“Kutokusamehe ni kama kunywa dawa ya panya na kungoja ili panya afe.”- Anne Lamott.
Alikuwapo msanii mmoja jina lake aliitwa Pablo Picasso 1881-1973, raia wa Hispania. Msanii
huyu alikuwa anataka kuchora kitu kizuri duniani, msanii huyu alimwendea Padre mmoja na
kumuuliza, Baba ni kitu gani kizuri duniani? Kwani ningependa nikichore kwenye turubai langu.
Padre akamjibu akamwambia, kitu kizuri duniani ni ‘imani’. Ni kwa sababu ya imani ndiyo
maana ninaweza kumfanya Mungu awepo altareni kila siku. Lakini ilimpa shida msanii yule
kwani hakujua ni kwa namna gani angeweza kuchora imani juu ya turubai lake.
Akawaendea wanandoa wawili na kuwauliza swali lile lile, ni kitu gani ni kizuri duniani? Wao
wakamjibu kwa kusema kitu kizuri duniani ni ‘upendo’, ni kwa sababu ya upendo ndiyo maana
tupo hapa. Msanii yule akajiuliza tena, nitauchoraje upendo kwenye turubai langu?
Msanii yule hakukata tamaa aliendelea na utafutaji wake, akawaendea askari jeshi wawili na
kuwauliza swali lile lile, basi wao wakamjibu kwa kusema, kitu kizuri duniani ni ‘amani’.
Alitafakari akaona amani, upendo na imani vyote hubeba maana nzuri, lakini nitavichoraje
kwenye turubai langu.
Alijikuta amechoka, akiwa na kiu ya maji aliingia kwenye mgahawa mmoja na pale ndani
alikutana na familia moja. Macho ya watoto yalionesha imani kwa wazazi wao. Na macho ya
wazazi yalionesha upendo kwa watoto wao. Na kwa hali hiyo amani ilikuwapo kwenye familia
ile.
Aliondoka akiwa na furaha na akawa amepata kitu kizuri duniani. Msanii yule alipofika nyumbani
alimwambia mke wake nimepata cha kuchora kwenye turubai langu. Jina la turubai hilo litaitwa
msamaha, kwa sababu wote niliokutana nao nimewauliza maswali ya usumbufu lakini
wakanisamehe kwa usumbufu wangu.
Nilipotoa makala yangu iliyokuwa inasema ‘Tujifunze kupendana na siyo kuumizana’, Katika
gazeti hili la JAMHURI Toleo No. 249, Julai 5-11, 2016. Mwanandoa mmoja ambaye kwa
sababu maalumu sitaweza kulitaja jina lake alinitumia ujumbe mfupi kwa njia ya simu yangu ya
kiganjani. Ujumbe wake ulikuwa unasomeka hivi;
Nimeumizwa! Nimeumizwa! Na tena nimeumizwa sana! William siwezi kusamehe! Labda
nitasamehe nikiwa kaburini…! Sijui kwa nini nilioa. Najuta kuoa. Najuta kufunga ndoa.
Ujumbe huu ni picha ndogo tu ya yale yaliyomo ndani ya nyumba zetu za kitawa, nyumba zetu
za mapadri na nyumba zetu za wanandoa. John Henry Newman alipochaguliwa kuwa Kardinali
wa Kanisa Katoliki, alichagua kaulimbiu inayosema; Moyo unaongea na moyo. Ninaomba
nizungumze na moyo wako kupitia makala hii.
Papa Fransisko anasema; asiyesamehe anaugua kimwili, kihisia na kiroho. Katika makala hii
nitauzungumzia msamaha. Rais wa 16 wa Marekani, Abraham Lincoln, anatupatia uwezekano
wa kuishi kwa msamaha na upatanisho.
Wakati akifanya kampeni za kuwania urais, alitokea mpinzani aliyefanya kila aina ya mbinu ili
kuharibu jina na sifa yake. Huyu mpinzani wake aliitwa Edwin McMasters Stanton. Edwin
McMasters Stanton alikuwa tayari kufanya lolote ili Lincoln asipate nafasi ya kushinda uchaguzi
wa urais. Hata hivyo, Lincoln alishinda na alipokuwa anaandaa Baraza la Mawaziri, jina la
Stanton likawapo. Wasaidizi wa Rais walifanya juhudi kubwa ila bila mafanikio kumweleza Rais
chuki aliyokuwa nayo Stanton dhidi yake. Hata hivyo, Rais alionekana kuzijua wazi mbinu

mbaya za Stanton dhidi yake wakati wa kampeni.
Rais akasema huyu ananichukia mimi ila siyo Marekani. Huyu ana sifa za kuiongoza Marekani
na watu wake. Akamteua kuwa waziri wa ulinzi. Stanton aliposikia uteuzi wake alishangaa
mshangao mkubwa. Akakubali ule wadhifa na akaifanya hiyo kazi kwa weledi mkubwa.
Lincoln aliuawa. Wakati wa maziko yake Stanton alisema, hakika huyu asingeondoa chuki yake
dhidi yangu, leo hii angezikwa huku akiacha adui duniani. Lakini kwa vile roho yake ilikuwa
tofauti na yangu ameacha rafiki duniani.
Kuna mwanaume mmoja alimwambia mke wake, wewe hupiki vizuri kama mama yangu.
Mwanamke akamjibu kwa kusema, na wewe huna pesa kama baba yangu.
Kwa nini tunaumizana? Kwa nini hatusikilizani? Kwa nini tunadharauliana? Ndoa zetu siku hizi
zina mashindano kama ya vyama ya siasa. Kila mmoja anajiona yupo sawa, hakuna
anayependa kujishusha, hakuna anayependa kukosolewa. Ule upendo halisi kati ya mke na
mume haupo tena.
Siku moja baba mmoja alimwambia mtoto wake kuwa kila mara anapotofautiana na mama yake
kimtazamo huwa ana neno la mwisho. Mtoto akauliza kwa mshangao, ni neno gani hilo baba?
Baba akatabasamu kisha akamjibu, ‘Ninaomba msamaha.’
Tujiulize; kuna faida yoyote ile anayopata mtu baada ya kukataa kusamehe? Jibu ni hapana.
Kuna faida yoyote anayopata mtu baada ya kukataa kupokea msamaha? Jibu ni hapana. Jaribu
tu kujiuliza; kwanini unashindwa kusamehe?
Msamaha ni zawadi, hebu jaribu kumpa mwenzako zawadi hii. Padri Faustine Kamugisha
anasema, ‘Mshangaze adui yako kwa kumpa zawadi ya msamaha.’ Sharti la kusamehewa ni
kusamehe.
Kila mwanadamu anahitaji kuwa na furaha na amani katika maisha yake. Hakuna mwanadamu
anayetamani kuwa na huzuni muda wote. Hakuna mwanadamu ambaye anapenda kuwa na
msongo wa mawazo muda wote. Lakini unaweza kujiuliza maswali kadhaa; kwa nini tunakutana
na watu ambao maisha yao ni kujilaumu na kuwalaumu wengine? Kwa nini tunakutana na
wanadamu ambao wamejikatia tamaa ya kuishi duniani? Hakuna mwanadamu aliyeshindwa
kusamehe halafu akawa na maisha mazuri.
Katika Biblia Takatifu imeandikwa; Utusamehe makosa yetu, kama nasi tunavyowasamehe
waliotukosea (Mt.6:12). Katika andiko hilo ukweli unabaki kuwa, ili tusamehewe ni lazima na sisi
tuwasamehe waliotukosea.
Msamehe mume wako, msamehe mke wako, wasamehe watoto wako, msamehe jirani yako,
msamehe mwajiri wako, msamehe mfanyakazi wako. Jisamehe wewe mwenyewe. Msamaha ni
kiungo cha amani katika jamii, msamaha ni mlango wa amani katika familia. Msamaha ni
mlango wa amani katika urafiki, samehe usamehewe. Usipende kusamehewa kama wewe
mwenye hupendi kusamehe. Msamaha unatibu majeraha ya chuki, unatibu majeraha ya
ugomvi, unatibu majeraha ya nafsi.
Kama tunahitaji amani ya kweli na ya kudumu lazima tuwe tayari kutoa msamaha na kuupokea.
Tuwe waenezaji wa sera ya msamaha. Papa Yohana wa XXIII anatuhimiza kwa nasaha hii,
‘Wanangu daima tafuteni yale yanayowaunganisha na siyo yale yanayowatenganisha.’
Msamaha unaunganisha. Ukitaka kuwa na furaha maisha yako yote msamehe kila
anayekukwaza. Msamaha ni fadhila ya wenye ujasiri.
Papa Yohana Paulo II alizaliwa tarehe 18 Mei 1920 na aliaga dunia tarehe 2 Aprili, 2005, Papa
Yohana Paulo II alimsamehe Mehmet Ali Agca ambaye alijaribu kumuua tarehe 31 Mei, 1981.
Papa Yohana Paulo II baada ya kumtembelea gerezani alipokuwa amefungwa Ali Agca na
kusema; Tuliyozungumza yatabaki siri yangu na yeye. Nilizungumza na Ali Agca kama rafiki
yangu ambaye nimemsamehe na ambaye nina imani kamili kwake. Huu ni mfano bora ambao

mimi na wewe tunaweza kujifunza.
Hayati Baba wa Taifa la Afrika Kusini, Nelson Mandela, alitumikia kifungo gereza kwa muda
usiopungua miaka 27. Alifungwa si kwa sababu alikuwa mhalifu. Hapana. Alifungua kwa sababu
alikuwa anapigania haki za watu weusi wa taifa lake, alifungwa kwa sababu alikuwa anapigania
uhuru wa taifa lake, alipotoka gerezani alitoa nasaha isiyoweza kusahaulika katika
kumbukumbu za kihistoria alisema; hakuna aliyezaliwa awe na chuki, watu wenye ujasiri
hawaogopi kusamehe kwa ajili ya amani.
Mandela anatukumbusha kwamba chanzo cha amani katika jamii ni msamaha. Kumbuka! Jirani
yako ni yule unayesita kumtakia mema. Jirani yako ni yule ambaye hampikiki chungu kimoja.
Jirani yako ni yule mgonjwa anayehitaji neno lako la kumfariji. Jirani yako ni huyo
aliyehukumiwa kwa miaka kadhaa baada ya kuwa umemshinda kesi mahakamani. Jirani yako
ni huyo ambaye unasita kumpa mkono wa amani.
Hakuna binadamu aliye chini ya jua ambaye ni mkamilifu, sisi sote tulio chini ya jua hatuko
wakamilifu. Pale tunapokoseana, tusameheane, msamaha unatufundisha unyenyekevu. Mtu
mnyenyekevu anafanikiwa kwa kila jambo analoliwazia. Unyenyekevu ni jina jingine la
msamaha. Kanuni ya kwanza ya kufanikiwa ni unyenyekevu, ya pili ni unyenyekevu na ya tatu
ni unyenyekevu.
Tufanye nini ili tuishi maisha yanayoongozwa na unyenyekevu? Mungu ni mwenye uwezo wa
juu kabisa; jinyenyekeze atakushukia, lakini ukijitukuza atakukimbia.
Yule mwovu shetani daima anatamani sana kuharibu picha ya Mungu ndani ya nafsi ya
binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Na picha ya sura hiyo anajaribu kuiharibu
kwa njia ya kuwafanya Watu kuwa wagumu wa kutoa msamaha pale wanapokesewa kidogo au
sana. Kuna wakati inatakiwa utafakari: Unapata faida gani pale unaposhindwa kutoa msamaha
kwa aliyekukosea? Kusamehe waliokukosea kiubinadamu ni jambo gumu sana, lakini ndilo
jambo ambalo na sisi linatupatia matumaini ya kusamehewa na Mwenyezi Mungu aliyetuumba
kwa sura na mfano wake.
Tuepuke dhana ya kuwa na kitabu cha kumbukumbu cha kuandika makosa ya wengine, kama
baadhi ya watu wasingekuwa tayari kuwasamehe wale wanaowakosea dunia ingegeuka kuwa
jehanamu. Ndani ya jamii yoyote hawatakosekana watu ambao wanahasimiana kwa sababu
nyingi na tofauti. Lakini tunapokuwa tayari kutoa msamaha kwa wale waliotukosea tunajiponya
wenyewe na kuwaponya wale wanaohitaji msamaha wetu.
Hatuwezi kuishi pasipo kutoa msamaha au kuupokea msamaha, kumbuka, msamaha unajenga
mahusiano yaliyovunjika. Una kila sababu ya kutoa msamaha, una kila sababu ya kuwa na
amani. Una kila sababu ya kuwa na uhusiano mzuri na familia yako. Una kila sababu ya kuwa
mshauri mzuri, hivyo basi kuwa mwepesi wa kutoa msamaha kwa wanaokukosea. Anza leo
kuomba msamaha kwa Mungu. Anza leo kuomba msamaha kwa uliowakosea. Anza leo
kuwasamehe waliokukosea. Leo hii utakuwa mwana wa Mungu na mbinguni ndiko kutakuwa
nyumbani kwako milele yote.
Nakusihi wewe ambaye umeumizwa na mzazi wako, msamehe. Uliyeumizwa na mtoto wako wa
kuzaa, msamehe, umeumizwa na mume wako, msamehe. Umeumizwa na mke wako,
msamehe. Umeumizwa na kaka yako, au dada yako, msamehe. Uliyeumizwa na jirani, rafiki,
mwajiri wako, msamehe. Kusamehe ni bure. Yawezekana kwa wakati huu mambo yako
hayaendi sawa, una mawazo, hupati usingizi. Unawaza lakini hupati majibu ya mawazo yako,
unahisi umetengwa. Unahisi umekataliwa na familia au jamii. Unakuwa mtu wa kunung’unika
kwa kila jambo.
Nakusihi, usitunze chuki moyoni kwa muda mrefu. Ajabu ni kwamba ukiwa na uvundo mwingi
wa chuki moyoni mwako unaweza ukaanza kuwaza mawazo ya kujinyonga, kulipiza kisasi,
kunywa pombe kupita kiasi ama kunywa sumu. Unapokuwa umeshindwa kusamehe
usitegemee kupata amani ndani ya roho yako. Chanzo cha kukosa furaha katika maisha ni
kutokutoa msamaha kwa waliokukosea.

Familia yako ni familia yako hata kama wamekutenga kwa makusudi. Ukweli unabaki kwamba
bado ni familia yako, usiangalie nyuma. Usiangalie ukatili wa nyuma, angalia mbele. Zingatia
nasaha hii ya Tanushree Podder; Ukiwasamehe wanandugu utamsamehe kila mmoja.
Maisha ya kutokusamehe hayana faida. Yana hasara, maumivu, majonzi na huzuni. Kumbuka
kwamba hupati faida yoyote ile unaposhindwa kusamehe waliokukosea, unaposamehe unapata
faida. Moyo wako unakuwa na amani, unakuwa mtu wa furaha na upendo. Unajikubali ulivyo,
unapata utulivu wa ndani. Unaondokana na mishtuko ya mara kwa mara.
Zig Ziglar anasema; unaposhindwa kusamehe unajisumbua bure, unajiumiza bure, unajitesa
bure na unajidanganya bure. Mungu akusaidie upate kuyaishi vyema uliyoyasoma katika sura
hii. Ubarikiwe sana.