Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dodoma
Tume ya Taifa ya Uchaguzi imetoa vibali vya kutoa Elimu ya Mpiga Kura katika Uchaguzi Mdogo wa Ubunge jimbo la Mbarali na kata sita za Tanzania Bara kwa asasi tatu za kiraia.
Taarifa ya Tume iliyosainiwa na Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Ramadhani Kailima imesema uamuzi huo umefikiwa baada ya Tume kukutana katika kikao chake leo Agosti 17,2023 jijini Dodoma.
“Tume imefikia uamuzi huo kwa kuzingatia kifungu cha 4C cha sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura 343 na kanuni ya 3 ya Kanuni za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa (Uchaguzi wa Madiwani) za mwaka 2020, inayoipa Tume jukumu la kutoa elimu ya mpiga kura nchi nzima, kuratibu na kusimamia taasisi na asasi za kiraia zinazotoa elimu hiyo,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo.
Kailima amezitaja asasi za kiraia zilizopata kibali cha kutoa elimu ya mpiga kura na maeneo watakayotoa elimu hiyo kuwa ni Alpha and Omega Reconciliation and Peace Building (AREPEB), itakayotoa Elimu Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali katika Jimbo la Mbarali, Umbrella of Women and Disabled Organisation (UWODO) itakayotoa Elimu Halmashauri ya Wilaya ya Madaba katika Kata ya Mtyangimbole na Bright Child Development Tanzania (BRIGHT CHILD), Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi katika Kata ya Mwaniko.
Aidha, Tume imetoa kibali cha utazamaji kwa Asasi ya kiraia ya Bridge Development Trust Organization (BRIDETO) ambayo iliomba kutazama uchaguzi mdogo katika Kata ya Mwaniko iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi na Kata ya Nala katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma.
Kailima amesema katika taarifa hiyo kuwa, Tume imefikia uamuzi huo wa kutoa kibali hicho kwa kuzingatia kanuni ya 16(5) ya Kanuni ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa (Uchaguzi wa Madiwani) za mwaka 2020
Amesema katika utekelezaji wa jukumu la kutoa elimu ya mpiga kura, asasi hizo zitapaswa kuzingatia Mwongozo wa Elimu ya Mpiga Kura wa Mwaka 2020 katika kipindi chote cha kutoa elimu hiyo katika uchaguzi mdogo.
Kwa mujibu wa ratiba ya uchaguzi mdogo iliyotolewa na Tume, uteuzi wa wagombea katika uchaguzi huo utafanyika Agosti 19, 2023 na Agosti 20 hadi Septemba 18, 2023 kitakuwa ni kipindi cha kampeni kwa vyama vya siasa na wagombea, na Jumanne ya Septemba 19, 2023 itakuwa ni siku ya uchaguzi.
“Tume inatumia fursa hii kuzipongeza asasi zote za kiraia zilizopata kibali cha kutoa elimu ya mpiga kura na utazamaji wa uchaguzi, na inazikumbusha asasi hizo kuzingatia sheria, kanuni, taratibu, miongozo na maelekezo ya Tume katika kipindi chote cha utekelezaji wa majukumu yao. ” alisema Kailima katika taarifa hiyo.
Kwa mujibu wa Tume vibali hicho kitatumika kuanzia tarehe Agosti 18, 2023 hadi Septemba 18, 2023.