Na Mwandishi Wetu, JamhurMedia, Dar es Salaam
BARAZA la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), limewaonya watu wanaojenga miradi bila kupata Cheti cha Tathmini ya Mazingira EIA kwenye baraza hilo kwamba wanakabiliwa na faini ya shilingi milioni 10.
Hayo yamesemwa leo katika Viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam na msosholojia wa Baraza hilo Suzan Chawe wakati akizungumza kwenye ufunguzi wa maonyesho ya kumbukumbu ya miaka 60 ya Uhuru.
Maonyesho hayo yamefunguliwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Abdulla.
Suzan amesema NEMC imekuwa ikifanyakaguzi za mara kwa mara na wale wanaokutwa wamejenga miradi bila EIA wamekuwa wakitozwa faidi inayofikia hadi shilingi milioni 10.
Amesema NEMC imekuwa ikiendesha kampeni ya elimu kwa umma kuhusu umuhimu wa EIA kwa wanaojenga miradi kabla ya kufanyakaguzi na kuwatoza faini.
“Mfano unaweza kukuta mtu anajenga kituo cha mafuta kwenye makazi ya watu jambo ambalo ni hatari kama ikitokea dharura tunaweza kupoteza maisha ya watu kwa hiyo tunasisitiza umuhimu wa EIA kabla ya kuanza shughuli za ujenzi,” alisema Suzan
Alisema kwa miaka 60 ya uhuru NEMC inajivunia mambo mengi ikiwemo kupigania ustawi wa mazingira kwa kuhakikisha miti mingi inapandwa na kulindwa.
Suzan alisema Baraza limefanya maboresho ya mifumo yake ya mapito ya taarifa za tathmini na kaguzi za athari kwa mazingira kwa kuimarisha miundombinu ya TEHAMA kulingana na matakwa ya mfumo wa serikali mtandao.
Alisema NEMC inasimamia miradi inayofanya tathmini ya athari kwa mazingira kwa njia ya kielektroniki kupitia usajili wa mtandaoni.
Alisema njia hiyo inamuwezesha mwekezaji kuanzisha mchakato wa kupata cheti cha EIA kupitia mfumo wa usimamizi wa mradi ( Project Management System).
“Kabla ya kufanya usajili wa mradi mwekezaji anatakiwa kuhakikisha mawazo ya wadau yamepatikana kuhusu utekelezaji wa mradi kwenye eneo husika” alisema Suzan