Na Mwamvua Mwinyi,JamhuriMedia,Kibaha
Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Adolf Ndunguru, amewasihi wauguzi wa kada ya utabibu,wakunga na wauguzi kutumia mitandao ya kijamii vizuri bila kwenda kinyume na maadili ya fani yao na nchi kijumla.
Aidha kakemea lugha chafu,kejeli kwa wagonjwa ili kuheshimisha kada hiyo.
Alitoa wito huo kwa wahitimu 106 wa mahafali ya 56 wa taaluma ya utabibu na uuguzi, katika Chuo Cha Afya na Sayansi Shirikishi Kibaha ,Mkoani Pwani yaliyofanyika Julai 28 mwaka huu.
Ndunguru aliwataka kutumia mitandao ya kijamii kupata maarifa,na kupanua wigo wa kutoa huduma bora za kiafya.
Alisisitiza,kutoa huduma bora kwa kutumia weledi unaozingatia taaluma badala ya kutekeleza wajibu wenu kwa maslahi ya fedha.
“Fani hii inazingatia maisha na uhai wa binadamu haufidiwi na Chochote,mmepewa dhamana kubwa kulinda afya za binadamu kupitia elimu mliyoipata”Anasema Ndunguru.
Kuhusu changamoto za uchakavu wa baadhi ya miundombinu Chuoni hapo, Ndunguru amewahakikishia watafanya kila linalowezekana kutafuta raslimali fedha za kutosha kuboresha miundombinu hiyo.
Kuhusiana na mikopo kwa Vyuo vya kati alifafanua, Katika bajeti ya Serikali 2023-2024 imeanzisha Utaratibu wa kutoa mikopo Vyuo vya kati eneo la teknolojia,afya na sayansi.
Awali Mkurugenzi wa Shirika la elimu Kibaha , Robert Shilling alieleza,Chuo hicho kinakabiliwa na changamoto kubwa ya uchakavu wa majengo kongwe, yaliyojengwa miaka 56 iliyopita.
Shilling alieleza licha ya changamoto hizo, wanaishukuru Serikali chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutoa Bilioni 1.200 ndani ya miaka miwili ya uongozi wake ili kutekeleza miradi ya maendeleo.
Nae Mkuu wa Chuo Tusekile Solile alibainisha , ipo mikakati waliyojiwekea kupanua chuo kwenye eneo lenye ukubwa wa ekari 100 ,kwa gharama ya Bilioni 17.
Alisema ,eneo hilo litaongezwa ujenzi wa hostel, madarasa mengine,bwalo,maabara, nyumba za watumishi ili kuongeza eneo la kujifunzia.
Chuo cha afya na sayansi shirikishi Kibaha ni miongoni mwa vyuo vya afya ngazi ya kati ,ni sehemu ya Shirika la Elimu Kibaha lilianzishwa mwaka 1963 kwa ushirikiano kati ya Serikali ya Tanganyika na nchi za Kinordic .