NAIBU Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Dk Hussein Mohamed Omar ameuagiza Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) kuhakikisha malipo ya wakulima na wafanyabiashara wa mazao wanaouzia wakala huo yanafanyika ndani ya saa 72 baada ya kupokea mazao yao na kuhakiki malipo.

Dk Omar ametoa agizo hilo jana alipotembelea wakala huo uliopo Wilaya ya Babati mkoani Manyara.

Kituo hicho kinaendelea na msimu mpya ununuzi wa mahindi kutoka kwa wakulima kwa bei ya Sh 700 kwa kilo 1 kama alivyoelekeza Rais Samia Suluhu Hassan hivi karibuni akiwa ziarani mkoani Morogoro.

Naibu Katibu Mkuu amezungumza na baadhi ya wakulima wauzaji wa mazao ambao licha ya kufurahishwa na kasi ya kituo hicho kupokea na kupima mazao walilalamikia ucheleweshaji wa malipo.

Ametoa maelekezo matatu kwa ofisa mtendaji mkuu wa NFRA ya kuhakikisha malipo yanafanyika ndani ya siku tatu tangu mkulima au mfanyabiashara alipofikisha mazao yake.

Pia kwa vituo kama Karatu ambavyo havina mizani za kisasa NFRA iongeze idadi ya mizani ili mkulima asikae kituoni muda mrefu kusubiri kushusha mazao yake.

Aidha kwa vituo ambavyo havina sehemu ya kutosha kuhifadhi mazao NFRA iweke utaratibu wa kuondoa mazao yaliyopokelewa kwenda maghala makubwa ili kupisha nafasi ya kutosha kwa wakulima wengine kuleta mazao yao.

Dk Omar ametoa wito kwa wakulima kupeleka mahindi yao katika vituo vya NFRA nchi nzima akiwahakikishia kuwa serikali bado inahitaji mahindi ya kutosha na inanunua kwa bei ya Sh 790 kwa kilo tofauti na kwa walanguzi ambao hununua kwa kati ya Sh 350 na 400 kwa kilo moja.

Msimamizi wa NFRA kituo cha Babati mhandisi Buchunguka Kilanda ameahidi kusimamia maelekezo hayo huku akisisitiza wakulima kukausha vizuri mazao yao kwa kuanika kuondoa unyevu ili kuepuka usumbufu wa kukataliwa mazao yake.