Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam
BARAZA la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), limeunda timu ya operesheni maalumu ya kufuatilia na kuwachukulia hatua za kisheria wachafuzi wa mazingira na kelele kwenye kumbi za starehe wakati wa sikukuu.
Hayo yalisemwa jana jijini Dar es Salaam na kaimu Mkurugenzi wa Utekelezaji wa Sheria wa baraza hilo, Jamal Baruti, wakati akizungumza na waandishi wa habari kwenye ofisi za baraza hilo Mikocheni.
Alisema timu hiyo itafanyakazi kwa kanda zote za Baraza nchi katika msimu huu wa sikukuu na kwamba kwa Mkoa wa Dar es Salaam na Pwani kutakua na timu ambazo zitakua zikitembelea maeneo yote yatakayo tolewa taarifa kuwa na changamoto za kimazingira na kufanya utatuzi kwa mujibu wa sheria na kanuni husika.
Alisema katika kuhakikisha zoezi hilo linakuwa na ufanisi mkubwa Baraza limejipanga kutekeleza zoezi hilo kwa kushirikiana na Mamlaka za Tawala za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa husika, wanachi pamoja na Mamlaka zingine za Serikali likiwemo Jeshi la Polisi.
“Baraza limejipanga kupokea na kufanyia kazi taarifa zote zinazohusiana na uvunjifu wa sheria ya mazingira kutoka kwa wananchi wema. Baraza kupitia timu yake maalumu ya upokeaji wa taarifa “Call Centre team” itakua ikipokea taarifa mbalimbali juu ya matukio ya uvunjifu wa Sheria ya Mazingirakwa muda wa masaa 24,” alisema.
“Baraza linatoa hamasa kwa Taasisi, kakampuni na watu wote nchini kuhakikisha wanaendelea kuzingatia sheria ipasavyo bila shuruti kwani uchafuzi wa Mazingira wa sauti na mitetemo iliyozidi viwango na utiririshaji wa maji taka ni hatari kwa afya ya Binadamu. Sambamba na hayo, inashauriwa kufuata taratibu za kisheria katika kupata vibali kutoka katika Mamlaka husika kabla ya kufanya mikusanyiko ya sherehe,” alisema.
Alisema Baraza limejikita zaidi katika kuendelea kutoa hamasa na elimu kuhusiana na uzingatiaji wa Sheria ya Mazingira kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kizazi kijacho.
“Kwa wale wote ambao watabainika kukaidi uzingatiaji wa Sheria ya Mazingira na Kanuni zake hatua stahiki za kiutawala na kisheria zitachuliwa,” alisisitiza.
Alisema miaka kadhaa iliyopita katika kipindi kama hiki cha msimu wa sikukuu za krismasi na mwaka mpya (NEMC) ilibaini kuongezeka kwa matukio ya uchafuzi wa Mazingira kwa njia ya sauti na mitetemo iliyozidi viwango pamoja na utiririsha wa maji taka toka viwandani.
Alisema uchafuzi wa mazingira wa namna hiyo umekuwa ukitokea kwa miji mikubwa ambayo inaidadi kubwa ya watu na ongezeko kubwa la shughuli za kiuchumi kama vile Dar es Salaam, Pwani, Arusha, Mwanza, Mbeya na maeneo mengine ya mikoa ambayo inakuwa kiuchumi kwa kasi.
Alisema kuongezeka kwa sauti na mitetemo inayozidi viwango vya kisheria hutokea katika maeneo ya mikusanyiko ya watu na maeneo ya starehe kama vile maeneo ya vilabu (Bar), Kumbi za starehe na maeneo mengine ya mikusanyiko ya watu katika jamii.