Tume ya Taifa ya Uchaguzi imewataka Watendaji wa Uboreshaji wa Majaribio wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura katika Halmashauri ya Wilaya ya Rorya Mkoa wa Mara kuweka utaratibu mzuri utakaoviwezesha vyama vya siasa na wadau wengine wa uchaguzi kushiriki katika uboreshaji katika Kata ya Ikoma.
Akifungua mafunzo kwa watendaji hao yaliyofanyika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Wilaya ya Rorya, Mjumbe wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Jaji wa Rufaa Mhe. Mwanaisha Kwariko alisema vyama vya siasa vinaruhusiwa kuweka mawakala katika uboreshaji huo.
Aliwataka watendaji hao kuvishirikisha vyama vya siasa katika masuala yote ambayo wanastahili kushirikishwa kwani jambo hilo litawarahisishia utekelezaji wa majukumu yao katika uboreshaji huo.
“Niwakumbushe kuwa, vyama vya siasa vinaruhusiwa kuweka mawakala katika vituo vya uandikishaji. Nitumie nafasi hii kuwasisitiza kuweka utaratibu mzuri utakaoviwezesha vyama vya siasa na wadau wengine wa uchaguzi kushiriki kikamilifu katika zoezi hili” alisema Jaji wa Rufaa Mhe. Mwanaisha Kwariro.
Mjumbe huyo wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi alitoa wito kwa watendaji hao wa uboreshaji wa majaribio kuhakikisha kuwa wanafanya kazi kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na Maelekezo ya Tume watakayopewa.
“Vilevile mhakikishe mnasimamia utunzaji wa vifaa vyote vitakavyotumika katika zoezi hili kwani vimenunuliwa kwa gharama kubwa” aliongeza Jaji wa Rufaa Mhe. Mwanaisha Kwariko.
Mafunzo hayo kwa watendaji wa uboreshaji wa majaribio wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura unajumuisha Mratibu wa Uandikishaji wa Uchaguzi wa Mkoa wa Mara, Afisa Mwandikishaji wa Jimbo la Rorya, maafisa waandikishaji wasaidizi, maafisa ugavi, maafisa TEHAMA na maafisa wanaoshughulikia masuala ya uchaguzi katika Jimbo la Rorya.
Tume ya Taifa ya Uchaguzi itafanya uboreshaji wa majaribio wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura katika Kata ya Ikoma iliyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Rorya, Mkoa wa Mara na Kata ya Ng’ambo iliyopo katika Halmashauri ya Manispaa ya Tabora, Mkoa wa Tabora, kuanzia tarehe 24 hadi 30 Novemba, 2023.