ngelejaMbunge wa Sengerema, William Ngeleja, ameahidi wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwamba endapo atafanikiwa kuteuliwa na chama chake na baadaye kuchaguliwa na Watanzania, kazi itakayokuwa mbele yake ni kuhakikisha uchumi wa Mtanzania mmoja mmoja unakua.
Katika mahojiano kati yake na mwandishi wa makala hii yaliyofanyika jijini Dar es Salaam hivi karibuni, Ngeleja anasema; “Hicho ndicho ninachokiamini ili kuleta maana halisi ya manufaa ya kukua kwa uchumi wetu kitakwimu kama ilivyo sasa.”
Anasema Serikali za awamu zilizotangulia zimefanya mambo makubwa yenye manufaa kwa Taifa kutokana na kujenga misingi imara ya kuuwezesha uchumi kupaa hadi kufikia hadhi ya uchumi wa kati ifikapo au kabla ya mwaka 2025.


“Hivyo, jukumu langu kubwa litakuwa kuwawezesha Watanzania kwa kila mmoja kunufaika na ukuaji wa uchumi wetu,” anasema Ngeleja na kuongeza: “Chama kikinipitisha na hatimaye kuwa rais wa nchi nitahakikisha uchumi wa mwananchi mmoja mmoja unakua.”
“Katika hili, lengo langu ni kuimarisha zaidi sekta za kilimo, uvuvi, mifugo na kuimarisha zaidi maslahi ya makundi dhaifu ya mama lishe, bodaboda, machinga, saluni, wapiga debe, mikokoteni na kadhalika,” anasema.
Ngeleja, anayegombea urais kupitia mchakato wa ndani wa CCM unaoendelea hivi sasa, ameahidi kulipa jiji la Dar es Salaam hadhi tofauti ya kiutawala na kibajeti ili kukabiliana na changamoto za foleni na miundombinu mbalimbali zinazolikabili jiji hilo kwa sasa.
Akisisitiza dhamira yake ya kutatua kero ya foleni jijini Dar es Salaam, Ngeleja anasema pamoja na juhudi nzuri za Serikali zinazofanywa kuboresha miundombinu ya jiji hili, hatua zaidi zinahitajika.
Anasema kwamba taarifa za kiutafiti zinaonesha zaidi ya Sh bilioni nne kwa siku zinapotea kutokana na kero ya foleni jijini Dar es Salaam.


Ngeleja anasema kuwa endapo atafanikiwa kupitishwa na chama chake na baadaye akachaguliwa kuwa rais wa nchi, pamoja na mambo mengine, atahakikisha jiji linapewa hadhi tofauti ya kiutawala na kibajeti, hatua ambazo zitaliwezesha kukabiliana na changamoto zilizopo kwa uhakika zaidi.
Ngeleja anasema ukweli kwamba jiji la Dar es Salaam linachangia pato la Taifa letu kwa zaidi ya asilimia 70 na huku likiwa na wakazi zaidi ya milioni tano kwa sasa, ni sababu tosha kabisa kustahili kupewa hadhi tofauti ya kiutawala na kibajeti.
Ngeleja anayetembea na kaulimbiu yake ya “Maono Sahihi, Mikakati Thabiti, Matokeo Halisi” (MMM) ameendelea kuwashawishi wana-CCM wenzake wamwamini huku akijivunia historia ya utendaji wake alipokuwa naibu waziri wa Nishati na Madini kabla ya kuwa waziri kamili kwa takribani miaka mitano na nusu.
Anasema vipaumbele vyake ni vinne – ujenzi wa uchumi imara; utawala bora; huduma za jamii na uimarishaji wa miundombinu.


Kuhusu ujenzi wa uchumi imara, Ngeleja anasema kwa vile sababu za kutoupunguza umasikini kwa kasi zinajulikana kwamba hali hiyo inasababishwa na kasoro ya ukuaji wa uchumi wetu kitakwimu (asilimia 7 kwa kila mwaka kwa karibu miaka kumi sasa) ambao hautokani na sekta ambazo wananchi wengi wamo (kilimo, uvuvi na ufugaji).
Anasema akifanikiwa kupata urais atarekebisha kasoro hiyo kwa kufanya yafuatayo: ataanzisha skimu za umwagiliaji kwa kila wilaya, ataongeza kasi ya kupima ardhi, atasimamia ukulima, ufugaji na uvuvi wa kisasa, ataimarisha vyama vya ushirika, ataimarisha sekta ya viwanda, atajenga mabwawa kwenye maeneo ya wafugaji, na atahakikisha kilimo kinakua kwa walau asilimia 10 badala ya asilimia nne kama ilivyo sasa kwa mwaka.


Ngeleja anasema atatilia mkazo nidhamu ya mapato na matumizi ya rasilimali za Taifa na atapambana na rushwa, ufisadi, na mmomonyoko wa maadili kwa nguvu zote.
Kuhusu michezo na sanaa, Ngeleja anasema kwa vile yeye ni mwanamichezo na mpenzi wa sanaa, atahakikisha kwamba tasnia ya sanaa na michezo inaimarishwa zaidi. Ameahidi kuwa msimamizi mzuri wa Ilani ya CCM pamoja na kuendeleza mafanikio yaliyopo sasa, yaliyoletwa na waasisi wa Taifa letu pamoja viongozi waliofuatia katika awamu zote hadi sasa.


Nini kilitokea Zanzibar? Katika hilo wachambuzi wa mambo wanasema kwamba historia ya utendaji ya wagombea wote wa CCM ilionekana visiwani Zanzibar alikokwenda kusaka wadhamini ili chama kimridhie kuwania nafasi hiyo ya juu kabisa kiserikali.
Wanasema hali hiyo ilibainika visiwani Pemba na Unguja wakati Ngeleja alipokwenda kukusanya wadhamini wa fomu yake kwenye kinyang’anyiro kinachoendelea ndani ya CCM hivi sasa.
Katika kazi hiyo ya kupata saini za wadhamini, Ngeleja alikumbana na faraja hiyo kutoka kwa wadhamini wake waliokuwa wakionesha furaha na imani ya kumuunga mkono, kutokana na namna wanavyomjua kwa umahiri wa utendaji wake, hususan alipokuwa waziri wa Nishati na Madini kwa takribani miaka mitano na nusu.


Kwa mfano, alipofika kuwasalimia viongozi wa CCM Ofisi ya Mkoa wa Magharibi, Mwenyekiti wa CCM wa mkoa huo, Yusuf Mohamed Yusuf maarufu kama ‘Mzee mrefu’, alimwelezea Ngeleja kama kada mahiri wa CCM anayebebwa na historia ya utendaji wake katika mbio hizi za urais.
Mwenyekiti huyo alimsifia Ngeleja kwamba anatosha kwa vigezo vyote kuwa rais wa Jamhuri ya Muungano na akaahidi kumuunga mkono.
Kwenye Ofisi ya Mkoa wa Kusini Unguja, Ngeleja alipata mapokezi ya heshima na kusifiwa kipekee kwa namna  Wazanzibari wanavyokumbuka uchapaji kazi wake.
Mjumbe wa Kamati ya Siasa ya Mkoa wa Kusini Unguja na aliyewahi kuwa Naibu Waziri wa Maji, Nishati na Ardhi (MUNA) kwenye Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Tafana Kasim Mzee, anampamba Ngeleja kwa sifa kemkem kwamba ni mchapakazi, muungwana, mwenye hekima na busara zinazomfanya akidhi vigezo vya kuwa rais wa nchi.


Anawakumbusha Wazanzibari mbele ya vyombo vya habari vilivyokuwa vimeambatana na Ngeleja kwa kutoa ushuhuda kwamba pamoja na changamoto za Shirika la Umeme Zanzibar (ZECO) kudaiwa deni kubwa na Tanesco wakati Ngeleja akiwa Waziri wa Nishati na Madini, hakuwahi kuikatia umeme Zanzibar. Hii ni kwa sababu Ngeleja anaamini katika kutatua changamoto kwa njia ya mashauriano.
Tafana aliendelea kumsifia Ngeleja kwamba hata wakati joto la mjadala kuhusu mafuta/gesi lilipopamba moto na kuelekea kutikisa Muungano wa Taifa kuanzia mwaka 2009 hadi mwaka 2012, Ngeleja alilikabili suala hilo kwa busara na hekima kubwa hadi likamalizika bila madhara kwa ustawi wa Muungano wetu.
Tafana alitumia matukio haya kuelezea imani aliyo nayo kwa Ngeleja kama mzalendo wa kweli, mchapakazi na kiongozi mahiri anayewajali wananchi wa pande zote mbili za Muungano, hivyo, anastahili kuungwa mkono ili hatimaye awe rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Ujumbe wa Ngeleja katika kuwashukuru wadhamini wake; anawaahidi mambo makuu manne wana-CCM endapo atafanikiwa kupitishwa na CCM na hatimaye kuwa rais wa nchi.


Mambo hayo ni kudumisha Muungano, kulinda Mapinduzi ya Zanzibar, kuilinda na kuiendeleza amani ya Taifa na kusimamia kukua kwa uchumi wa mtu mmoja mmoja huku akiapa kupambana na rushwa, ufisadi na mmomonyoko wa maadili.