Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dodoma

BARAZA la Taifa la Hifadhi ya Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Kanda ya Kati imefanikiwa kusajili miradi ya maendeleo 105 na kuipa cheti cha tathmini ya athari kwa mazingira (EIA) katika kipindi cha kuanzia Julai hadi Desemba mwaka jana.

Hayo yalisemwa jana na Kaimu Meneja wa NEMC Kanda ya Kati, Novatus Mushi wakati wa ukaguzi wa miradi mbalimbali ya uwekezaji kwenye kanda ya kati.

Alisema malengo ya kusajili miradi kuanzia Julai hadi Desemba ilikuwa miradi 62 lakini wamefanikiwa kuvuka lengo na kusajili miradi 105 na miradi waliyotarajia kuifanyia tathmini ni 62 lakini wamefanikiwa kuifikia miradi 51.

Mushi alisema ili kutimiza adhma ya Serikali ya kujenga na kupanua shughuli katika makao makuu Jijini Dodoma, Ofisi ya Kanda imekuwa katika msitari wa mbele kuteleza adhma hiyo.

“Kwa kuzingatia mpango huo, ofisi imekuwa ikishauri, kusimamia na kufanya ufuatiliaji wa miradi ya Serikali ili ifikie malengo yaliyokusudiwa kwa mujibu wa Sheria ya Mazingira na taratibu ziliwekwa,” alisema

Alisema NEMC imeshasajili miradi 37 ya serikali ambayo ni majengo nane ya ofisi, majengo matano ya taasisi za elimu, Hospitali/zahanati/vituo vya afya 13, bandari kavu moja, kiwanja cha michezo, kiwanja cha maonyesho, miradi minne ya kusambaza maji, miradi miwili ya kilimo na miwili ya nishati ya jua.

Aidha, alisema kutokana na uhitaji wa huduma mbalimbali za kijamii katika Makao Makuu ya Serikali, Ofisi ya Kanda ya Kati imeendelea kusajili na kufanya tathmini kwa miradi ya uwekezaji ili kufanikisha ukuaji endelevu wa Jiji la Dodoma na maeneo jirani.

Alisema katika kipindi cha Julai-Desemba 2024, Ofisi ya Kanda ya Kati imesajili jumla ya miradi 69 ya uwekezaji ambapo kuna viwanda 15, miradi 21 ya madini, miwili ya kilimo, miradi 11 ya ujenzi, mradi mmoja wa usambazaji maji na miwili ya misitu.

Alisema kwa kipindi cha Julai, 2024 hadi Januari, 2025, Baraza limeshiriki katika kaguzi na tathimini shirikishi za kufuatilia uzingatiaji wa Sheria katika miradi ya kimkakati ikiwemo mradi wa mwendokasi (SGR), mji wa serikali Mtumba, barabara ya mzunguko na miradi ya kilimo ya BBT, ujenzi wa bwawa la maji-Farkwa, ujenzi wa uwanja wa kimataifa wa ndege Msalato.

Alisema ofisi ya Kanda kwa kipindi cha Julai -Desemba, 2024, imefanikiwa kupokea jumla ya malalamiko 24 na kuyapatia ufumbuzi.

Aidha, alisema kati ya malalamiko yaliyowasilishwa, malalamiko yaliyohusu kelele chafuzi yalikuwa ni 14 sawa na asilimia 58% ya malalamiko yote. “Malalamiko ya kelele chafuzi yalihusu kelele zinazotokana na uendeshaji wa maeneo ya starehe, viwanda na nyumba za ibada wakati malalamiko mengineyo 10 yalihusiana na uchafuzi na uharibifu wa mazingira katika maeneo mbalimbali ya Mikoa ya Dodoma, Singida na Iringa,” alisema.

Mushi alisema ofisi za NEMC Kanda ya kati ilifanikiwa kufuatilia na kutatua malalamiko yote 24 yaliyopokelewa kwa njia ya simu, barua pepe au barua kutoka katika maeneo yote yanayosimamiwa na Kanda.

Alisema kwa kipindi cha Julai, 2024 hadi Januari, 2025, Baraza limefanikiwa kutembelea na kukagua jumla ya miradi 603 ya uwekezaji katika Mikoa ya Dodoma, Iringa na Singida sawa na asilimia 75% ya makadirio kwa kipindi cha mwaka wa Fedha 2024/25.

Mushi alisema katika kipindi cha Julai, 2024 hadi Januari, 2025, Ofisi za Baraza Kanda ya Kati zilifanikiwa kupokea maombi matano ya uteketezaji wa vifaa tiba na dawa chotora vyenye uzito wa tani 20 kutoka katika taasisi za umma na binafsi.

Alisema katika kipindi cha Julai, 2024 hadi Januari, 2025, Ofisi za Baraza-Kanda ya Kati zilifanikiwa kupokea maombi matano ya vibali vya ukusanyaji na usafirishaji wa taka hatarishi chini ya tani tano na mpaka sasa maombi yamewasilishwa Ofisi ya Makamu wa Rais kwa ajili ya kupatiwa vibali.

“Pia, kwa kipindi cha Julai, 2024 hadi Januari, 2025, Ofisi ya NEMC Kanda ya Kati imefanikiwa kutoa vitabu vya ukusanyaji taka hatarishi (tracking documents) na kupokea nakala 143 za vitabu vya ukusanyaji wa taka hatarishi vilivyotumika kutoka kwa watu binafsi wenye vibali na kampuni binafsi zenye vibali,” alisema.

Alisema usimamizi thabiti wa kanuni ya taka hatarishi na taka za kielektroniki unasaidia kupunguza athari za kimazingira na pia kuthibiti uharibifu wa miundombinu ya Serikali kama vile miradi ya Shirika la Reli na TANESCO.

“Katika kutimiza agenda ya kuifanya Dodoma kuwa ya kijani, Ofisi ya Kanda imehakikisha kuwa miradi yote inayosajiliwa kwa ajili ya tathmini katika Jiji la Dodoma inatekeleza agenda hiyo. Hivyo, takribani miradi 24 pendekezwa ya uwekezaji kwa Jiji la Dodoma ilipatiwa maelekezo ya kuotesha miti katika maeneo yao,” alisema

Alisema ofisi ya kanda imeshiriki katika kampeni za kupanda miti katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Dodoma na juhudi zaidi za uhamasishaji zimefanyika katika kipindi cha ukaguzi wa miradi ya uwekezaji.