HARARE, ZIMBABWE

Shirika lisilo la kiserikali nchini Zimbabwe limeishitaki serikali ya nchi hiyo kupinga mipango ya kusafirisha wanyama aina ya tembo kwenda China.

NGO hiyo, Advocates4Earth, inaituhumu China kwa kuwasababishia tembo madhila kwa kutowapatia huduma stahiki.

Katika kesi iliyoifungua katika Mahakama Kuu nchini Zimbabwe, Advocates4Earth inaiomba mahakama kuzizuia taasisi za Zimbabwe Parks na Mamlaka ya Wanyamapori nchini humo kutotekeleza mpango wa kusafirisha tembo kwenda China.

Lenin Tinashe Chisaira, kiongozi mkuu wa Advocates4Earth, anasema shirika lake linataka mamlaka nchini humo kuzingatia sheria zilizopo.

“Kimsingi tunaiomba mahakama itoe amri kua Serikali ya Zimbabwe na taasisi zake zizingatie sheria na mikataba ya kimataifa, hasa mkataba unaohusu tembo wa Afrika wasisafirishwe kwenda maeneo ambako hawatunzwi ipasavyo,” anasema Chisaira na kuongeza:

“Tunaamini kuwa kuna baadhi ya taasisi za serikali zinapanga kukiuka mikataba hiyo kwa kusafirisha baadhi ya tembo wetu kwenda maeneo yasiyofaa kama vile China, bila kufuata misingi ya sheria zilizopo.”

Waziri wa Mazingira wa nchi hiyo, Nqobizitha Mangaliso Ndlovu, ni mmoja wa washitakiwa wanaotajwa katika nyaraka za kesi hiyo.

Idadi ya tembo nchi humo imeongezeka katika miaka ya hivi karibuni hadi kufikia takriban 100,000, jambo ambalo limeanza kusababisha usumbufu kwani baadhi ya wakulima wameanza kulalamika kuwa wanyama hao wanaharibu mashamba yao na maeneo ya malisho.

Hata hivyo, Mamlaka ya Wanyamapori nchini Zimbabwe imekanusha kuwa na mpango wa kusafirisha tembo kwenda China. Tinashe Farawo, msemaji wa mamlaka hiyo anasema tuhuma hizo hazina ukweli wowote.

“Hawa ni watu wanaojaribu kutafuta uhalali wao. Katika hotuba yake Rais [Emmerson] Mnangagwa aliwaonya watu hao. Ni watu wanaotangaza mabaya tu ya serikali. Ukweli utaendelea kubaki kuwa hatukamati tembo wowote hivi sasa kwa ajili ya kuwasafirisha kwenda popote nje ya nchi. Walete ushahidi wa madai yao,” anasema.