Kila kitu kinachoonekana duniani kilianza na mawazo. Mawazo ndiyo kiwanda kikubwa cha uumbaji wote unaoonekana duniani. Hata katika vitabu vya dini tunaelezwa kuwa Mungu aliamua (Mawazo) kuumba mbingu na nchi.
Ninaposoma Biblia kuhusu habari hizi za uumbaji wa Mungu, kuna kitu huwa najifunza kwa namna ambavyo Mungu aliumba mbingu na nchi. Kimsingi Mungu aliamua kuumba dunia hii pamoja na vyote vilivyomo. Licha ya kwamba tunaambiwa kuwa vitu vyote vilikamilika kuumbwa kwa muda wa siku saba, lakini kutokea kwake kulichukua miezi, miaka na karne nyingi baadaye.
Kwa mfano, baada ya Mungu kutamka kuwa mimea iwepo katika ardhi, tunaambiwa kuwa ili kuota ilibidi mimea hiyo isubiri binadamu aumbwe ili awepo mtu wa kuilima ardhi na kuitunza hiyo mimea. Kuna kitu tunaweza kukipata hapa: Mawazo yako ni ya thamani sana na kila unapowaza na kuamua, mara zote jambo lile huwa limeshaumbika kabisa.
Kwa maana hii yafaa tujifunze kuwa na mawazo ambayo yataumba mambo na vitu tunavyovihitaji pekee na si vile tusivyovihitaji. Jambo jingine la kushika ni kuwa huwezi kutenda kile usichowaza. Matendo yote ni matokeo ya mawazo.
Na kama mtu akisema hutenda pasipo kuwaza, hiyo siyo kweli. Ubongo wa binadamu unazo sehemu kadha wa kadha zinazohusika na kumbukumbu na takwimu mbalimbali. Kila tunachoamua ni matokeo ya taarifa fulani ambazo zimeshakuwamo katika ubongo wetu huko nyuma. Yawezekana hata muhusika akawa hana habari ya kuwa taarifa hizo zipo ubongoni mwake, lakini kutofahamu huku hakuzuii taarifa hizo kuendelea kutumika na ubongo katika kuamua.
Wapo watu ambao hujikuta wanaamua uamuzi wasioupenda ama wanapata matokeo wasiyoyapenda. Tatizo si matokeo, tatizo ni uamuzi ambao yanakuja hivyo yanavyokuja kwa sababu ya taarifa zinazoujaza ubongo wako.
Nimesema kuwa ili upate matokeo unayoyataka ni lazima akili yako ijikite katika kutafakari yale tu unayoyataka. Jambo hili la akili kutafakari yale tu unayoyataka siyo jambo rahisi hata kidogo.
Kwa kawaida asili ya binadamu huongozwa na woga na mashaka. Uamuzi mwingi wa binadamu huweza kutawaliwa na woga na mashaka kuliko kutawaliwa na kujiamini na matumaini. Na kama akili yako isipoona ama kutafakari yale unayoyataka ni vigumu sana kupata matokeo unayoyataka.
Haiwezekani wewe ukawa tajiri ikiwa akili yako inauona na kuuhusudu umasikini. Ni jambo lisilowezekana mtu kuishi kwa amani na furaha ikiwa akili yako inaona kuwa watu wanaokuzunguka ni wabaya. Utapata unachokiona akilini mwako.
Na ifahamike kwamba suala la akili ya mtu kujiweza kufikiria kile unachokipenda siyo kazi rahisi, ni suala linalohitaji bidii nyingi katika uamuzi. Kufikiria kujenga nyumba yako ya kuishi wakati hata kulipa kodi katika nyumba uliyopanga kunakusumbua; inahitaji bidii kubwa.
Ni rahisi kujisemea kuwa ‘sitaweza kujenga nyumba yangu kwa sababu hata kodi tu ya hiki chumba kimoja inanitoa jasho’. Kufikiria kuanzisha biashara wakati hata mtaji huna siyo lelemama.
Na jambo hili la malalamiko ya wengi kuwa hawana mitaji ni matokeo ya namna wanavyowaza. Wanawaza kuwa haiwezekani kupata mtaji, ndicho kinachotokea kwamba wanakuwa hawana mitaji. Kuhusu hili la uwezekano wa kuzalisha fedha na mitaji pasipo kutumia fedha nimeeleza kwa kina katika sura za uchumi ndani ya kitabu changu.
Huwezi kutenda jambo pasipo kufikiria.
Na nimekwishasema kuwa kufikiria unatakiwa kujaza akilini mwako picha, mambo na taarifa unazozihitaji tu ili uwe na matendo unayohitaji. Ni kweli kuwa inahitajika nia ya dhati sana kufikiria kupata cheo kikubwa kabla hujapata ajira. Lakini kama kweli unakitaka hicho cheo huna namna zaidi ya kuwaza kuhusu hicho cheo na siyo kuwaza kuhusu tatizo lako la ajira.
Kufikiria uwekezaji wakati huna hata hela ya kula siyo jambo rahisi, lakini linawezekana. Kutafakari habari za kuwa na familia bora wakati ndoa haioneshi dalili yoyote ya kutengemaa hilo linahitaji akili yenye nia bora.
Ukiwa unaumwa ni lazima uwaze uzima ili uzima ukujie na si kuwaza kuhusu ugonjwa wako. Hii ni kanuni ya kiasili na kiroho na inatueleza kuwa mara zote mtu huvuta na kupata anachokiwaza. Na wataalamu wa saikolojia wanatueleza kuwa ubongo huwa hauna vikanushi. Ubongo unafikiria kwa uelekeo wenye uzani sawa.
Unapotaka joto sema nahitaji joto na kamwe usiseme sipendi baridi. Ukisema sipendi baridi ubongo unarekodi neno baridi na unakuletea baridi badala ya joto. Kama unahitaji maisha mazuri sema ninahitaji maisha mazuri na usiseme sipendi maisha magumu. Ukisema hivyo basi ubongo unarekodi maisha magumu na unakudhihirishia maisha magumu.
Wewe mwenyewe jaribu kuchunguza katika jamii, je, ni watu gani wenye maisha mazuri? Je, ni wale wanaolalamika sana kuhusu maisha ama ni wale ambao hawalalamiki kuhusu maisha? Utakachogundua ni kuwa kadiri mtu anavyotajataja habari za maisha magumu, ndivyo hayo maisha magumu yanavyodhihirika maishani mwake. Kiuhalisia ni kwamba hata kama ungetaja habari za ugumu wa maisha kutoka asubuhi mpaka jioni, hilo halibadilishi ugumu huo wa maisha, badala yake linafanya hali kuwa vile vile na pengine kuwa ngumu zaidi. Kama unataka utajiri sema ninataka kuwa tajiri na usiseme siupendi umasikini. Ukisema habari za kuwa siupendi umasikini ni kwamba ubongo unarekodi neno kuu umasikini na hatimaye unajikuta kuwa umezungukwa na manukato ya kimasikini.
Mawazo yanayoutawala ubongo wako wakati mwingi ndiyo yatakayofanya uwe na fikra za namna fulani. Mfumo wako wa kifikra ndiyo unaoamua aina ya uamuzi unaoamua mara kwa mara. Uamuzi unaoamua unapelekea namna ya kutenda kwako. Namna ya kutenda kwako ndiko kunakopelekea matokeo ya aina yoyote unayoyaona katika maisha yako.
Hakuna jambo wala matokeo yanayokutokea kwa bahati mbaya. Kuna umuhimu pia wa mtu kuwa na fikra za kishukrani katika maisha. Mara nyingi binadamu tunashindwa kupata tunayoyataka kwa sababu ya kutokuwa na shukrani kwa kila tulichonacho.
Nafahamu kuwa wengi tunaamini kuwa kuna Mungu (ingawa aina ya Mungu tunayemwamini inaweza kutofautiana kutoka imani hadi imani). Hata hivyo katika imani zote duniani waumini wake hufundishwa kuwa na moyo wa shukrani. Moyo wa shukrani ni matokeo ya fikra za shukrani. Ni vigumu sana kumshukuru Mungu ama binadamu mwenzio ikiwa huna fikra za shukrani. Mara zote fikra za kishukrani huwa hazilalamiki wala kunungunika, hazilazimishi wajibu wala hazipuuzi haki.
Ili kuweza kuwa na mawazo sahihi yatakayokupeleka kwenye uamuzi sahihi katika kila jambo, ni vema sana kuwa na fikra za shukrani. Isisahaulike kuwa maneno yanayomtoka mtu huwa ni matokeo ya fikra zilizoijaa akili yake. Kwa jinsi hii ni kwamba mawazo yetu na uamuzi wetu uwe ni ule unaosapoti picha nzuri zilizomo vichwani mwetu.
Ukitaka kufanikiwa kiuchumi na kimaisha kwa ujumla, hakikisha unakuwa na mfumo chanya wa mawazo.