Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Wakala wa Taifa wa Uhifadhi wa Chakula nchini (NFRA) umesema kuwa unajivunia mafanikio uliyoyapata katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuongeza uwezo wa uhifadhi wa chakula cha akiba na ziada kuuza nje ya nchi.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam hivi karibuni, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka hiyo Dkt Andrew Komba amesema katika kipindi cha miaka minne iliyopita, taasisi hiyo imefanikiwa katika maeneo mbalimbali ya utendaji, ikiwemo kuongeza uwezo wa uhifadhi wa chakula cha akiba na kuuza takribani tani 600,000 za mazao katika masoko ya kimataifa .

“ Katika miaka ya nyuma, NFRA ilikuwa na uwezo wa kuuza kati ya tani 50,000-60,000 katika masoko ya kimataifa,”

“Lakini baada ya Serikali ya Rais Dkt Samia kutuwezesha, uhifadhi wa akiba ya chakula hapa nchini ili kukabiliana na upungufu utakapojitokeza umeongezeka,”

“Lakini pia tumeweza kuuza nje ya nchi chakula cha ziada na hii imesaidia kuinua maisha ya wakulima wetu na nchi kupata faida kutokana na mauzo hayo ya nafaka ya nje ya nchi,” amesema Dkt Komba.

Dkt Komba amesema kuwa katika kipindi cha mwaka wa fedha 2023/2024 NFRA ilikuwa na uwezo wa kuhifadhi shehena ya takribani tani 351,000, lakini hadi kufikia sasa, uwezo wa taasisi hiyo umeongezeka hadi kufikia kuhifadhi tarkiban tani 776,000.

Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Uhifadhi wa Chakula Nchini (NFRA) Dkt Andrew Komba Akizungumza na waandishi wa habari alipokuwa akizungumzia mafanikio yaliyopatikana ndani ya kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Rasi Dkt Samia Suluhu Hassan.

Pia amesema kuwa kupitia mauzo ya nafaka, NFRA imekusanya takribani bilioni 540 ya mauzo ambapo fedha hizo zimekuwa zikitumika katika kupanua maeneo mbalimbali ya utendaji, ikiwemo ukarabati wa miundombinu na maghala.

“Mafanikio haya yanatokana na mizunguko ambayo Rais Samia amekuwa akiifanya katika nchi tofauti tofauti , akitumia nafasi hiyo kuinadi NFRA na kusaidia kupata masoko ya uhakika kwa nchi zenye uhitaji wa chakula,” amesema Dkt Komba.

Ameongeza kuwa kupitia Wizara ya Kilimo, Serikali imeiwezesha taasisi hiyo kuwa na maghala yenye uwezo wa kutunza jumla ya tani 48,000.

“Rais Samia akiwa katika ziara yake ya kikazi mkoani Ruvuma mwaka jana alitukabidhi jumla ya maghala 28 yenye uwezo wa kuhifadhi takribani tani 28,000,”

“ Hivyo serikali kupitia wizara, imetusaidia ujenzi wa maghala yenye uwezo wa kuhifadhi tani takribani 76,000 za chakula” Alisema Dkt Komba.

Katika kutanua wigo wa utendaji, NFRA Katika kipindi cha mwaka wa fedha uliopita ilifanikiwa kuzindua maghala mengine mawili ambayo yalijengwa katika mikoa ya Katavi na Sumbawanga ili kuongeza uwezo wa maeneo ya uhifadhi wa akiba ya chakula.

“Ili kuhakikisha nchi inakuwa na hifadhi ya chakula cha kutosha, Rais Dkt Samia aliiwekea NFRA malengo ya kuwa na uwezo wa kuhifadhi tani 3,000,000 ifikapo mwaka 2030,”

“ Hivyo, Rais Samia , Waziri wa Wizara ya Kilimo Hussein Bashe pamoja na viongozi wengine wamekuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha NFRA inafikia malengo haya ” Alisema Dkt Komba

Amesema katika kipindi cha mwezi Julai hadi Novemba mwaka 2024, NFRA imeweza kununua tani 479,000 kutoka kwa wakulima na manunuzi haya hayajawahi kufanyika katika taasisi hiyo katika miaka ya nyuma.

NFRA ina jumla ya tani 776,000 katika maghala yake ambapo kati ya hizo tani 400,000 zitauzwa katika masoko ya ndani na nje na tani 300,000 zitabakishwa katika maghala kwa ajili ya kulinda usalama wa chakula nchini.

Endapo uzalishaji wa chakula kutoka kwa wakulima utapungua, Dkt Komba amesema NFRA itakuwa na uwezo wa kuilisha nchi kwa mwaka mzima.

“kwa sasa NFRA inashehena yakutosha ambayo itaiwezesha nchi kufanya biashara ya kuuza mazao katika masoko ya ndani na nje pia itaendelea kuwa na shehena ambayo itasaidia kulisha nchi endapo majanga ya njaa au maafa yatatokea”.Alisema Dkt Komba