Na Cresensia Kapinga, JamhuriMesia, Songea

Waziri wa Utamaduni, Michezo na Sanaa Dkt. Damas Ndumbaro, amesema kuwa kuna umuhimu mkubwa wa kuonesha utamaduni wa Taifa letu , kuimarisha umoja na kujivunia urithi wetu wa kitamaduni.

Hayo yamebainika jana wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana Tamasha la tatu la utamaduni la Taifa linalofanyika mkoani humo.

Ndumbaro amesema kuwa katika kipindi hiki Cha kuelekea kwenye kilele Cha Tamasha la tatu la utamaduni la Taifa shughuli mbalimbali zinaendelea kufanyika ikiwemo maonesho ya sanaa, michezo,na vikao vya mijadala kuhusu maendeleo ya utamaduni.

Waziri Dkt. Ndumbaro mbaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Songea mjini amesema kuwa lengo kuu la Tamasha hilo ni kuleta pamoja watu kutoka sehemu mbalimbali za nchi na kujadili jinsi ya kukuza na kulinda utamaduni wa Taifa.

Hata hivyo Dkt. Ndumbaro amewaomba wananchi wa Mkoa wa Ruvuma kujitokeza kwa wingi katika uwanja wa majimaji mbapo zitafanyika shughuli za kilele Cha Tamasha la tatu la utamaduni la Taifa kuanzia Septemba 20 mwaka huu.

Alisema kuwa mgeni rasmi katika kilele hicho atakuwa Raisi wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan hivyo amewataka wananchi wajitokeze kwa wingi kuanzia kwenye mapokezi hadi eneo la tukio ambako utafanyika uzinduzi Rasmi wakuanza kwa sherehe hizi za utamaduni kitaifa,ambazo zitaambaatana na matukio mbalimbali ya kimila,desturi na tamaduni za Mtanzania.

“Ili tuweze kuzindua tamasha hili tunahitaji watu wajitokeze kwa wingi ili Rais wetu wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan akiona kwenye vyombo vya Habari aupe tano Mkoa wetu na ajisikie kuthaminiwa na kuhamasika zaidi kuja mkoani kwetu.” Amesema Dkt. Ndumbaro.

Amesema kuwa pamoja na kuwa mgeni rasmi Raisi Dkt.Samia Suluhu Hassan kwenye kilele cha Tamasha la Tatu la Utamaduni la Kitaifa hapa Mkoani Ruvuma lakini pia anatarajia kufanya ziara katika Mkoa wa Ruvuma ambapo atatembelea Halmashauri zote 8 za Mkoa huu wa Ruvuma pamoja na kufanya mikutano ya hadhara kwenye halmashauri hizo.

Aidha amewaomba wananchi kujitokeza kwa wingi kwenye Tamasha hilo na kuwakumbusha kwamba ni tamasha la kitaifa watu zaidi ya 5,000 wanatarajia kuwepo kutoka Mikoa mbalimbali hapa nchini Tamasha ambalo kitaifa mwaka huu linafanyika mkoani Ruvuma.

Please follow and like us:
Pin Share