Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amemfuta kazi mkuu wa Idara ya Ujasusi wa taifa hilo kutokana na kushindwa kuligundua shambulio la Oktoba 7, 2023 la Hamas.
Baraza la mawaziri la Israel lilikutana Alhamisi jioni ili kuidhinisha rasmi kufutwa kazi mapema kwa Ronen Bar, ambaye aliteuliwa Oktoba 2021 kwa muhula wa miaka mitano kama mkuu wa Shin Bet.
Netanyahu alitangaza nia yake ya kumfukuza Bw Bar katika taarifa yake ya video siku ya Jumapili, akitaja “kutokuaminiana” kati ya wanaume hao wawili ambao alisema “kumekua baada ya muda”.
Hatua hiyo ilizua hasira na kuchochea zaidi maandamano dhidi ya serikali mjini Jerusalem, ambayo yalishuhudia maelfu ya Waisraeli wakiungana na waandamanaji wanaopinga mashambulizi mapya ya Israel dhidi ya Gaza.
Tangu Jumanne, Israel imeanzisha wimbi kubwa la mashambulizi dhidi ya kile ilichosema kuwa ni wapiganaji wa Hamas katika ardhi ya Palestina, na hivyo kumaliza mapatano tete ambayo yalikuwa yamedumu kwa muda wa miezi miwili.
Shin Bet ni wakala wa kijasusi wa ndani wa Israeli na una jukumu muhimu katika vita. Shughuli na uanachama wake ni siri za serikali zinazoshikiliwa kwa karibu.
Bw Bar ametaja uamuzi wa kumtimua kuwa umechochewa kisiasa. Mwanasheria Mkuu wa Israel Gali Baharav-Miara – mkosoaji mkubwa wa Netanyahu ambaye mwenyewe anakabiliwa na kesi ya kufutwa kazi – alidai kuwa Bw Bar hangeweza kufukuzwa kazi hadi uhalali wa hatua hiyo kutathminiwa.
Barua iliyotumwa na Netanyahu kwa wajumbe wa serikali yake kabla ya mkutano huo ilirejelea “kupotea kwa uaminifu wa kitaalam na kibinafsi” kati ya waziri mkuu na Bw Bar, na kupendekeza kumalizika kwa muhula wake tarehe 20 Aprili.
“Kupotea kwa uaminifu wa kitaaluma kumeimarishwa wakati wa vita, zaidi ya kushindwa kwa uendeshaji wa 7 Oktoba [2023], na hasa katika miezi ya hivi karibuni,” ilisema, ikirejelea mashambulizi ya Hamas dhidi ya Israeli ambayo yalisababisha vita vya Israel-Gaza.
Takriban watu 1,200 waliuawa na 251 kuchukuliwa mateka wakati wa mashambulizi hayo. Israel ilijibu kwa mashambulizi makubwa ya kijeshi, ambayo yameua zaidi ya Wapalestina 48,500, wizara ya afya inayoendeshwa na Hamas inasema.
