Na Stephano Mango,JamhuriMedia, Songea

Waziri wa Katiba na Sheria ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Songea Mjini Dkt.Damas Ndumbaro amewataka waandishi wa Habari hapa Nchini kupambana na mifumo kandamizi ya ukatili wa kijinsia na kuwa mstari wa mbele kuhakikisha wanafanya uendelevu wa kuibua,kuandika na kuripoti taarifa za matukio ya vitendo vya ukatili Kwa jamii.

Dkt Ndumbaro ameyasema hayo jana mjini hapa wakati akizungumza na waandishi kutoka katika wilaya zote za Mkoa wa Ruvuma wanaoshiriki warsha ya siku mbili kuhusu ukatili wa kijinsia.

Dkt Ndumbaro amesema kuwa washiriki wa mafunzo haya wanatakiwa kuandika na kuibua vitendo vya ukatili wa Kijinsia na kwamba kwa waandishi 3 watakaofanya vizuri katika uandishi wa Taarifa anuai watapata zawadi mbalimbali

Amesema kuwa katika kuelekea Uzinduzi wa kampeni ya Mama Samia Legal Aid itakayofanyika Julai 22 katika uwanja wa Majimaji Mjini Songea Mkoani Ruvuma ,na baada ya uzinduzi huo utoaji elimu utaendelea Kwa muda wa siku 10, hivyo Waandishi wanatakiwa kuhabarisha Umma juu ya Kampeni hiyo.

Ameeleza kuwa Waandishi watatu ambayo watakaoshinda kuripoti vizuri taarifa hizo Wizara ya Katiba na Sheria itawazawadia fursa mbalimbali ikiwemo fedha taslimu ,Medali pamoja na kupata nafasi ya kuwa Balozi wa kupinga ukatili wa Kijinsia Kwa wananchi,na pia Balozi huyo atapata fursa ya kwenda Kwenye mikoa mbalimbali hapa Nchini akiwa ameambatana na maafisa wa Wizara ya Katiba na Sheria.

Warsha hiyo ya siku mbili imefadhiliwa na Serikali kupitia wizara ya Katiba na Sheria,na mwezeshaji wa warsha hii ya ukatili wa kijinsia ni Dkt.George Chambua ambaye ni Mbobezi wa masuala ya GBV.

Kwa upande wake Mratibu wa Mafunzo hayo George Mollel ameitaja Kampeni ya Huduma ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia kuwa inalenga kulinda na kukuza haki ya upatikanaji haki kupitia huduma za msaada wa kisheria nchini

Mollel amesema kuwa kampeni inatarajia kuboresha upatikanaji wa haki kwa watu wasiojiweza hususan wanawake,Watoto na makundi mengine yaliyo katika mazingira magumu,kampeni itachangia kuimarisha amani na utulivu na kuleta utengamano wa kitaifa

Amesema kuwa elimu ya kisheria italenga katika masuala ya ukatili wa kijinsia,migogoro ya ardhi,mirathi,usuluhishi kwa njia mbadala,mifumo ya kisheria na masuala yahusuyo haki za binadamu kwa ujumla.

Please follow and like us:
Pin Share