Katika kitabu chake cha “Long Walk to Freedom”, Nelson Mandela hakuficha kueleza mapenzi yake katika mchezo alioupenda na kuucheza – mchezo wa masumbwi.
Anasema, ingawa niliweza kushiriki kucheza masumbwi nikiwa Fort Hare, nilipoanza kuishi jijini Johannesburg ndipo nilipojiingiza moja kwa moja kwenye mchezo huo. Sikuwa mchezaji mahiri.
“Nilikuwa katika daraja la uzani wa juu, na sikuwa na nguvu wala kasi kubwa. Sikupenda zaidi madhara yaliyosababishwa na masumbwi.”
Anasema alikuwa akivutiwa na namna mcheza masumbwi alivyokuwa akichezesha mwili kwa ajili ya kujilinda dhidi ya makonde ya mpinzani wake, namna mpiganaji alivyoweza kushambulia na kujilinda, namna mchezaji alivyoweza kumshinda mwenzake na sayansi ya mchezo mzima wa masumbwi.
Anautaja mchezo wa masumbwi kama mchezo wenye usawa.
“ Ndani ya ulingo, daraja (uzito), umri, rangi, na utajiri ni mambo yasiyo katika mchenzo wa masumbwi.
Unapopambana na mpinzani wako, ukajua uwezo na udhaifu wake, unakuwa huwazii rangi au hadhi yake katika jamii.
“Sikuhusika na mapambano makali ya masumbwi baada ya kuingia katika siasa. Nikaamua kuwa mkufunzi; nikabaini mazoezi ni mazuri zaidi wasiwasi na msongo uliotokana na mapambano ya masumbwi,” anasema Mandela.
Anasema uamuzi huo ulimfanya awe anaamka na kuingia katika eneo la mazoezi ambako alidumu kwa nusu saa kila jioni ya Jumatatu hadi Alhamis.
“Nilikuwa nikienda nyumbani moja kwa moja baada ya kazi, namchukua Thembi, na kwenda katika Kituo cha Jamii.
Tulifanya mazoezi kwa saa moja, tulikimbia, tulifanya mazoezi ya kuruka kamba, mazoezi ya viungo, ngumi za lashalasha, na kufuatiwa na dakika 15 za mazoezi ya mwili, kunyanyua vitu vizito na hatimaye kumalizia na mpambano.
Kama tulikuwa tukifanya mazoezi kwa ajili ya pambano au mashindano, tulikuwa tukiongeza muda wa mazoezi kwa saa mbili hadi saa mbili na nusu,” anasema.