Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Hanang
Waathirka wa maafa yaliyotokea wilayani Hanang Mkoa wa Manyara, Desemba 3, mwaka huu, wameendelea kunuifaika na misaada mbalimbali ya kibinadamu iliyotolewa na wadau pamoja na serikali, baada ya serikali kuongeza kiwango cha ugawaji wa misaada kwa kaya kutokana na ongezeko la misaada inayoendelea kupokelewa kutoka kwa wadau.
Awali, Serikali ilikuwa ikiwagawia waathirika hao misaada muhimu kama unga, mchele, unga wa ngano, mafuta ya kupikia, sukari, chumvi, maharagwe ya kuwatosheleza kwa kipindi cha mwezi mmoja, pamoja na misaada mingine isiyo ya chakula kama magodoro, mashuka, nguo, mablanketi, mikeka, vyombo vya ndani na vitu mbalimbali, lakini kwa sasa waathirika hao wamezidi kuneemeka baada ya wadau kuzidi kutoa misaada na serikali kuongeza kiwango cha ugawaji ili kuhakikisha misaada yote inayotolewa inawanufaisha walengwa kama ilivyokusudiwa.
Wakiongea na Msemaji Mkuu wa Serikali, Bw. Mobhare Matinyi, ambaye alitumia siku nzima ya Jumamosi Desemba 23, 2023 kutembelea vituo mbalimbali vya ugawaji wa misaada hiyo, waathirika hao wameelezea kuridhishwa kwao kwa misaada wanayopokea na kuwashukuru wadau wote waliochanga pamoja na serikali kwa kuratibu na kusimamia zoezi zima la ugawaji wa misaada hiyo.
Thomas Gabriel Thomas, mkazi wa Katesh A mwenye fsmilia ya watu tisa, ambaye nyumba yake ilijaa tope na kupoteza baadhi ya mali vikiwemo vyakula, anasema kuwa awali serikali ilimpatia mahitaji ya kumtosheleza kwa kipindi cha mwezi mmoja ambayo yalijumuisha maji ya kunywa, unga wa sembe, mchele, sukari, mafuta ya kupikia, maziwa, mayai, unga wa nganio, nguo, mablanketi, shuka pamoja na mikeka lakini kutokana na kuongezeka kwa misaada serikali iliwaita tena kituo cha shule ya msingi Ganana kwenda kupokea misaada zaidi.
“Kwa kweli naishukuru sana serikali ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hasaan pamoja na wadau wote kwa kutushika mkano kwa kiasi kikubwa maana leo (jana) nimeitwa tena kupokea misaada zaidi kama hii unayoiona”, ameeleza Thomas huku akivitaja vitu alivyopokea kuwa ni pamoja na sukari kilogramu 300, unga kilogramu 125, mahindi kilogramu 300, mablanketi nane, mafuta ya kupikia lita 20, mikeka nane, magodoro nane, sabubi za kufulia, mayai, unga wa lishe kwa ajili ya mtoto pamoja na jiko la gesi la uzito wa kilo tano.
Kwa upande wake, Innocent Desdery wa Kijiji cha Gendabi ambacho kwa kiasi kikubwa kiliathiriwa na maporomoko ya tope lililoambatana na mawe na magogo, anaeleza kuwa misaada wanayopata kama waathirka wa maafa imevuka kiwango cha matarajio yao kwa sababu baada ya mgao wa kwanza, wamekuwa wakitangaziwa kwenda katika vituo kupokea misaada zaidi.
“Tumekuwa tukitangaziwa kuja hapa kupokea misaada zaidi na hapa tayari nimepokea mahindi kilo 300, unga wa ngano kilo 150, unga wa mahindi kilo 300, mchele kilo 150, sukari zaidi ya kilo 100, magodoro manne, maharagwe kilo 30, mafuta ya kupikia lita 76 pamoja na vitu vingine kama vyandarua, huka, sabuni, jiko la gesi, dawa za meno, chumvi, maziwa pamoja na maji ya kunywa ya chupa ambayo hata sikuwahi kuwaza siku moja nitakunywa maji ya kiwandani,” ameeleza Innocent.
Baada ya Msemaji Mkuu wa Serikali kutembelea vituo vya kutolea na kupokelea misaada vya shule ya msingi Ganana, kituo cha Katesh pamoja na shule ya msingi Gendabi, Mkuu wa Wilaya ya Hanang, Bi. Janeth Mayanya amesema kuwa wadau mbalimbali wameendelea kuwasilisha misaada, hivyo serikali itaendelea kuwataarifu kufika katika vituo kupokea misaada kwa kadri itakavyokuwa inawasilishwa kwa sababu waathirika wa maafa ndio wanufaika wakuu wa misaada hivyo.
Amesema kuwa pamoja na misaada ya kibinadamu, serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu inaendelea pia kuratibu ugawaji wa mbegu za kisasa pamoja na mbolea kwa wanachi ambao mashambao yao waliharibiwa na maporomoko ya tope zito lililochanganyika na mawe na magogo kutoka Mlima Hanang.