Wahenga walisema asiyesikia la mkuu huvunjika guu. Kwa Bukoba nilikotokea wanasema ‘akagunjua kalafa tikaulila nzamba’ (ka-mnyama ka-kufa huwa hakasikii baragumu). Baragumu ni njia ya mawasiliano iliyokuwa ikitumiwa tangu enzi. Hata wauza samaki kwa Bukoba huwa wanatumia baragumu (olukuri) wanapotembeza (wanapouza) samaki.

 

Wawindaji wakienda porini, hutumia baragumu kwa ajili ya kuashiria wapi wamemwona mnyama wanayemwinda na kuwapa mbwa wanaofukuza mwelekeo wa alipo mnyama. Sasa kwa mnyama asiyekuwa makini au ambaye siku yake ya kufa ikiwa imefika, badala ya kusikia baragumu akajificha, yeye anatoka hadharani kuchanja mbunga.

 

 

Sitanii, leo nimeona bora nigusie vurugu zinazoendelea katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC). Kwa wanaofahamu historia ya Jumuiya hii, watakumbuka Mwanasheria Charles Njonjo wa Kenya jinsi alivyoshiriki kikamilifu kuvunja Jumuiya ya Afrika Mashariki ya mwaka 1977. Jumuia hii ilivunjika kutokana na matamshi ya Njonjo yaliyokuwa mawazo ya Wakenya.

Njonjo alisema Kenya ndiyo Afrika Mashariki na Afrika Mashariki ndiyo Kenya. Kenya ilionesha dharau kubwa katika Jumuiya kwa kiwango cha Tanzania na Uganda kugeuzwa wanachama daraja la pili. Yale yale yaliyotokea mwaka 1977 yanatokea sasa mwaka 2013.

Rais Paul Kagame wa Rwanda ametumia fursa ya Wakenya kutoipenda Tanzania kwa dhati, wameungana na wamemwingiza mkenge Museveni, sasa Jumuiya inaondoka.

 

Kagame anakataa ushauri wa kuzungumza na waasi nchini Congo, lakini kilichodhihirika Agosti 30, 2013 kimedhihirisha wazi pasi shaka kuwa Kagame ndiye mmiliki wa M23 inayosumbua Congo. Amepeleka vikosi vitatu vya jeshi DRC, vifaru vimepigwa picha vikivuka mpaka kutoka Rwanda kwenda DRC. Hatua hii imethibitisha wazi kuwa madini na mbao za Congo ndiyo chimbuko la utajiri wa Rwanda.

 

Tumeshuhudia sasa wanazindua miundombinu Mombasa bila kumwalika Rais Jakaya Kikwete wakishirikiana na Museveni, tuliyemsaidia kuingia madarakani, ila naamini huyu mzee bado anawapima akili zao.

 

Uhuru Kenyatta sijajua labda anakerwa na kauli ya John Magufuli aliyoitoa kwenye Mkutano wa Raila Odinga kuwa CCM inamuungano mkono Odinga. Anadhani Tanzania ni CCM, hivyo msimamo wa CCM ni msimamo wa Tanzania.

 

Kabla sijaendelea, nimeona ni bora hapa chini nibandike neno kwa neno habari ya Ndugu Manyerere Jackton, aliyoiandika katika Gazeti la Tanzania Daima, Oktoba 6, 2010 alipokuwa ziarani Ngara, mkoani wa Kagera, kama ifuatavyo:-

 

Ngara wapinga Rwanda, Burundi kukaribishwa EAC, Chanzo kikuu ni vita, ukabila, Wasema watavuruga amani nchini

Na Manyerere Jackton, Ngara

WANANCHI katika Wilaya ya Ngara, mkoani Kagera, wanapinga nchi za Rwanda na Burundi kupewa uanachama katika Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Msimamo wa wananchi hao umefahamika kwenye mikutano iliyohutubiwa na Naibu Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk. Diodorus Kamala, juzi.

 

Naibu waziri huyo yuko katika ziara ya kuitambulisha wizara, kueleza fursa zinazotokana na Jumuiya hiyo; na kukusanya maoni mbalimbali ya wananchi, yakiwamo ya ama, Burundi na Rwanda ziruhusiwe kujiunga au zisiruhusiwe.

 

Akiwa katika Kijiji cha Kabanga, wilayani Ngara, ambako ni mpakani mwa Tanzania na Burundi, wananchi walitoa maoni yao kwa uwazi na kupinga kwa nguvu zote Burundi na Rwanda kupewa uanachama kwenye Jumuiya ya Afrika Mashariki.

 

Aliyeanza kutoa maoni yake ni Suleiman Minani, na akasema: “Kujiunga kunahitaji muda, hawa wamekuwa katika mapigano kwa muda mrefu, wametuletea uhalifu, hasa ujambazi. Hapa Ngara ujambazi umeletwa na wakimbizi hawa.

 

“Sisi Watanzania Kiswahili ndicho kitambulisho, Warundi na Wanyarwanda sasa wakizungumza Kiswahili, wanaonekana ni Watanzania.

 

“Kwa nini Serikali inachelewa kutoa vitambulisho kwa raia wake?” alihoji.

Mwananchi huyo alitoa mfano kwa kusema wakati fulani alisafiri na Wanyarwanda kwenda Mwanza. Walifika kwenye kizuizi, na akastaajabu kuona wakitoa kadi za uanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), na kuruhusiwa kuendelea na safari.

 

“Mimi nilipita kwa kitambulisho cha gazeti, hatuna vitambulisho na viwango vya kuoleana ni vikubwa, kule (ng’ambo upande wa Burundi) tuna wajomba, mimi nashauri wasubiri kujiunga kwenye Jumuiya, wakiruhusiwa sasa, usalama wetu utayumba,” alisema.

 

Mwananchi Seleman Senduka alisema: “Kabla ya kuwakaribisha Rwanda na Burundi, kwanza tujue sisi (Kenya, Tanzania na Uganda), tumefaidika vipi na Jumuiya yetu.”

 

Naye Jason Bahina alisema: “Sisi Watanzania hatuna matatizo ya ukabila na vita; wenzetu wanamalizana kwa kuuana. Wanahukumiana kwa kuangaliana pua.

 

“Kabla ya kuwakaribisha, CCM ifanye kwanza kazi ya kisiasa, ijiridhishe kama kweli kujiunga kwao hakutaleta mgogoro. Kilichosambaratisha Jumuiya ya kwanza ni tofauti za kisiasa, kwa hiyo kabla ya kuwakaribisha Rwanda na Burundi, lazima mataifa haya yaeleweke siasa zao.”

 

Mwananchi mwingine, Joseph Balindie, yeye alisema wananchi wana wasiwasi mkubwa kuona Rwanda na Burundi zinataka kujiunga kwenye Jumuiya ya Afrika Mashariki.

 

“Tuna wasiwasi, tabia za wenzetu – kuwashirikisha ni ngumu, wale wanauana, kuwashirikisha si rahisi,” alisema.

 

Naye Gideon Ruvulahende (66), alisema: “Kuungana ni jambo zuri, sasa kama Rwanda na Burundi nao wanataka kuungana na sisi, kwanza wapewe masharti ya kuumaliza ukabila wao.”

 

Japhet Israel (62) alisema kwa umri wake huo, hajawahi kusikia Rwanda na Burundi kuna amani. Alikiri kuwa wananchi katika nchi hizo ni ndugu zetu, na kwamba hata baadhi yao wanafanana na Watanzania, lakini kwa suala la kuwakaribisha kwenye Jumuiya kwa sasa, haliafiki.

 

“Tukiungana tutaharibu usalama wetu, kwanza wajirekebishe, wajue sote tu Waafrika, wajue Watutsi na Wahutu wote ni Waafrika, wajue weupe (Watutsi) na weusi (Wahutu) ni Waafrika, wakijua hivyo, sasa ndipo wakaribishwe kujiunga,” alisema Israel. Ofisa Uhamiaji Mkuu wa Kituo cha Kabanga, Harride Mwaipyana, alitumia fursa ya mkutano huo wa hadhara kutoa maoni yake.

 

“Nipo hapa kuanzia mwaka 1999, nimesoma tabia za pande zote. Tusikurupukie kitu bila kukijua. Sisi Tanzania, Kenya na Uganda tunajuana tabia zetu. “Tabia za hawa wenzetu (Rwanda na Burundi) ni mbaya – hawana amani, wanabaguana, kuna vikao vya usiku vya kujadiliana. Wanakutana kwa mambo ya siri wakitumia vijisherehe, wanaalikana.

 

“Ukiwaingiza hawa, nchi itaharibika, wanapenda kutawala, wanajiona ni bora kuliko mtu yeyote duniani, tusiwakaribishe kabisa. Tuchukue muda mrefu sana. “Mheshimiwa Naibu Waziri naomba ulichukue hili kwa umuhimu wa kipekee. Ujambazi wameleta wao…,” alisema Mwaipyana, akionekana dhahiri kuchukizwa na Rwanda na Burundi kujadiliwa kujiunga kwenye Jumuiya ya Afrika Mashariki.

 

Maoni kama hayo yametolewa na wananchi wengi katika maeneo mengi ambayo Dk. Kamala ameyazuru. Kutoka Gazeti la Tanzania Daima, Ocktoba 5, 2006. Kinachotokea leo kinathibitisha bila chembe ya shaka wasiwasi waliokuwa nao wakazi wa Ngara. Inawezekana Kenya, Uganda, Burundi na Rwanda, na sasa nasikia zimeialika Sudan Kusini kuna jambo wasilotaka kulisema. Na hili mimi nalisema. Hawa wanadhani wakitupa msukosuko kama nchi, tutakubaliana na madai yao ya muda mrefu.

 

Nchi hizi mara zote zimekuwa zikitaka suala la ardhi liwe la Jumuiya ya Afrika Mashariki. Kimsingi hili haliwezekani. Lugha hii inamaanisha kuwa wanataka ardhi ya Tanzania ndiyo ichukuliwe. Ukichukua ardhi ya nchi za Rwanda, Burundi, Kenya na Uganda ukubwa wa eneo la Tanzania bado unazidi nchi hizi kwa wastani wa kilomita za mraba 100,000.

 

Ukiacha ukubwa wa eneo la ardhi ya Tanzania, pia mfumo wa ardhi nchi za Kenya na Uganda, sina hakika sana kisheria Rwanda na Burundi, ila nikisoma kwenye mitandao sioni tofauti kubwa, kwa nchi hizi ni majanga. Nasema ni majanga kwa sababu katika nchi hizi ardhi inamilikiwa na watu binafsi. Siwezi kuthibitisha hili, ila inaelezwa kuwa familia ya Kenyatta inamiliki asilimia 25 ya ardhi yote ya nchi hiyo.

 

Hapa unaweza kuona tatizo lilivyo. Uganda Kabaka anamiliki asilimia kubwa ya ardhi katika eneo linaloitwa Buganda, na hii ina maana kuwa hakuna mtu yeyote anayeweza kugusa ardhi hii wanayoimiliki. Rwanda na Burundi kuna msongamano mkubwa wa watu na hivyo kwao kupata ardhi ya ziada ni mahitaji na si matakwa.

 

Kinachotokea sasa ni kuwa wakubwa hawa wamekuwa sawa na hadithi ya ‘Sungura mjanja’. Wameruka hadi wamechoka mikia, ila sasa wanasema ‘hawazitaki mbichi hizi’. Mwelekeo wa kutususa ninaouona sasa unaelekea katika kuunda Jumuiya ya Afrika Mashariki ‘Academia’. Hapa kuna hatari, manyang’au wawili wakiunganisha nguvu, mwisho wa siku wakikuta hakuna wa kupambana naye wanageukana.

 

Kuna kila dalili kuwa busara isipotawala, Kagame akaona bora aendeleze vita DRC kujipatia utajiri wa Wacongo, hakika sitashangaa vita hii ikisambaa ikaingia Rwanda, hatimaye ikaivunja Jumuiya ya Afrika Mashariki. Je, wewe msomaji unadhani EAC iko kwenye mkondo salama? Nipe jibu.