilo hapa nchini.

Ombi hilo la Tanzania limetolewa mapema na Balozi wa Tanzania nchini Kenya ambaye pia ni Mwakilishi wa Kudumu wa shirika hilo, Dk. Simbachawene wakati wa kikao cha pamoja kati ya Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), Shirika la Makazi Duniani (UN- Habitat) na Ujumbe wa Tanzania unaoshiriki Kongamano la 11 la Miji Duniani linalofanyika katika Jiji la Ketowice, Poland.

Akijibu ombi hilo la Tanzania, Mkurugenzi wa Shirika la Makazi Duniani, Kanda ya Afrika, Oumar Sylla, amesema sera nzuri na uongozi bora wa Rais Samia Suluhu Hassan unaipa moyo taasisi hiyo ya makazi duniani kuzirejesha ofisi zake nchini Tanzania.

Sylla anasema shirika hilo linaitambua Tanzania kuwa miongoni mwa nchi zitakazokuwa na idadi kubwa ya watu duniani katika miaka michache ijayo, hivyo ni muhimu kuwa na ofisi yake itakayoratibu na kusimamia changamoto za makazi, ukuaji wa miji na idadi kubwa ya watu.

Anasema Serikali ya Tanzania inatakiwa kuandaa mazingira ya kuanzishwa tena kwa ofisi hiyo katika ardhi yake.

Naye Mratibu Mwandamizi wa Miradi ya Uendelezaji Makazi wa Shirika la Makazi Duniani, Kanda ya Afrika, Ishaku Maitumbi, anasema shirika hilo kwa kushirikiana na UNDP, limesaidia baadhi ya Serikali za Mitaa nchini ambazo tayari zina mipango ya vipaumbele vya maendeleo na mipango miji kuzijengea uwezo na kuibua miradi.

Anasema dola milioni 30 za Marekani zinatumika kugharamia miradi katika halmashauri za Serikali za Mitaa 15 zilizopo mikoa sita ya Dodoma, Mara, Mwanza, Simiyu, Tanga na Mtwara.

Maitumbi anavitaja vigezo vilivyotumika kutoa misaada kwa halmashauri hizo kuwa ni kiwango cha umaskini na mahitaji yake, uwezo wa kutekeleza miradi katika mikoa husika, na uwezekano wa miradi iliyowekezwa kuwa endelevu.

Mkuu wa Utafiti wa UNDP Tanzania, Godfrey Nyamrunda, ambaye pia alipata fursa ya kuzungumza anasema, miradi hiyo ina manufaa makubwa na amezitaka Mamlaka za Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kusimamia kikamilifu miradi inayosaidiwa na taasisi hizo mbili ili iwe na manufaa kwa nchi.

Akizungumza katika kikao hicho, Balozi wa Tanzania nchini Ujerumani, Dk. Abdallah Possi, amesema ili miradi inayosaidiwa iwe na manufaa, ni lazima wanaoisimamia wajengewe uwezo na uelewa hususan unaohusu miji na makazi.

Kongamano la Miji Duniani limefanyika jijini Ketowice, Poland likiwa na washiriki 25,000 kutoka mataifa mbalimbali duniani na kwa sehemu kubwa linajadili changamoto za miji na namna ya kuziondoa ili kuwa na miji bora na salama kwa vizazi vijavyo.

Imeelezwa katika kongamano hilo kuwa ifikapo mwaka 2050, asilimia 70 ya watu duniani watakuwa wakiishi mijini, hivyo kuna umuhimu wa kuwa na mipango madhubuti ya kukabiliana na changamoto za ukuaji wa miji na ongezeko la watu.

Tanzania inawakilishwa katika kongamano hilo na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi, Halmashauri ya Jiji la Dodoma, NHC, Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART), Wakala wa Barabara za Vijijini (TARURA), Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) na Chuo cha Usafirishaji.

Miradi mbalimbali na vivutio vilivyopo nchini Tanzania vimeonyeshwa katika Banda la Tanzania, ikiwamo filamu ya The Royal Tour.