Na Dotto Kwilasa, JamhuriMedia, Dodoma

Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC),limesajili jumla ya miradi 8,058 ya mazingira ambapo kati ya hiyo, 5,784 ni ya Tathmini ya Athari kwa Mazingira (TAM) na 2,274 ni ya Ukaguzi wa Mazingira.

Hayo yameelezwa leo March 24,2025 Jijini Dodoma na Mkurugenzi Mkuu wa NEMC Dkt. Immaculate Sware Semester wakati akizungumza na waandishi wa habari na kueleza kuwa Vikao 3,836 vya wataalam vilifanyika kwa ajili ya kufanya mapitio ya taarifa za TAM na Ukaguzi wa Miradi na kutoa mapendekezo ya maboresho ya masuala ya msingi ya kuzingatiwa katika taarifa hizo.

Amesema Miradi 4,570 iliidhinishwa na kupewa vyeti vya mazingira na kwamba Kati ya hivyo, 3,058 ni vya TAM, 765 ni vya Ukaguzi, huku vyeti vingine vikiwemo vya kubadili masharti 169, vyeti vilivyohamishwa umiliki 552, vyeti vya muda (PEC) 53 na cheti kilichorudishwa (certificate of surrender) ni kimoja.

“Katika kuboresha utoaji wa huduma za vibali vya TAM, Baraza lilianzisha mfumo wa kielectroniki unaotumika kusajili hadi kuidhinishwa kwa miradi ya TAM ambao umeongeza ufanisi,kabla ya mfumo Baraza lilikuwa linasajili takribani miradi 900 kwa mwaka na baada ya mfumo Baraza linasajili zaidi ya miradi 2,000 kwa mwaka, haya ni mageuzi makubwa, “ameeleza

Amefafanua kuwa Usajili na Utoaji Vyeti kwa Wataalam Elekezi wa Mazingira
Katika kipindi cha mwaka 2020/21- 2024/25, Baraza limefanikiwa kusajili wataalam Elekezi wa Mazingira 1,023 na kutoa vyeti vya utendaji kwa Wataalam Elekezi 503 baada ya kukidhi vigezo kwa mujibu wa Kanuni za Usajili na utendaji wa Wataalam Elekezi wa Mazingira za mwaka 2021.

Katika suala zima la elimu kwa umma linalosisitiza masuala ya uhamasishaji na kuzuia Madhara ya matumizi ya mifuko ya Plastiki,Mkurugenzi huyo ameeleza kuwa Baraza limefanikiwa kuandaa vipindi 88 vya uhamasishaji kupitia vyombo vya habari na mikutano 20 ya wadau kuhusu madhara ya matumizi ya mifuko ya plastiki.

“Kaguzi zilifanyika katika maeneo 178 ya uzalishaji na usambazaji wa mifuko ya plastiki, ambapo maeneo 57 yalikutwa na makosa na kuchukuliwa hatua stahiki za kisheria,zaidi ya Tani 150 za vifungashio visivyokidhi viwango vilikamatwa, vikataifishwa na kuteketezwa kwa mujibu wa Sheria,

Hata hivyo suala la udhibi wa vifungashio vya plastiki ni letu sote kuanzia ngazi ya familia hadi Taifa hivyo hatuna budi kushirikiana kwa ajili ya kuleta matokeo chanya, “amefafanua.

Kwa upande wa Kaguzi na Ufuatiliaji wa Uchafuzi wa Mazingira kwa kipindi cha miaka minne amesema jumla ya kaguzi 9,606 zilifanyika na malalamiko 1,483 yalishughulikiwa hasa katika eneo la kelele na mitetemo.

Amesema Uchafuzi wa mazingira ulidhibitiwa katika miradi mikubwa yenye viashiria hatarishi (Bwawa la Mwalimu Nyerere, Bomba la Mafuta ( EACOP), SGR n.k), ambapo programu 50 za elimu na vipindi 75 vya uhamasishaji vilifanyika.

“Vibali vya Mazingira na Ufuatiliaji wa Taka Hatarishi kwa kipindi cha miaka minne vilitolewa vibali 781 kwa wafanyabiashara mbalimbali,pia, nyaraka 1,477 za ufuatiliaji zilitolewa, ambapo 1,089 zilirejeshwa na kufanyiwa mapitio na kubaini kuwa tani 165,834 za taka hatarishi kama chuma chakavu, betri zilizotumika, magurudumu, vioo, mafuta machafu, plastiki na taka za kielektroniki zilifuatiliwa kwa mafanikio kote nchini,”ameeleza.