Uongozi wa Baraza la Wafugaji Ngorongoro mkoani Arusha umepinduliwa.

Waliochukua hatua hiyo wanawatuhumu viongozi hao kwa ufisadi na matumizi mabaya ya fedha na rasilimali za baraza hilo.

Uongozi wote wa juu umeondolewa. Walioondolewa ni Mwenyekiti wa Baraza la Wafugaji, Edward Maura; Makamu Mwenyekiti wa Baraza, Shutuk Kitamwas na Katibu wa Baraza la Wafugaji, Johanes Tiamasi.

Taarifa ya waendesha mapinduzi hao iliyosainiwa na Lengai Moluo imewataja walioziba nafasi hizo kwa muda wa mpito kuwa ni Lengai Moluo (Mwenyekiti), Daniel Orkey (Katibu); Emmanuel Tonge (Mweka Hazina) na naibu wake ni Rokoine Moti.

Moluo amezungumza na JAMHURI na kusema kikao kilichowang’oa viongozi hao kiliketi Agosti 7, mwaka huu katika hosteli ya Lutheran mjini Karatu; na kwamba kilihudhuriwa na wajumbe 56 miongoni mwa idadi kamili ya wajumbe 72.

“Tupo kwenye mchakato wa uchaguzi, lakini tumeona kwanza tushauriane na serikali katika ngazi ya tarafa, wilaya na wataalamu wa masuala haya. Chanzo cha sisi kufanya haya mabadiliko ni baada ya kuona kuna uvunjifu mkubwa wa katiba ya Baraza la Wafugaji Ngorongoro na usimamizi mbaya wa rasilimali. Tunajua vitisho vipo, havikosekani, lakini yote hayo tuliyatarajia,” amesema Moluo.

Baada ya kutolewa taarifa ya ‘kufutwa’ kwa uongozi, Meneja Baraza la Wafugaji, Peter Matele, anadaiwa kutoa taarifa ya kutotambua mabadiliko hayo.

“Ofisi ya Baraza la Wafugaji Ngorongoro inapenda kuwataarifu na kuuhabarisha umma kuwa taarifa na muhtasari uliosambazwa katika mitandao ya kijamii na vyombo vya habari si taarifa sahihi, kwani Ofisi ya Baraza la Wafugaji haina taarifa juu ya mkutano wowote wa kawaida au wa dharura ulioitishwa kwa taratibu za Baraza… Hivyo, uongozi ulioko madarakani ndiyo uongozi halali kwa mujibu wa katiba ya Baraza la Wafugaji Ngorongoro,” imesema taarifa hiyo iliyosainiwa na Matele.

Chanzo cha mvutano

Wajumbe hao 56 kwenye kikao chao waliainisha baadhi ya mambo wanayosema yamewasukuma kuung’oa uongozi wa baraza. Mambo hayo ni:

1: Ukiukwaji wa katiba ya Baraza la Wafugaji Ngorongoro.

2: Kusitishwa kwa mchakato wa mabadiliko ya katiba ya Baraza la Wafugaji bila maelezo.

3: Kupuuzwa kwa maoni na maelekezo ya wajumbe wa kamati tendaji ya Mei 30, 2018.

4: Kuzorota na kutofanya kazi kwa hosteli ya Baraza la Wafugaji pamoja na watumishi wanaolipwa mishahara bila kuzalisha.

5: Matumizi ya mafuta na magari ya Baraza la Wafugaji kwa shughuli binafsi kinyume cha sheria na taratibu.

6: Kuzorota kwa uhusiano kati ya Mamlaka (NCAA), Baraza la Wafugaji  na wadau wengine muhimu.

7: Matumizi ya fedha za vikao bila idhini ya wajumbe.

8: Kuandaliwa malipo hewa ya wajumbe.

9: Matumizi mabaya ya madaraka yasiyoainishwa na katiba wala Baraza la Wafugaji.

10: Kutoonekana Sh milioni 100 za mkataba wa Rhino Lodge.

11: Uamuzi mkubwa wenye athari kwa baraza na jamii kufanyika nje ya vikao kinyume cha katiba ya Baraza la Wafugaji.

12: Kupitisha matumizi ya fedha za shamba la Hanang (Bassotu) bila kupitia vikao halali vya Baraza la Wafugaji.

13: Watendaji wa Baraza kunyimwa kutekeleza majukumu yao kwa uhuru/kitaalamu kwa mujibu wa katiba.

14: Kufukuza na kuajiri watumishi bila kupitia vikao halali vya Baraza la Wafugaji.

15: Kukiukwa kwa utaratibu wa mwaliko wa vikao kwa mujibu wa katiba ya Baraza la Wafugaji kinyume cha ibara ya 8:10 ya katiba ya Baraza la Wafugaji.

16: Kukiukwa kwa utaratibu wa makusanyo na ukopaji wa fedha za mahindi na urejeshwaji; na

17: Viongozi kuwagawa wajumbe wa Baraza la Wafugaji kwa masilahi binafsi.

Taarifa hiyo inasema baada ya kujadili hoja na kutilia maanani jukumu la Baraza la Wafugaji kisheria, kikatiba na masilahi mapana ya jamii ya wafugaji ndani ya Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro, wajumbe wa Baraza la Wafugaji kwa kura 56 kati ya wajumbe 72 wa Baraza la Wafugaji wameamua kwa dhati kufanya ‘mapinduzi’ kwa kuwaondoa viongozi wa baraza hilo.

Wanadai kuwa Maura ameshindwa kutimiza matakwa ya kikatiba ya baraza, hivyo ameshindwa kutekeleza wajibu wake kama kiongozi wa baraza.

Wajumbe hao wametangaza majina matano ya kamati iliyoundwa kuchunguza tuhuma zilizoainishwa dhidi ya viongozi waliopinduliwa.

Wajumbe hao ni: Emmanuel Shangai (Mwenyekiti), Gabriel Lohay (Katibu), Lazaro Saitoti (mjumbe), Daniel Lormunyei (mjumbe) na Godfrey Lelya (mjumbe). Kamati hiyo imepewa wiki mbili – kuanzia Agosti 7, 2018 – kuwasilisha taarifa ya uchunguzi.

“Kuanzia leo (Agosti 7) unaelekezwa na Baraza la Wafugaji kufanya kazi na uongozi mpya ulioainishwa. Pia unajulishwa kuwa viongozi waliovuliwa madaraka wanakoma kutoa maelekezo yoyote kwa ofisi yako,” inasema nakala ya barua iliyopelekwa kwa Kamishna wa NCAA, Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mwenyekiti wa Bodi ya NCAA, Mbunge wa Ngorongoro na kwenye mbao za matangazo kwa umma.

 

Wajumbe waliohudhuria kikao kilichofanyika Agosti 7, 2019 katika Hosteli ya Lutheran, Karatu 

1: Lengai Moluo 

2: Daniel Orkery 

3: Emmanuel Shangai

4: Lohay Gabriel 

5: Daniel Lormunyei 

6: Jemis Ndete 

7: Mwato Olesikai 

8: Metui N Sabore 

9: Moinga Tobiko 

10: Simon Saitoti 

11: Agustino Siando 

12: Joshua B Oleiti 

 13: Maria Gutamuhoga  

14: Kilimbei Sabore 

 15: Ngoilila Sangau 

  16: Siwan Nengiok 

  17: Manie Osokoni 

  18: Meleji Olesikoony 

  19: Julius Ngoshiyte 

  20: Mbirias Olerinya 

  21: Edward Mbesere 

  22: Kilimbei Lembeu 

  23: Ikonet Kerai 

  24: Olturur Nairaba 

  25: Godwin Olemoirr 

  26: Reteti Raposhi 

  27: Samwel Saunyi 

  28: Langalay Lesasi 

  29: Roimen Lelya 

  30: Larangi Sindila 

  31: John Turmey 

  32: Mbai Sung’are 

  33: Agustino Rumay 

  34: Gidungush Gitigan 

  35: Thomas Marite 

  36: Gwandaja Gidamusungu  

  37: Kiseyan Mwasuni 

  38: Kayeni Kimaay 

  39: Gidanigi Bwanahodi  

 40: Kelai Lormunyei 

  41: Sakai Maya 

  42: Nasanya Sapuro 

  43: Laini Lemasengi 

  44: Nasikare Shuaka

  45: Nalamala Arkaroronjoi

 46: Mbarnoti Tipilit 

 47: Msaba Neoya 

  48: Norkiseya 

  49: Osoin Saitoti 

  50: Lazaro Saitoti 

  51: Sokoine Moir 

  52: Nagol Turere 

  53: Lesikar Tobiko 

  54: Godfrey Lelya 

  55: Simon Lenara 

  56: Nengai Melau 

Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Ngorongoro kimeingilia kati mgogoro ulioibuka katika Baraza la Wafugaji Ngorongoro. Katibu wa CCM wa Wilaya ya Ngorongoro, Amos Shimba, anasema chama hicho hakiungi mkono ubadhirifu, lakini kinapinga staili iliyotumiwa kuwaondoa viongozi wa baraza.

“Hatupingi kuchukua hatua, lakini tunasisitiza taratibu lazima zifuatwe. Wanaotuhumiwa wanapaswa kuitwa na kuambiwa tuhuma zao na wao wapate muda wa kuzijibu. Hiyo ndiyo haki. Kilichofanywa na hao waliotangaza mabadiliko ya uongozi ni uhuni. Hao ni wahuni tu.

“Baraza lina utaratibu wa kisheria na kikatiba, utaratibu huo ufuatwe. Sisi kama chama tunatambua wale walioko madarakani kwa mujibu wa katiba ya baraza, lakini hawa wahuni hapana. Kama kweli wana makosa wapewe nafasi ya kujibu,” anasema.

Mwenyekiti wa Baraza anayedaiwa kupinduliwa, Edward Maura, amezungumza na JAMHURI na kusema hatambui mapinduzi yaliyoongozwa na kundi lililojitangazia madaraka.

“Hakuna ukweli wowote wa mimi na wenzangu kuondolewa. Mimi nimeingia madarakani kwa uchaguzi halali na kwa kufuata katiba ya Baraza la Wafugaji. Kama wajumbe wanataka kuniondoa ni vizuri wakafuata katiba, maana imeweka wazi utaratibu wa kumuondoa kiongozi.

Kwanza ni lazima kuwe na akidi ambayo ni nusu ya wajumbe wa baraza (wajumbe ni 72); pili inatakiwa waandike kusudio la kuniondoa kwa siku 14 na mimi nitoe majibu ya madai au hoja zao.

“Ofisi ya Baraza haijapokea notisi yoyote. Kile kikao walichoketi Agosti 7 ni batili kwa sababu hata wajumbe wenyewe walikuwa safarini wakienda Nane Nane, lakini wakakusanywa Karatu na kusainishwa mambo ambayo wamekuja kujua hayakuwa sahihi,” anasema Maura.

Anasema hoja zote za madai yao zina majibu. “Wafuate katiba, tumebaini kikao walichoketi kilikuwa batili na wajumbe wamekiri kutojua lengo la kikao hicho. Jumatato [kesho] tutakutana ili tuone hatua za kuchukua kwa hao walioendesha mapinduzi hayo batili.”

Mauara anasema kinachoendelea ni matokeo ya siasa. Anamtaja Shangai kuwa aligombea naye uenyekiti, akamshinda na tangu wakati huo amebadilika na kuwa adui yake.

“Saitot (Lazaro) alikuwa katibu mwanzoni, alituhumiwa kula fedha akaondolewa kwenye nafasi yake ili aendelee na kesi yake. Alikuwa diwani kupitia Chadema, akajiuzulu na kurejea CCM. Akataka aendelee na nafasi yake kwenye baraza, lakini katiba inasema ili uwe kiongozi au mjumbe kwenye baraza sharti uwe na nafasi fulani ya uongozi. Yeye akawa si kiongozi kwa hiyo ana chuki. Moluo ana tuhuma nyingi za kupokea fedha za kijiji na kujiwekea kwenye akaunti yake, ameuza rasilimali za kijiji, anachunguzwa na vyombo vya serikali.

“Ameitisha kikao na anachukua hatua bila hata kumsikiliza anayemtuhumu. Uliona wapi hiyo kwenye utawala wa sheria? Lengo lao si kusaidia baraza, bali ni kutubomoa sisi viongozi. Mimi sina wasiwasi wowote – bado ni mwenyekiti halali wa Baraza la Wafugaji Ngorongoro. Kuna NGO [jina tunalihifadhi] inafadhili uasi huu,” anasema Moluo.

Hata hivyo, kuna taarifa kuwa baada ya uamuzi wa wajumbe 56, viongozi kadhaa wa CCM, Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro na Ofisi ya Mbunge wa Ngorongoro walianza kuhaha wakilenga kuonyesha kuwa wajumbe hawakushiriki mapinduzi hayo. Hata hivyo, JAMHURI limepata nakala yenye sahihi za wajumbe walioshiriki mapinduzi hayo.