Na Mwandishi Wetu,JamhuriMedia,Arusha
WADAU wa habari nchini wameshauriwa kuweka nguvu za pamoja katika harakati za kutafuta mabadiliko ya sheria ya habari ambazo zimekuwa kikwazo.
Ushauri huo umetolewa na Waziri wa Katiba na Sheria, Dk.Damas Ndumbaro wakati akizungumza na viongozi wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) pamoja Wadau wa Haki ya Kupata Habari (CoRI) mkoani Arusha.
Amesema kuwa huu ni muda mzuri katika kuomba mabadiliko ya sheria ambazo zimekuwa haziendani na utendajikazi wa sekta hiyo kwa kuwa hata Rais Samia Suluhu Hassan ameonyesha nia.
“Wote tunafahamu kuwa rais wetu Samia Suluhu Hassan ameonesha moyo mkubwa wa kutetea na kutoa haki za vyombo vya habari na waandishi wa habari nchini.
“Hivyo ni wakati sasa wa kusimamia suala hili sheria zibadilishwe sasa hivi, kwani mkisubiri miaka 10 ijayo,hamuwezi kujua atakayekuja baada ya hapo atakuwa na mtazamo gani juu ya vyombo vya habari,” amesema Dkt. Ndumbaro.
Hata hivyo waziri Ndumbaro amekubaliana na hoja za TEF na wadau kuwa suala la Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO) nchini kuwa na mamlaka ya kuwa mlalamikaji, mwendesha mashitaka, mtoa hukumu na msimamizi wa hukumu aliyoipitisha linafifisha misingi ya utawala bora na utawala wa sheria hivyo hili ni moja ya mambo yanayopaswa kubadilishwa.
“Hili la dispute settlement (utatuzi wa migogoro), linahitaji uwazi mkubwa. Kuna hatari kubwa katika kuweka madaraka yote kwenye chombo kimoja [Mkurugenzi wa Idara ya Habari/MAELEZO…] nafahamu sheria ililenga ku-balance conflicting interests (kuweka mlinganyo kwa maslahi yanayogongana), maana serikali zote duniani huwa zinawaza kudhibiti.” amesema.
Amesema kuwa ndiyo maana kilianzishwa chombo kama Mahakama ambayo ina jukumu la kusikiliza kila upande wenye malalamiko na kuamua nani anastahili haki ipi, hivyo akasema mamlaka ya kufungia chombo vya habari hayapaswi kuwekwa kwenye mikono ya mtu mmoja.
“Ni vyema likawapo Baraza la Usuluhishi. Fair Competition (ushindani wa haki) hazitegemei mtu mmoja.
Kunakuwapo na jopo linalofanya uamuzi. Tuunde vyombo na tuhakikishe sheria hizi tunatengeneza mfumo utakaodumu miaka mingi,” amesema na kurejea mfano wa Serikali ya Marekani iliyotoka kulifungia gazeti la Washington Post miaka ya 1970 kwa kuchapisha nyaraka zilizoonyesha kuwa Serikali ya Marekani haikufuata utaratibu katika kuingia vitani na Vietnam, ila Mahakama ilipopitia ushahidi wa pande zote mbili, ililiruhusu gazeti hilo liendelee kuchapisha taarifa hizo.
Ameongeza kuwa imethibitika kuwa baadhi ya nchi duniani hutumia mwavuli wa kudai kuwa wanazuia baadhi ya taarifa kwa sababu za usalama wa taifa, lakini taarifa nyingi huwa zinazuiwa kukinga maovu ya watu binafsi yasifahamike suala lisilohusiana na usalama wa taifa.
“Ni kweli masuala yanayohusu usalama wa taifa lazima yalindwe, lakini si kulinda maovu ya watu binafsi yakafichwa kwenye mwavuli wa usalama wa taifa… tunapaswa kutunga sheria zetu zenye viwango na zitakazodumu kwa muda mrefu.Wakati ni huu.
Pia amemsifia Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye ambaye ni mwanahabari na ameonyesha nia ya kusimamia mabadiliko ya sheria hizo, hivyo ameshauri Jukwaa la Wahariri Tanzania na wadau kuhakikisha wanazungumza kwa karibu na Waziri Nape.
Ameahidi yeye na wabunge wengine watashiriki kikamilifu katika kusaidia Tanzania ikapata sheria nzuri za habari, kwani sheria nzuri za habari zitawezesha kukuza haki ya kupata habari, uhuru wa vyombo vya habari na haki ya watu kutoa maoni itakayozalisha maendeleo ya haraka kwa nchi.
Vyombo vya habari vipo katika mazungumzo na serikali kuomba Sheria ya Huduma za Habari, MSA 2016 irekebishwe katika vifungu vinavyofifisha Uhuru wa Vyombo vya Habari kikiwamo kifungu cha 9(a) kinachompa Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO) mamlaka ya kufungia vyombo vya habari bila kupitia utaratibu wa kuwasilisha malalamiko popote au pande zote mbili zilizo katika mgogoro kusikilizwa.
Jukwaa la Wahariri Tanzania na wadau, wanapendekeza mamlaka haya ya Mkurugenzi yafutwe na kiundwe chombo ambacho pamoja na mambo mengine kitashughulikia masuala ya usuluhishi yanapotolewa malalamiko dhidi ya chombo cha habari, badala ya kazi hiyo kufanywa na mtu mmoja.
Sheria nyingine zinazolalamikiwa ni Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Huduma za Posta (EPOCA, 2010), Sheria ya Makosa Mtandaoni (2015), Sheria ya Haki ya Kupata Habari (2016) na Kanuni za Maudhui Mtandao (2018) kama zilivyorekebishwa mara kadhaa. Sheria hizi zina vifungu vinavyofifisha uhuru wa habari nchini hivyo zinahitaji kubadilishwa.