Katika makala zangu zilizopita, nilieleza kwa kina jinsi vyama vinavyokaa madaraka kwa muda mrefu katika nchi za Kiafrika, vilivyojizatiti kuhakikisha kwa gharama yoyote ile vinaendelea kuongoza hata kwa njia zisizokuwa za kidemokrasia.
Nilitaja mitaji mikubwa ya vyama hivyo vikongwe vinavyojihakikishia kutawala maisha ni rushwa, vyombo vya dola na tume za uchaguzi zilizokosa uhuru na kuegemea upande mmoja wa chama kinachotawala. Pia, ujinga na umaskini uliokithiri kwa wananchi wa mataifa hayo.
Tangu joto la uchaguzi lilipoanza nchini, minyukano iliyogubikwa na hila za kila namna kutoka CCM kushindwa kutimiza ndoto za kuwaletea maendeleo kiuchumi, kielimu na kiafya kwa zaidi ya miaka 50.
Sifa ya CCM imebaki kuwa moja tu ya kuwaunganisha Watanzania ambao wanaishi kama ndugu wakiheshimiana na kuthaminiana, jambo lililoasisiwa na mtu wa watu na kipenzi cha watu, aliyechukia ubaguzi, dhuluma, chuki na ufisadi, Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
Lakini CCM ya Mwalimu Nyerere ni tofauti kabisa na hii ya sasa ambayo ilianza kujaa nyufa tangu utawala wa awamu ya pili chini ya Mzee Ali Hassan Mwinyi, baada ya kulizika Azimio la Arusha kwa kuanzisha lile la Zanzibar ambalo ndiyo chimbuko la ufisadi, ongezeko la rushwa, wizi wa mali za umma na ubaguzi wa matabaka baina ya wanaofaidi keki ya Taifa na wale ambao hawatakiwi hata kuikaribia.
Chama chetu kimeendelea kuwa na rekodi mbaya sana kwa awamu zote na hii ya nne chini ya Mwenyekiti, Jakaya Kikwete, imekuwa na madudu ya aina yake pengine kuliko zilizopita.
Kutokana na madudu haya, imekuwa vigumu kwa mgombea wetu wa urais kukinadi chama chetu na sasa amekuja kama mgombea binafsi: ‘ Chagua Magufuli’,’ Mchapakazi’, ‘Muadilifu’ na kadhalika. Mgombea wetu anaona kutamka CCM mbele ya umati ni sawa na kumnadi shetani kuwatawala Watanzania.
Ni wazi kwamba Dk. John Pombe Magufuli akifanikiwa kupenya katika tundu la sindano na kuwa rais wa awamu ya tano, hatakwenda kinyume na maelekezo ya chama kilichompa nafasi ya kutawala ambayo hakuitarajia kutokana mwenendo wa chama hicho.
Naye yule kada namba nane wa CCM aliyechomoka na kukimbilia mabadiliko mwishoni mwa wiki iliyopita, Mzee Kingunge Ngombale-Mwiru, huku akikiponda chama hicho kwamba kinaongozwa kwa ubabaishaji bila kuheshimu Katiba, akatoa kioja kwamba sasa kumekuwa na ‘kidumu Chama Cha Mapinduzi’ na ‘kidumu chama tawala’ ambako duniani hakuna kitu kinachoitwa ‘chama tawala’.
Uchaguzi huu unafanyika mara ya nne bila Mwalimu Nyerere huku wimbi kubwa la wananchi wanaotaka mabadiliko, likishika kasi na kukitikisha Chama Cha Mapinduzi kinachotumia hila mbalimbali kujinasua na anguko la aibu na kishindo kikubwa, kwa kujaribu kuusambaratisha umoja wa vyama vinavyopigania Katiba ya Wananchi (UKAWA).
Wamefanikiwa kuwanunua baadhi ya viongozi wa Ukawa akiwamo Profesa Ibrahim Lipumba, aliyekuwa Mwenyekiti wa CUF, aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Willibrod Slaa, na kukiingia chama cha NCCR-Mageuzi kwa ‘kumrubuni’ Makamu Mwenyekiti wake, Leticia Masore, kwa lengo hilo hilo la kuusambaratisha umoja huo.
Uandikishaji wapiga kura mafichoni unaofanywa kwa kuthubutu kuibeba CCM, ili walanguzi waendelee kutafuna keki ya ‘wapumbavu na malofa’ kama ulionaswa katika kiwanda cha MMI Steel cha Dar es Salaam, baada ya kuwapo kwa taarifa kuwa mashine ya kusajili wapiga kura kwa mfumo wa kielektroniki (BVR) inatumika kuandikisha wafanyakazi katika kiwanda hicho na vyama kutopewa nakala ya daftari la wapiga kura, kumeibua hofu iwapo Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) inaweza kutenda haki.
Mwenendo mzima wa NEC, Polisi na CCM unaashiria kwa makusudi mazima kuwa washirika hao watatu wana nia ya kuvuruga amani ya nchi kwa mwenendo wao na kauli zao. Wananchi wapenda amani kushiriki uchaguzi ni haki ya kila mmoja na kuhakikisha kura zao ziko salama ni haki yao kwa sababu ya kukosa imani na taasisi hizo.