Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam
BARAZA la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Kanda ya Kaskazini limesema limefanisha miradi yote mikubwa kama barabara, viwanda na migodi kuwa na cheti cha Tathmini ya Athari kwa Mazingira (EIA).
Hayo yalisemwa jana na Meneja wa NEMC wa Kanda hiyo, wakati akizungumzia mafanikio ambayo wamepata kwenye kusajili miradi mbalimbali ya uwekezaji.
Alisema NEMC Kanda ya Kaskazini imefanikiwa kuendesha program mbalimbali katika vyombo vya habari kwa lengo la kutoa elimu kwa umma, fursa zilizopo katika mazingira na utunzaji wa Mazingira na majukumu ya Baraza la kwa ujumla.
“Miongoni mwa mafanikio makubwa ni kwamba NEMC Kanda ya Kaskazini imekuwa ikiandaa shughuli mbalimbali za kufanya usafi wa mazingira na upandaji wa miti na kwa muda mfupi tumefanikisha kupandwa miti mingi,” alisema.
Alisema NEMC Kanda ya Kaskazini inasimamia Sera na Sheria za Mazingira kuhakikisha kuwa uchumi wa nchi unakuwa sambamba na uhifadhi wa mazingira.
Alisema wamekuwa wakisimamia utunzaji wa mazingira katika miradi mbalimbali ya kimaendeleo ikiwemo miradi ya huduma za afya ambapo kanda ya kaskazini inasimamia jumla ya miradi ya afya 1286.
Alisema miradi ya shughuli za kiutalii ni 317, miradi ya nishati ni 247, miradi ya viwanda vya mbao ni 201, miradi ya uwekezaji katika viwanda 176 na miradi ya kilimo 118.
Alitaja miradi mingine kuwa ni ya ghala za kuhifadhia bidhaa, vifaa au mali nyingine inayofikia 74, miradi ya ujenzi 27, miradi ya uchimbaji wa madini 26, miradi ya wakulima wa mifugo 12, miradi 11 ya ujenzi wa majengo, , miradi mitano ya mawasiliano na miradi mitatu ya miundombinu.
Alisema Kanda ya Kaskazini inahudumia mikoa mitatu ambayo ni Kilimanjaro, Arusha na Manyara ambapo Makao makuu ya Kanda hiyo yanapatikana katika Mkoa wa Arusha.
Alisema Kanda ya Kaskazini imebarikiwa kuwa na vivutio mbalimbali vya utalii na Mifumo Ikolojia nyeti yenye umuhimu Kitaifa na Kimataifa.
Alitaja maeneo hayo kuwa ni pamoja na maeneo yaliyohifadhiwa kama vile Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro na Hifadhi za Taifa za Tarangire, Mkomazi, Kilimanjaro, Ziwa Manyara na Arusha.
Alisema hiyo pia inahusisha maeneo kadhaa yanayohifadhiwa kama vile Mapori Tengefu, Vitalu vya Uwindaji wa Kitalii na Misitu ya Hifadhi.
Aidha, alisema pia unapatikana Mlima mrefu kuliko yote Barani Afrika (Kilimanjaro) wenye urefu wa Mita 5985 kutoka usawa wa Bahari.
“ Pia kuna uchimbaji wa vito mbalimbali vya thamani ambapo miongoni mwao ni madini ya Tanzanite ambayo yanapatikana Tanzania pekee,” alisema.
Alisema NEMC itaendelea kuongeza uelewa kwa umma kuhusu masuala ya usimamizi wa Mazingira ili Kuhakikisha kunakuwa na Uzingatiaji na Utekelezaji wa Sheria ya Usimamizi wa Mazingira na Kanuni zake katika uendeshaji wa shughuli mbalimbali za maendeleo.
“Tutaendelea kuhakikisha miradi ya maendeleo kabla ya kutekelezwa inafanyika Tathmini ya Athari kwa Mazingira au kwa iliyopo inafanyiwa Ukaguzi wa Awali wa Mazingira, ikiwa ni pamoja na kufanya mapitio ya miradi hiyo ili kupata Cheti cha Mazingira,” alisema
Alisema wataendelea kutoa elimu ya Utunzaji wa Mazingira kwa umma kupitia vyombo vya habari kama radio, televisheni na magazeti na kuendesha na kuratibu tafiti mbalimbali zinazohusu Usimamizi na Uhifadhi wa Mazingira