Mkurugenzi wa uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) Dk Athumani Kihamia amesema msimamizi wa uchaguzi Jimbo la Buyungu mkoani Kigoma ataendelea kutekeleza majukumu yake kwa kuwa malalamiko yaliyotolewa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ya kumkataa hayakufuata taratibu za kisheria.
Awali, Chadema walitoa taarifa ikilalamikia kasoro zilizopo katika jimbo hilo ikiwamo msimamizi wa uchaguzi kutotangaza orodha ya majina ya wanaokusudia kuwateua kuwa wasimamizi na wasimamizi wasaidizi wa vituo vya kupiga kura.
Pia, walilalamika kuwa msimamizi huyo hajatangaza orodha ya wapigakura vituoni.
“Sheria inaagiza majina hayo yanapaswa kubandikwa siku nane kabla ya siku ya kupiga kura ili wananchi wapate ruhusa ya kuhakiki majina na vituo vyao,” inaeleza taarifa ya Chadema.
Akitoa ufafanuzi huo jana, Dk Kihamia alisema malalamiko hayo hayana msingi wa kisheria kwa sababu hayakupelekwa kama rufaa ila yametolewa kama malalamiko.
“Kwa maana hiyo napenda kuwajulisha umma kwamba malalamiko haya hayamuondolei sifa msimamizi wa uchaguzi kwa kumuondoa kusimamia shughuli za uchaguzi Jimbo la Buyungu.
“Kwa kuwa Chadema wamelalamika kwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi na malalamiko hayo wameyaleta kama barua, (hivyo) walipaswa wayalete ndani ya muda unaokubalika ambao ni saa 48 tangu kupokea hizo taarifa,” alisema.
Wakati huohuo; mkutano wa kumnadi mgombea udiwani Kata ya Turwa, (Chadema) umeshindwa kufanyika baada ya polisi kuwatanya kwa mabomu ya machozi wafuasi wa vyama vya upinzani waliohudhuria mkutano huo. Hata hivyo, Kamanda wa polisi mkoa wa Mara, Henry Mwaibambe hakupatikana kuzungumzia suala hilo.
Katika tukio hilo, mbunge wa Tarime Mjini, Esther Matiko na wananchi wengine zaidi ya 10 walidaiwa kukamatwa na polisi.
Kiongozi wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe alisema kwamba alikwenda kituo cha polisi kwa ajili ya kumuona Matiko lakini polisi walimzuia.