Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dodoma
BARAZA la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limekemea vikali matumizi ya vifungashio vya plastiki visivyokidhi viwango ambavyo vimegeuzwa kama mifuko ya kubebea bidhaa sokoni.
Hayo yamesemwa leo na Ofisa Mazingira Mwandamizi wa NEMC, Innocent Makomba wakati akizungumza na waandishi wa habari kwenye maonesho ya siku ya mazingira duniani yaliyofanyika jijini hapa.
Amesema NEMC inaendelea kusimamia Kanuni ya mwaka 2022 iliyoweka katazo la matumizi ya mifuko ya plastiki na wanafanya oparesheni kwenye viwanda vinavyozalisha vifungashio hivyo.
“Kwasasa tunaendelea na oparesheni kwenye viwanda maana huko ndiko kwenye shina, lakini pia watanzania tubadilike tunapokwenda kufanya manunuzi tubebe mifuko yetu inayotakiwa kwa mujibu wa Kanuni ili kuepuka kutumia vifungashio kama mifuko,”amesema.
Ametoa rai kwa viwanda vinavyotengeneza vifungashio hivyo kuacha mara moja na NEMC haitasita kuvichukulia hatua kwa mujibu wa sheria.
“Vifungashio hivi vina athari maana wakati mwingine vinafungashiwa chakula cha moto, inayohatarisha mtu kupata saratani,”alisema.
Kuhusu Tathmini ya Athari za Mazingira, Ofisa huyo alisema NEMC imejipanga kufanya mapitio ya miradi yote ili kuangalia kama imefanyiwa tathmini ya athari kwa mazingira katika kukabiliana na hatari za kimazingira zinazotokana na shughuli za miradi hiyo.
Alisema lengo ni kuangalia miradi iliyofanyiwa Tathmini ya Athari kwa Mazingira (TAM) na ambayo haijafanyiwa tathmini hiyo ili ifanyiwe.
“Lengo ni kuhakikisha athari za mazingira haziharibu ardhi yetu, ustahimilivu wa hali ya jangwa na ukame, tutakachokwenda kufanya kwenye miradi yote iliyofanyiwa tathmini, masharti waliyopewa na Waziri kama yanazingatiwa,”amesema.
Amesema NEMC itaendelea kutekeleza maelekezo ya viongozi katika kusimamia utekelezaji wa Sheria ya mazingira ili kuhakikisha urejeshaji wa mazingira yaliyoharibiwa unafanikiwa.
“Tutahakikisha Sheria yetu inasimamiwa kikamilifu ikiwamo kufanyika kwa Tathmini ya athari za mazingira kwa miradi yote inayokwenda kutekelezwa,”amesema.
Naye, Ofisa Mazingira Mkuu kutoka NEMC, Pendo Kundya, amesema katika maonesho hayo wametoa elimu kwa umma na kupokea maoni namna ya kuboresha mazingira nchini.
“Tumetoa elimu shughuli mbalimbali zinazofanywa na NEMC kama vile tathmini ya athari kwa mazingira, tafiti zinazofanywa za mazingira, udhibiti wa kelele, mifuko ya plastiki na uzingatiaji wa sheria ya mazingira,”amesema.
Amesisitiza wananchi kupenda mazingira na kuyatunza kwa kuwa kila mwananchi ana jukumu hilo na sio kuiachia serikali peke yake