Ndugu wa aliyekuwa Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mwanza, Liberatus Barlow aliyeuawa kwa kupigwa risasi, wamesema wanataka majibu ya kina kutoka kwa Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, Said Mwema.

Akizungumza na Jamhuri, mdogo wa Barlow, Christian Lyimo mwishoni mwa wiki, alisema anazungumza mara kwa mara na IGP Mwema lakini majibu anayopewa hayamridhishi.

 

“Kimsingi hatuoni kasi ya hicho kinachoitwa kesi. Alipouawa [Imran] Kombe tulikuwa tunasikia taarifa za kina zikitolewa juu ya maendeleo ya kesi. Lakini hili la kaka yangu Barlow sisi kama wanafamilia hatuambiwi chochote.

 

“Tangu mauaji yametokea Oktoba mwaka jana, hatujasikia kesi inaendeleaje na wala sisi ndugu hatujaitwa kuonyeshwa hao watuhumiwa wa mauaji ya kaka yetu. Nimewasiliana mara kwa mara na Mwema, lakini anasema atanijulisha ila hakuna kinachoendelea.

 

“Mimi nataka nikutanishwe na hao waliomuua wanieleze walikuwa wametumwa na nani na kwa minajili ipi walimuua. Yananikera maneno yaliyaondikwa na gazeti la kila siku (jina linahifadhiwa) kuwa aliuawa kwa sababu ya mapenzi na rushwa.

 

“Mimi nimemfahamu kaka yangu [Barlow] alikuwa hali rushwa na wala hajihusishi na masuala ya mapenzi. Sisi tulikuwa tunalima mashamba hadi ekari 200 tunavuna mazao na kuuza hivyo kama asingeweza kujiingiza kwenye masuala ya rushwa.

 

“Nasema damu ya kaka yangu haitamwagika hivi hivi. Sisi ni familia ya imani, tunaomba kwa Mungu na wote walioshiriki kumuua watapata ugonjwa ambao hawatapona. Nataka Mwema atujulishe kama familia mwenendo wa kesi umefikia wapi?” alisema Lyimo.

 

Kuhusu kijana Mohamed Malele aliyeko Hospitali ya Taifa Muhimbili, alisema maneno yaliyosemwa na kijana huyo si ya kupuuzwa.

 

“Huyu kijana alisema wazi kuwa alitakiwa akamuue kaka yangu yeye akakataa. Sasa nasema, hapo Muhimbili anafanya nini? Kama ni kichaa kweli si apelekwe Mirembe Dodoma?” alihoji Lyimo.

 

Inaelezwa kuwa kati ya waliomuua Barlow mmoja wa walioshiriki mauaji hayo alikwenda uwanjani kuaga mwili wa Barlow. Mtu mmoja aliyekuwa anakimbilia Uganda kwa kutumia boti alikamatwa na kwa sasa inadaiwa kuwa watuhumiwa wanane wako ndani kuhusiana na tukio hilo.

 

Hata hivyo, Lyimo anasema kasi ya upelelezi hairidhishi na familia haifahamishwi chochote kinachoendelea, hivyo wanapata wasiwasi kuwa huenda kesi ya ndugu yao ikaishia hewani ndio maana wanataka IGP Mwema atoe kauli kueleza kinachoendelea.