Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) limejitokeza na kukana kuhusika na ujenzi wa jengo la ghorofa 16 katika Mtaa wa Indira Gandhi, jijini Dar es Salaam, ambalo lilianguka wiki iliyopita.

Taarifa iliyotolewa na Kitengo cha Mawasiliano na Huduma kwa Jamii cha NHC, imesema

NHC; “Mradi huu wa ubia kati ya NHC na M/s Ladha Construction Limited ya Dar es Salaam, ulianza kutekelezwa Februari 4, 2008 ambako Shirika la Nyumba litakuwa na hisa asilimia 25 na mbia ana asilimia 75 mara baada ya mradi kukamilika.”

 

Kwa mujibu wa sera ya ubia iliyoanza kutumika mwaka 1993 na kuhuishwa mwaka 1995 na 2005, NHC ilikuwa ikitoa ardhi ambayo ilikuwa ikihesabika kama asilimia 25 ya mtaji wake kwenye jengo husika, na mbia alikuwa akipata asilimia 75.

 

Mkurugenzi Mkuu wa sasa wa NHC, Nehemia Mchechu, alianza kuongoza Shirika hilo wakati mkataba huo, na mingine ya aina hiyo, ikiwa imeshaanza kutekelezwa. Moja ya kazi zake za awali zilikuwa kuipangua, ambako Shirika lilifanikiwa kufuta mikataba 64.

 

“Kwa mujibu wa mkataba huo, mbia mwendelezaji M/s Ladha Contruction Limited kama walivyo wabia wengine, anapaswa kabla ya kuanza ujenzi kupata vibali kutoka kwenye mamlaka husika, na kuwa na wataalam wa ujenzi na washauri waliokubalika na kuthibitishwa na mamlaka husika.

 

“Aidha, mbia huyu akishapata wataalam hao ndiye anayehusika kuingia nao mikataba ya kazi ya kujenga na kusimamia ubora wa jengo husika kwa mujibu wa sheria. Katika mradi huu mbia mwendelezaji aliajiri wataalam wote waliosajiliwa na mamlaka husika ambazo ni CRB, ERB, AQRB na mansipaa husika na mamlaka nyinginezo. Kwa kuwa ujenzi ulikuwa bado haujakamilika, NHC ilikuwa bado halijapata asilimia 25 ya umiliki wake,” imesema taarifa hiyo.

 

Taarifa kamili ya NHC imechapishwa Uk. 7