Siku zilizopita, niliwahi kuzungumzia nafsi inavyoweza kutenda mambo mema au mabaya kutokana na binadamu anavyotaka. Naweza kusema kwa vile binadamu ameumbwa akiwa na silika; hali ya kujitambua na anapata uwezo wa kufanya lolote atakalo.
Nafsi ni roho. Nafsi inayochungwa na kulelewa vyema, hutengeneza binadamu mwema na karimu. Nafsi inapoachwa na kudekezwa, hutengeneza binadamu mwenye choyo na tamaa. Binadamu wa aina hii ya pili huwa katili kwa kiumbe chochote.
Nafsi hutushauri, au hutushawishi au hutusukuma katika mambo ya kufanya, kufuata au kupuuza mwenendo wetu ndani ya jamii ya binadamu. Asili hiyo hutufanya binadamu kuwa ndani ya amali njema au mbaya hapa duniani na kesho ahera.
Kisa nilichoeleza kinafanya binadamu na binadamu kutofautiana katika kutafuta heshima, uongozi au utajiri. Hapo ndipo linapochomoza suala la UTU. Mfalme au kiongozi hupendeza sana kwa watu akiwa na sifa ya utu (ubinadamu).
Nafsi iliyokatili hujifurahisha yenyewe na kujipendelea mambo mazuri ya anasa, kujilimbikizia mali kwa njia isiyo halali. Mfalme au kiongozi huchukiza mno mbele ya watu anaowatawala au kuwaongoza. Hali hii ukweli huondoa upendo na amani kati ya viongozi na wananchi.

Nafsi ya utu imejaa mikono ya heri, haki na uzalendo. Inabeba viongozi wenye huruma, wavumilivu, hekima, busara na mioyo yenye uthubutu na ujasiri. Nafsi za kinyama zina mikono ya dhuluma, uonevu na unyang’anyi. Nayo hubeba wafalme na viongozi wanafiki na wahujumu uchumi wa taifa.

Duniani kuna nchi zenye wafalme, viongozi na wananchi wenye aina hizo za nafsi; ikiwamo Tanzania yenye baadhi ya sampuli ya choyo na tamaa. Nazungumzia wanafiki, dhulumati na makatili. Sifa hizo kwao ni tamu kama asali, ingawa ni chungu kama shubiri kwa raia na wananchi wa kawaida.

Viongozi hao waliobeba sifa za unafiki, waliojaa mikono ya dhuluma na nafsi za ukatili wameifanya Tanzania kuwa nchi ya kimaskini ilhali sivyo. Wananchi wamekuwa mafakiri pasipo sitahiki. Huu ni msiba mkubwa.
Baadhi yao wamediriki kuwa wanafiki na wahujumu wakubwa wa uchumi wetu tuliowakabidhi kuulinda, kuunadi, kuuza na kuuhifadhi. Wametumia uongozi, elimu na weledi wao kazini pamoja na uaminifu wetu kwao, kutuhujumu kiuchumi na kutuweka patupu. Inasikitisha.
Madini, misitu na wanyama ni hazina kubwa tuliyotunukiwa na Mwenyezi Mungu, tusiwe maskini wala ombaomba kwa mataifa mengine duniani. Lakini kilicho mbele yetu leo ni kutembeza bakuli kupewa misaada na huku hali ya maisha ikiwa ngumu kama kuvunja mpingo.

Tuliwaamini. Kumbe hawakuwa na utu wala uaminifu na uzalendo. Wamejaa tamaa na ulaghai. Bado siamini tulifanya makosa kuwachagua na kuwateua kushika madaraka na mamlaka ya kulinda na kuhifadhi uchumi wa Taifa letu. Lakini wenzetu wametukosea makusudi.

Watanzania tunalia mikono kichwani na kusaga meno kwa uchungu kubaini mali inaliwa na wajanja. Loo salala! Nafsi za ndugu zetu (viongozi na wataalamu) zimekubali kughilibiwa kwa kupewa vipande vya mkate na kashata, wakighafilika kutolewa nyongo zao.
Katika kipindi cha miaka takribani 20 (1998-hadi sasa), tumepigwa kweli kweli na kuzamishwa kina kirefu cha dhuluma ya madini, wanyama, misitu n.k. Sababu tuliowaamini kuingia mikataba ya kunadi na kuuza madini yetu kwa mataifa mengine wamefanya purukushani huku wakicheka na kufurahi.

Madhali tumepata nguvu na uwezo wa kuibuka kutoka kina kirefu cha dhuluma ya madini, chini ya kiranja wetu mkuu mwenye nafsi ya UTU na UZALENDO, Rais, Dk. John Pombe Magufuli, tusijilegeze kuibuliwa. Tumshike barabara na tumlinde tuondokane na dhuluma na umaskini.

Tugange yajayo na kuwapeleka ndugu zetu kwenye mikono ya sheria. Mikataba iangaliwe siyo itazamwe. Serikali, Bunge na Mahakama mna dhima kubwa katika ngoma hii. Manju wanahitajika mno sasa kuliko zamani. Samahani mama Tanzania kwa kukuvunjia heshina. Tunatubu kwako.